1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu akataa nadai ya upinzani Thailand

2 Desemba 2013

Waziri Mkuu wa Thailand amesema yuko tayari kufanya kila liwezekanalo kumaliza maandamano ya ghasia dhidi ya serikali yake na kurudisha amani nchini akini hawezi kukubali madai ya upinzani yanayokwenda kinyume na katiba.

https://p.dw.com/p/1ARvM
Waziri Mkuu wa Thailand Yingluck Shinawatra akizungumza na taifa kupitia televisheni 28.11.2013.
Waziri Mkuu wa Thailand Yingluck Shinawatra akizungumza na taifa kupitia televisheni 28.11.2013.Picha: picture-alliance/dpa

Waziri Mkuu wa Thailand leo hii amesema yuko tayari kufanya kila liwezekanalo kumaliza maandamano ya ghasia dhidi ya serikali yake na kurudisha amani nchini humo lakini hawezi kukubali madai ya upinzani yanayokwenda kinyume na katiba kukabidhi madaraka kwa baraza lisilochaguliwa na wananchi.Ghasia za kisiasa zinapamba moto katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangkok huku kukiwa hakuna ishara ya kumalizika kwa ghasia hizo.

Kauli hiyo ya Waziri Mkuu Yingluck Shinawatra iliitowa kupitia televisheni Jumatatu (02.12.2013) wakati wa mkutano na waandishi wa habari kutoka katika makao makuu ya polisi ya taifa ambayo yalikuwa chini ya ulinzi mkali.Amesema madai ya upinzani kukabidhi madaraka kwa baraza lisilochaguliwa na wananchi ni kukiuka katiba.

Kauli yake yaashiria suluhu

Katika kauli thabiti lakini yenye kuashiria kutaka suluhu amesema serikali iko tayari kuwa na mazungumzo lakini yeye mwenyewe binafsi haoni njia ya kuondokana na tatizo hilo. Ameongeza kusema kwamba hapingi kujiuzulu wala kuvunjwa kwa bunge iwapo ufumbuzi huo utakomesha maandamano hayo na kwamba serikali haijaribu kun'gan'gania madaraka.

Purukushani katika maandamano dhidi ya serikali mjini Bangkok 02.12.2013.
Purukushani katika maandamano dhidi ya serikali mjini Bangkok 02.12.2013.Picha: picture-alliance/dpa

Waandamanaji ambao wengi wao ni watu wa tabaka la kati mjini Bangkok ambao ni wafuasi wa chama cha upinzani cha Demokratik wanamshutumu Yingluck kuwa kibaraka wa kaka yake waziri mkuu wa zamani Thaksin Shinawatra ambaye anaishi uhamishoni baada ya kupinduliwa katika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2006.

Wakati waziri mkuu huyo akizungumza mapambano ya mitaani kati ya polisi na waandamanaji yalioanza mwishoni mwa juma yalikuwa yakipamba moto. Waandamanaji walikuwa wakiwarushia polisi miripuko iliotengenezwa kienyeji wametumia magari ya taka na matinga tinga kujaribu kuvunja vizingiti vya zege vilivyowekwa kwenye makao makuu ya serikali na taasisi nyengine na polisi ilijibu kwa kutumia gesi ya kutowa machozi,maji ya kuwasha na hata risasi za mpira.Takriban watu watatu wameuwawa na zaidi ya 200 kujeruhiwa katika maandamano hayo ya siku tatu mfululizo.

Madai ya kiongozi wa upinzani

Kiongozi wa upinzani Suthep Thaugsuban ambaye alikutana na waziri mkuu hapo Jumapili amesema hatoridhika na kujiuzulu kwa Yingluck na kuitishwa kwa uchaguzi mpya bali anataka baraza la wananchi lilisilochaguliwa kumteuwa waziri mkuu mpya na kuongeza ,"Iwapo Waziri Mkuu Yingluck Shinawatra atasikiliza sauti ya wananchi na kukabidhi madaraka kwa wananchi kwa heshima tutamhurumia kwani sisi sote ni raia wema."

Kiongozi wa maandamano ya upinzani nchini Thailand Suthep Thaugsuban.
Kiongozi wa maandamano ya upinzani nchini Thailand Suthep Thaugsuban.Picha: Reuters

Watu wengi wameyashutumu madai hayo ya kiongozi wa upinzani kuwa sio ya demokrasia.Mkutano wa Suthep na waziri mkuu hapo jana umefanyika mbele ya viongozi waandamizi wa kijeshi licha ya kwamba kulikuwa na hati ya kumkamata.Hati ya pili ya kumkamata imetolewa leo hii kwa madai ya uasi ambapo naibu kamanda wa polisi Meja Generali Chayut Thanataweerat amesema hukumu yake ni adhabu ya kifo au kifungo cha maisha gerezani.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AP/AFP

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed