Waziri Mkuu wa Ugiriki ashutumu vitisho vya wakopeshaji | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.06.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waziri Mkuu wa Ugiriki ashutumu vitisho vya wakopeshaji

Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras amewashutumu wakopeshaji wake kwa vitisho na kusema kwamba Umoja wa Ulaya haukuundwa chini ya misingi ya vitisho wakati nchi hiyo ikiwa katika mazungumzo ya kunusuru isifilisike.

Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras.

Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras.

Waziri Mkuu huyo wa Ugiriki akizungumza mjini Brussels Ijumaa (26.06.2015) baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya amesema kuweka muda wa mwisho na vitisho ni mambo yasiokuwa na nafasi Umoja wa Ulaya wakati nchi yake ikiwa katika juhudi za kufikia makubaliano na wakopeshaji wake wanaodai nchi hiyo ifanye mageuzi magumu ya kubana matumizi ili iweze kupatiwa msaada wa kuinusuru isifilisike na madeni.

Tsipras amekaririwa akisema "Misingi iliojenga Umoja wa Ulaya ni demokrasia, mshikamano, usawa na kuheshimiana.Misingi hii haikujengwa na vitisho na kuweka muda wa mwisho.Na hususan katika wakati huu mgumu hakuna mwenye haki ya kuhatarisha misingi hiyo.Serikali ya Ugiriki itaendelea kwa nguvu kupigania misingi hii kwa niaba ya wananchi wa Ulaya na bila ya shaka kwa niaba ya wananchi wa Ugiriki."

Serikali ya Ugiriki na wakopeshaji wake wako kwenye mkwamo katika kufikia makubaliano yatakayowezesha nchi hiyo kupatiwa fedha ili kuizuwiya isifilisike zikiwa zimebakia siku chache kabla ya kulipa deni lake kwa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF hapo Juni 30.

Merkel na pendekezo jipya

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameihimiza Ugiriki kukubali pendekezo aliloliita kuwa la ukarimu kutoka kwa wakopeshaji wake wa Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF ambalo linajumuisha euro zisizopunguwa bilioni 12 katika mkopo zaidi wa uokozi utakaotolewa katika kipindi cha miezi mitano ijayo.

Merkel na Rais Francois Hollande wa Ufaransa wamemtaka Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras kukubali pendekezo hilo la ukarimu kutoka taasisi hizo baada ya kukutana naye kwa faragha kwa dakika 45 pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels.Inaelezwa kwamba waliangalia kwa kina pendekezo hilo ambapo fedha zake zitatolewa kwa haraka iwapo Ugiriki itakubali kusaini makubaliano.

Wakopeshaji wa Ugiriki wamependekeza nyongeza ya euro bilioni 12 itakayotolewa kwa miezi mitano kwa Ugiriki iwapo nchi hiyo itakubali kufanya mageuzi katika makubaliano muhimu kuhusu mzozo wa madeni wa nchi hiyo.

Ushawishi wa Merkel na Hollande

Mkutano wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras mjini Brussels. (26.06.2015)

Mkutano wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras mjini Brussels. (26.06.2015)

Kansela huyo wa Ujerumani ambaye mawazo yake na ya Hollande yana uzito mkubwa kutokana na kwamba nchi zao kuwa wakopeshaji wakuu wa Ugiriki amesema pendekezo hilo linapindukia masharti ya mpango wa pili wa uokozi.

Merkel amekaririwa akisema pendekezo hilo liko kama ilivyo siku zote kwenye kanuni ile ile ya mshikamano kwa upande mmoja na juhudi za wahusika kwa upande wa pili.

Waziri wa Kazi wa Ugiriki Panos Skourletis ameonya kwamba Ugiriki huenda ikalazimika kuitisha uchaguzi wa haraka iwapo wakopeshaji wataendelea kushikilia madai yao ambayo amesema ni sawa na kuitaka Ugiriki ijiuwe.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/dpa

Mhariri : Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com