Watu zaidi kuyahama makaazi yao
1 Juni 2012Shirika la kuwahudumia wakimbizi UNHCR limesema kuwa sababu hizo ni pamoja na ukimbizi wa kiuchumi, mabadiliko ya tabia nchi , ukosefu wa chakula , na mapigano.
Mkuu wa Shirika hilo la kuwahudumia wakimbizi duniani UNHCR Antonio Guterres ametoa sababu nyingine kuwa uhaba wa maji, mashindano ya kutafuta rasili mali na pia ongezeko la watu duniani. Antonio aliyasema hayo alipokuwa akizundua ripoti hiyo katika makao makuu ya Umoja wa mataifa mjini New York .
Kwa sasa kuna takriban watu milioni 26 waliokosa makaazi ndani ya nchi zao huku idadi ya watu milioni 15-16 wakiwa ni wakimbizi na wengine Millioni moja wakiomba hifadhi ya kisiasa katika mataifa ya nje. Hata hivyo shirika hilo halikutoa idadi ya watu wanaokadiriwa kuongezeka kwa miaka kumi ijayo.
Hatua za pamoja
Antonio Guterres amesema hili ni suala la kimataifa na linapaswa kutafutiwa suluhisho la kimataifa huku akisisitiza kuwepo pia kwa suluhisho la kisiasa.
"Wakimbizi wengi hungoja suluhu ya kisiasa ipatikane nchini mwao ili waweze kurudi nyumbani na kuishi maisha ya kawaida" lilisema shirika hilo la kuwashughulikia wakimbizi duniani UNHCR.
Wakimbizi hukabiliwa na hali ngumu ya maisha
Ripoti hii ya kila mwaka imetoa sura ya hali halisi ya wakimbizi wa nje ya nchi na wale waliokosa makaazi ndani ya nchi zao. Wakimbizi hujikuta katika hali ngumu ya maisha iliojaa changamoto nyingi hasaa katika suala la kupata suluhisho huku wafanyakazi wa kutoa misaada wanaowasaidia wakikabiliana na vitisho kutoka maeneo yaliyoathirika.
Hata hivyo Mkuu wa UNHCR Antonio Guterres amesema kwa sasa ni nchi nyingi tu zilizofungua mipaka yake kuwapokea wakimbizi ambao nchi zao zinakumbwa na ghasia na machafuko ikiwemo wale waliokimbia nchi zao kutokana na maandamano ya kutaka mabadiliko nchini mwao katika maeneo ya kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya kati.
Mwandishi :Amina Abubakar/DPA
Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman