Westerwelle atangaza sera mpya ya Ujerumani | Magazetini | DW | 10.02.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Westerwelle atangaza sera mpya ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya kukamatwa Katibu Mkuu wa chama cha upinzani nchini Kongo Jacquemain Shabani. Pia yameandika juu ya mvutano wa kisiasa nchini Senegal baada ya Rais Wade kuruhusiwa kugombea

German Foreign Minister Guido Westerwelle gestures during a statement in Berlin, Germany, Thursday, Feb. 9, 2012. Germany says it is expelling four Syrian diplomats following the arrest earlier this week of two men accused of spying on Syrian opposition groups in Germany. Westerwelle said in the statement, that he ordered the expulsions of the four Syrian Embassy employees, and that the ambassador had been informed. (Foto:Gero Breloer/AP/dapd)

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle

Gazeti la "die  tageszeitung" limearifu  juu ya kukamatwa, nchini Kongo kwa Katibu Mkuu wa chama cha upinzani,cha Umoja wa Kidemokrasi na maendeleo ya kijamii,UDPS Bwana  Jacquemain Shabani.

Gazeti hilo limeripoti kuwa Katibu Mkuu huyo wa chama kikuu cha upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo alikamatwa kwenye uwanja wa ndege wa mjini Kinshasa na hivyo kuzuiwa kupanda ndege na kuelekea Ujerumani.Gazeti la"die  tageszeitung"limearifu kwamba,baada ya kukamatwa, Katibu Mkuu Shabani alipelekwa sehemu isiyojulikana. Hata hivyo mwanasiasa huyo sasa ameshaachiwa lakini amenyang'anywa pasipoti yake.

Alialikwa kufanya ziara Ujerumani na Wakfu wa Friedrich-Ebert ili kukutana na viongozi wa kisiasa, pia wa chama kikuu cha upinzani nchini Ujerumani  SPD.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limechapisha taarifa juu ya mwelekeo  mpya katika uhusiano baina ya   Ujerumani na nchi zinazoinukia kiuchumi. Gazeti hilo limeripoti kwamba Ujerumani inakusudia kuimarisha uhusiano wake na nchi zinazoinukia kiuchumi. Kutokana na pendekezo la Waziri wa mambo ya nje Westerwelle,Baraza la mawaziri  la Ujerumani limeipitisha dhana mpya ya uhusiano na mataifa makubwa mapya.

Gazeti  la "die  tageszeitung" limemkariri Waziri Westerwelle akisema kuwa dunia imebadilika na kwamba Ujerumani inapaswa kuenda sambamba na mabadiliko hayo. Kulingana na dhana hiyo mpya Ujerumani itaimarisha uhusiano siyo tu na China, India ,Brazil,Urusi na Afrika Kusini, bali pia na nchi kama Vietnam,Columbia na Nigeria.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" wiki hii limechapisha makala iliyoandikwa na Lothar Rühl juu ya sera za usalama na ulinzi kwa lengo la kudhibiti migogoro.Katika makala hiyo Bwana Rühl anatoa mwito kwa nchi za Ulaya wa kuwa  macho juu ya Afrika.

Amesema tukio muhimu sana mwaka jana, yalikuwa mapinduzi katika nchi za Kiarabu ikiwa pamoja na Kaskazini mwa Afrika.Tukio hilo ulikuwa mtihani mgumu kwa nchi za Ulaya na jinsi ya kukabiliana na migogoro. Katika makala yake Lothar Rühl anaeleza kuwa matukio ya nchini Libya na Tunisia yalizishtukiza nchi za Ulaya.

Na sasa ingawa Ulaya inaweza kusaidia katika kuyafanikisha mapinduzi, inapaswa kutilia maanani kwamba,wanaitikadi kali wa kiislamu wanazidi kuimarika Kaskazini mwa Afrika.

Gazeti la mrengo wa shoto "Neues Deutschland" wiki hii linauzungumzia mvutano wa kisiasa nchini Senegal uliosababishwa na uamuzi wa Baraza la Katiba la nchi hiyo kumruhusu Rais Abdoulaye Wade kugombea kipindi kingine cha Urais.

Gazeti la "Neues Deutschland" limeripoti kwamba maandamano ya kuupinga uamuzi huo yanaendelea nchini Senegal.  Gazeti hilo limearifu kuwa wiki iliyopita   zilitokea ghasia mara kwa mara.

Katika mapambano baina ya wafuasi wa chama cha upinzani na polisi, watu  watano waliuawa katika mji mkuu Dakar na katika mji wa Kaskazini Podor. Waliouawa walikuwa pamoja na mwanafunzi mmoja.

Rais Abdoulaye Wade mwenye umri wa miaka 85 anawania kipindi cha tatu cha Urais na atasimama katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 26  mwezi huu.

Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" wiki hii linakumbusha juu ya safari ya "Zarafa." Huyo ni Twiga ambae miaka 200 iliyopita alifika Paris baada ya safari ya kilometa 7000 kutoka Sudan. Wakati angali mtoto alibebwa mgongoni na ngamia kutoka Sudan hadi Misri.Na kutoka hapo alipakiwa katika meli. 

Mnamo mwaka wa 1826,meli iliwasili katika mji wa Marseille ikiwa na Twiga  aliekuwa wa kwanza kuokekana nchini Ufaransa. Watawala wa kituruki walimpelekea Mfalme wa Ufaransa Karl wa 10 mnyama huyo kama zawadi ili  kumtuliza, baada ya watawala hao kuwashambulia wapigania uhuru wa  Kigiriki.Waturuki walimhonga mfalme huyo ili asiingie katika vita dhidi yao.

Kutoka mji wa Marseille, Zarafa alitembea umbali wa maili 550 hadi  Paris kwa Mfalme aliemweka myama huyo katika bustani yake ambapo kila mtu aliweza kumwona.  Jumatano iliyopita mkasa huo uliadhimishwa kwa filamu katika  senema za Paris.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/ Othman Miraji/