1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ujerumani yaahidi uungaji mkono zaidi kwa Ukraine

21 Novemba 2023

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amewasili mjini Kyiv Jumanne (21.11.2023) kwa ziara ambayo haikutangazwa kusisitiza uungaji mkono wa nchi yake kwa Ukraine katika mapambano yake dhidi ya wanajeshi wa Urusi

https://p.dw.com/p/4ZFUv
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius akizungumza na waandishi wa  habari katika mkutano wa siku mbili wa jeshi la nchi hiyo mnamo Novemba 10, 2023
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani - Boris PistoriusPicha: Christophe Gateau/dpa/picture alliance

Hii ilikuwa ziara ya pili ya Pistorius mjini Kyiv tangu achaguliwe kuwa waziri wa ulinzi wa Ujerumani mwanzoni mwa mwaka huu, na inakuja siku moja baada ya waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin pia kufanya ziara ambayo haikutangazwa nchini Ukraine kusisitiza kuhusu uungaji mkono wa Marekani.

Soma pia:Marekani kuendelea kuiunga mkono Ukraine dhidi ya Urusi

Wakati alipokuwa akiweka shada la maua kwenye uwanja wa Maidan kuadhimisha muongo mmoja wa maandamano ya kihistoria ya kuunga mkono demokrasia huko Kyiv ambapo takriban raia 100 waliuawa, Pistorious alisema kuwa yuko nchini humo kwa mara nyingine tena, kwanza kuahidi msaada zaidi lakini pia kuelezea mshikamano wa nchi yake na ushirikiano mkubwa na pia kuvutiwa kwa Ujerumani na mapigano ya ujasiri na kishujaa nchini humo.

Soma pia:Marekani yaitoa wasiwasi Ukraine kuhusu msaada wa kijeshi

Pistorius aliyewasili nchini humo kwa kutumia treni, baadaye atafanya mazungumzo na mwenzake wa Kyiv pamoja na rais Volodymyr Zelensky.

Ujerumani ambayo ni mfadhili wa pili mkubwa wa msaada wa kijeshi kwa Ukraine baada ya Marekani, inataka kutoa hakikisho baada ya kuibuka kwa wasiwasi wa kupungua kwa msaada kwa Ukraine kutokana na vita katika Mashariki ya Kati.

Zelensky ahusisha maandamano ya Maidan na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine

Rais Zelensky,  ameyahusisha  maandamano hayo ya kihistoria ya kuunga mkono demokrasia huko Kyiv muongo mmoja uliopita na uvamizi wa Ukraine, akitaja maandamano hayo kwenye uwanja wa Maidan kama "ushindi wa kwanza" katika vita na Urusi.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin akihutubia wakati wa hafla ya kapteini mstaafu Larry L.Taylor katika ukumbi wa Conmy mnamo Septemba 6, 2023
Waziri wa ulinzi wa Marekani - Lloyd AustinPicha: Celal Gunes/AA/picture alliance

Maandamano hayo ya vuguvugu la waandamanaji wanaounga mkono Ulaya ambapo takriban raia 100 walikufa katika mapigano makali na vikosi vya usalama katika mji mkuu hatimaye yalisababisha kuondolewa madarakani kwa Rais Viktor Yanukovych aliyekuwa anaungwa mkono na Urusi.

Mashambulizi ya vikosi vya Urusi yasababisha uharibifu nchini Ukraine

Katika hatua nyingine,  jeshi la Ukraine limesema kuwa vikosi vya Urusi vimerusha makombora manne, moja la masafa marefu na ndege 11 zisizo na rubani na  kuharibu hospitali ya jiji kuu katika mji wa Selydove mkoani Donetsk, jengo la mgodi wa Kotlyarevska na miundombinu mingine ya kiraia.

Hata hivyo haikubainisha iwapo hospitali hiyo ilikuwa inatumika au kama kulikuwa na majeruhi wowote.

Soma pia:Urusi imefanya mashambulizi dhidi ya Ukraine baada ya wiki kadhaa ya kusimamisha mapigano

Takriban watu wanne waliuawa katika mji huo wiki iliyopita baada ya vikosi vya Urusi kushambulia kwa makombora jengo la makazi katika eneo hilo. Jeshi hilo pia limesema kuwa limelenga na kuangusha ndege 10 zisizo na rubani na kombora hilo la masafa marefu.

Ukraine imekuwa ikikabiliana na ongezeko la mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundombinu muhimu hasa vituo vya nishati huku msimu wa baridi ukizidi kushika kasi.