Widodo ashinda uchaguzi wa urais Indonesia | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.07.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Widodo ashinda uchaguzi wa urais Indonesia

Gavana wa jimbo la Jakarta, Joko Widodo, ameshinda katika uchaguzi wa urais nchini Indonesia ambacho kilikuwa kinyang'anyiro kikali kati yake na mkuu wa zamani wa majeshi Prabowo Subianto.

Widodo ambaye anajulikana kwa jina la utani Jokowi ameshinda uchaguzi huo uliofanyika tarehe tisa mwezi huu kwa asilimia 53 dhidi ya Pabowo Subianto aliyepata asilimia 47 ya kura kulingana na matokeo kamili yaliyotolewa leo katika taifa hilo la tatu kwa ukubwa kidemokrasia.

Matokeo hayo yanakuja saa chache tu baada ya Prabowo ambaye hapo awali alikuwa amedai pia kushinda katika uchaguzi huo kutangaza kuwa anajiondoa kutoka kinyanga'nyiro hicho kwasababu zoezi hilo lilikumbwa na udanganyifu mkubwa wa kura.

Prabowo asema kulikuwa na udanganyifu

Prabowo mwenye umri wa miaka 62 alitarajiwa kupinga matokeo hayo katika mahakama ya kikatiba iwapo hangetangazwa mshindi lakini wakili wake amewaambia wanahabari hawana tena nia hiyo kwani hawana misingi yoyote kisheria kufanya hivyo baada ya kujiondoa kutoka kinyang'anyiro hicho.

Wagombea urais wa Indonesia Prabowo Subianto na Joko Widodo

Wagombea urais wa Indonesia Prabowo Subianto na Joko Widodo

Hatua hiyo ya kuijondoa kwa Prabowo sasa kunaepusha mgogoro wa kisheria na kisiasa kuhusu uchaguzi huo mkuu. Licha ya madai ya Prabowo kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu mwingi wa kura,waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi huo wamesema zoezi hilo liliendeshwa kwa njia ya huru na haki.

Ushindi wa Widodo ambaye alizaliwa katika kitongoji duni na ambaye wakati mmoja alikuwa anauza samani nje ya nchi, unatarajiwa kupokelewa vyema na wawekezaji nchini humo kwani wanatumai ataleta nguvu mpya katika uchumi wa taifa hilo lililo na watu milioni 240 na lenye waislamu wengi zaidi duniani ambalo uchumi wake umekuwa ukizorota hivi karibuni.

Widodo atajwa mtu wa watu

Gavana huyo wa Jakarta ndiye mgombe wa kwanza wa urais nchini Indonesia ambaye hana mafungamano na kiongozi wa zamani wa kiimla Suharto ambaye aliiongoza nchi hiyo kwa maiaka 30 kabla ya kupinduliwa kushinda uchaguzi moja kwa moja.

Gavana wa Jakarta Joko Widodo ameshinda uchaguzi wa rais

Gavana wa Jakarta Joko Widodo ameshinda uchaguzi wa rais

Licha ya kuwa Widodo hana tajriba kubwa kuhusu siasa za kitaifa, amejijengea jina kama mtu wa watu na kiongozi muadilifu anayetaka mabadiliko ya kidemokrasia akiyadhihirisha hayo alipochaguliwa mwaka 2012 kuwa gavana wa mji mkuu wa Indonesia, Jakarta.

Miongoni mwa mambo yanayompa sifa nzuri ni kuwa hana doa la kuhusishwa na watu wenye ushawishi jeshini na katika biashara nchini humo ambao wameiendesha Indonesia kwa miongo kadhaa.

Tume ya uchaguzi nchini humo imesema idadi ya wapiga kura waliojitokeza ilikuwa asilimia 70,idadi ambayo imeshuka kidogo ikilinganishwa na uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2009 ambapo asilimia 72 ya wapiga kura walishiriki.

Mwandishi:Caro robi/Afp/Ap

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com