Waziri wa ulinzi wa Marekani Gates leo ameanza ziara nchini Pakistan. | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.01.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waziri wa ulinzi wa Marekani Gates leo ameanza ziara nchini Pakistan.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates yupo nchini Pakistan kwa ziara ya siku mbili.

default

Waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates yupo Pakistan kwa ziara ya siku mbili.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates amesema sehemu ambapo Taliban wanajificha kwenye mpaka baina ya Afghanistan na Pakistan lazima zishughulikiwe la sivyo nchi hizo zitakabiliwa na mashambulio mabaya zaidi.

Waziri Gates amesema hayo mjini Islamabad leo ambapo anaendelea na ziara ya siku mbili nchini Pakistan.

Waziri huyo amesema atajadili na viongozi wa Pakistan juu ya uwezekano wa kuimarisha operesheni za kijeshi dhidi ya wanaitikadi kali wa kiislamu kaskazini magharibi mwa Pakistan.

Lakini jeshi la nchi hiyo limesema kuwa halina mpango wa kuanzisha operesheni mpya dhidi ya wapinzani mnamo mwaka huu.

Msemaji wa jeshi la Pakistan amewaambia waandishi habari kwamba jeshi la Pakistan ambalo limelemewa halina mipango ya kuanzisha mapambano dhidi wapinzani katika kipindi cha miezi 12 ijayo.

Hatahivyo waziri wa ulinzi wa Marekani R. Gates amelipongeza jeshi la Pakistan kwa mashambulio liliyoyafanya dhidi ya wapiganaji wa Taliban na kusababisha al -Qaeda na magaidi wengine wazikimbie sehemu zao za maficho.

Bwana Gates ametahadharisha juu ya mashambulio yanayofanywa na makundi mbambali chini ya uongozi wa al-Qaeda yenye lengo la kuziyumbisha siyo tu Pakistan , au Afghanistan bali eneo lote la kusini mwa Asia.

Hii ni mara ya kwanza kwa waziri Gates kufanya ziara nchini Pakistan tokea ateuliwe kushika wadhifa huo chini ya utawala wa rais Obama unaoizingatia Pakistan kuwa sehemu muhimu sana katika harakati za kupambana na wanaitikadi kali wa kiislamu katika eneo la kusini mwa Asia.

Maafisa wa Marekani wameeleza wazi kwamba wanaitaka Pakistan iwafuatilie Taliban waliomo nchini humo pamoja na makundi yenye uhusiano na mtandao wa al-Qaeda.

Madhumuni ya ziara ya waziri Gates nchini Pakistan ni kuwashawishi viongozi wa nchi hiyo kutandaza operesheni dhidi ya wapinzani hadi katika jimbo la Waziristan ya Kaskazini.

Hatahivyo msemaji wa jeshi ya Pakistan meja Athar Abbas ameeleza kuwa itachukua muda wa nusu mwaka hadi mwaka mzima ili kuweza kuleta utulivu katika jimbo Waziristan ya kusini ambako majeshi ya Pakstan yanaelekeza operesheni zao kwa sasa.

Meja Abbas amesema wakati askari 30,000 sasa wapo katika jimbo la Waziristan ya Kusini, usalama wa eneo hilo unahitaji kuimarishwa kabla ya kuanzisha operesheni mpya.

Mwandishi/Mtullya Abdu /AFPE.

Mhariri/Othman Miraji

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com