1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wote 157 wafariki katika ajali ya ndege ya Ethiopia

10 Machi 2019

Ndege ya Ethiopia nambari ET-302 ilikuwa imebeba raia wa mataifa 33 kuelekea Nairobi nchini Kenya kabla ya kuanguka karibu na mji wa Bishoftu nchini Ethiopia

https://p.dw.com/p/3Ek2X
Boeing 787 Ethiopian Airlines
Picha: Reuters

Hakuna mtu hata mmoja aliyenusurika  kati ya watu 157 waliokuwa kwenye ndege ya shirika la ndege la Ethiopia iliyoanguka jumapili asubuhi (10.03.2019) ikitokea mji mkuu wa Ethiopia Adis Ababa kuelekea Nairobi Kenya,kwa mujibu wa shirika la habari la Ethiopia. Raia kutoka mataifa 33 walikuwemo kwenye ndege hiyo yenye nambari ya usajili ET 302 iliyoanguka karibu na mji wa Bishoftu ulioko kiasi kilomita 50 Kusini Mashariki mwa mji mkuu Adis Ababa kwa mujibu wa ripoti.

Msemaji wa shirika la ndege ya Ethiopia ameliambia shirika la habari la kijerumani Dpa, raia 32 wakenya, Waethiopia 17, na wachina 8 ni miongoni mwa abiria waliokufa waliokuwa wakisafiri na ndege hiyo. Hakuna taarifa za haraka zilizotolewa kuthibitisha uraia wa abiria wengine waliokuwemo kwenye ndege hiyo.

Äthiopien Addis Abeba Ethiopian Airlines Flugzeug
Picha: Reuters/A. Dalsh

Ndege aina ya Boeing 737 iliyokuwa na abiria 149 na wafanyakazi 8 iliruka mwendo wa saa 8.38 za asubuhi kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa  Bole na kupoteza mawasiliano dakika chache baadae kwa mujibu wa shirika hilo la ndege la Ethiopia.

Ofisi ya waziri mkuu wa Ethiopia kwa niaba ya serikali imetowa ujumbe wa salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo. Shughuli ya utafutaji miili na uokoaji zinaendelea ingawa imeelezwa hakuna mtu aliyenusurika huku pia ikitajwa kwamba chanzo kilichosababisha ajali hiyo hakijafahamika.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Sylvia Mwehozi

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW