1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Westerwelle-Balkans

Saumu Ramadhani Yusuf26 Agosti 2010

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ameitolea mwito Serbia kukoma kuupinga uhuru wa jimbo la Kosovo na badala yake ijishughulishe zaidi katika kuwania kujiunga na Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/OxCH
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani akifanya mazungumzo SerbiaPicha: AP

Akiwa katika ziara yake ya kwanza kwenye nchi hiyo ya eneo la Balkans amezungumzia juu ya msimamo wa Ujerumani wa kutokubaliana na azimio la Serbia ililoliwasilisha mbele ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa.Azimio hilo linataka pafanyike mazungumzo zaidi  juu ya suala la uhuru wa Kosovo ambao unapingwa hadi sasa na Serbia pamoja na washirika wake.

Superteaser NO FLASH Serbien Deutschland Guido Westerwelle bei Boris Tadic in Beograd
Rais Boris Tadic, wa Serbia akisalimiana na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido WesterwellePicha: AP

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle akiwa nchini Serbia hii leo ameitaka nchi hiyo kukubaliana na ukweli wa mambo kwamba imelipoteza jimbo lake la zamani la Kosovo,akisema uhuru wa jimbo hilo ni wa halali na ulio  wazi kabisa.Mjini Belgrade Westerwelle amewatolea mwito viongozi wa Serbia kulifutilia mbali azimio lao dhidi ya uhuru wa Kosovo ambalo wanatarajia kulipitisha  katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mnamo mwezi wa Septemba.

Waziri Westerwelle ameiambia Serbia  kwamba itakuwa jambo la busara zaidi ikiwa nchi hiyo itaachana na azimio lake na kuanzisha mazungumzuo na jimbo hilo akisisitiza kwamba maridhiano ndio njia pekee inayoweza kufanikiwa ikiwa upande mmoja haukubaliani na ukweli wa mambo.

Serbia inapanga  kutafuta uungaji mkono wa azimio lake  ambalo limewatia katika mvutano na  Marekani pamoja na Umoja wa Ulaya.Nchi 22 za Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani zinautambua uhuru wa Kosovo. Azimio la Serbia linalaani hatua ya Kosovo ya kujitangazia uhuru ingawa mahakama ya sheria ya kimataifa ICJ mwezi wa July ilitangaza hatua hiyo ya Kosovo kuwa halali  na kutaka paanzishwe upya mazungumzo  juu ya suala hilo.

Msimamo  wa mahakama ya ICJ  ulifikishwa katika Umoja wa mataifa na serikali ya Kosovo inatarajia kwamba baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litaunga mkono uhuru wake licha ya upinzani wa  Serbia.

Aidha waziri wa mambo ya nje Westerwelle akizungumza katika chuo kikuu cha Belgrade amesema kwamba Serbia kama nchi nyingine za magharibi za eneo la Balkan zina nafasi ya kujiunga  katika Umoja wa Ulaya  ingawa ameonya kuwa safari ya kuelekea katika chombo hicho ni ngumu na nzito.

NO FLASH Kosovo ist Serbien Graffiti
Nchi 69 zinautambua uhuru wa Kosovo ikiwemo zenye nguvu isipokuwa Urussi na ChinaPicha: AP

Baada ya mazungumzo na waziri mkuu Mirko Cvetkovic Westerwelle alisema kwamba mustakabali wa  nchi za balkans utatokana na Umoja wa Ulaya lakini akasisitiza kwamba Umoja huo hauwezi kuwakaribisha wanachama ambao wanachochea mizozo ya nje.Ujerumani iko tayari kuwa mpatanishi katika mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Serbia na Kosovo ili kuutatua mvutano uliopo.Uhuru wa Kosovo umetambuliwa na nchi 69 ikiwemo nchi zenye nguvu duniani isipokuwa Urussi na China.

Waziri huyo wa Ujerumani aliwasili Belgrade leo asubuhi akitokea Zagreb na amepangiwa kuelekea Bosnia baadae hii leo na  hatimae kuitembela Kosovo hapo kesho ijumaa kituo chake cha mwisho katika ziara yake hiyo ya nchi za iliyokuwa Yugoslavia.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri Josephat Charo