1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wahimizwa kula mboga na matunda kuliko nyama nyekundu

Amina Mjahid
17 Januari 2019

Watafiti wanasema binaadamu wanatakiwa kula zaidi maharage na dengu na kupunguza ulaji wa nyama nyekundu ili kuilinda dunia na afya zao kwa ujumla.

https://p.dw.com/p/3Biok
Obst und Gemüse
Picha: Colourbox

Katika utafiti uliochapishwa kwenye jarida la sayansi la Lancet, mabadiliko makubwa yanahitajika katika uzalishaji na ulaji wa chakula ili kuepusha vifo vya mamilioni ya watu na kuilinda sayari kutokana na uharibifu.

Kitu muhimu hapa ni kuwa na mabadiliko ya lishe ya dunia na hii inamaanisha kutumia sukari kwa kiwango kidogo na kupunguza ulaji wa nyama nyekundu na badala yake kula kwa wingi mbogamboga, kunde, matunda na njugu, umebainisha utafiti huo.

Proteinquellen
Picha: Colourbox

Watafiti kutoka kamisheni ya EAT-Lancet wamesema iwapo watu watafuata mpango huo wa lishe,  zaidi ya vifo milioni 11 kila mwaka vinavyotokea kabla ya wakati vinaweza kuepukika, Hewa chafu ya kaboni huenda ikapungua huku ardhi zaidi, maji na uwepo wa viumbe hai vikahifadhiwa.

Nyama kiasi gani ni afya?

Mpango huo wa lishe bora kwa dunia unaashiria kila mwanadamu ale gramu 14 tu ya nyama nyenkundu kwa siku, gramu 29 ya vyakula vitokanavyo na kuku, na gramu 13 ya mayai au yai moja na nusu kwa wiki.

mpango huu unatokana na utafiti uliofanywa kwa takriban miaka mitatu ulioanzishwa na kamisheni hiyo ya Lancet kwa kuwahusisha wataalamu 37 kutoka mataifa 16.

"Tuko katika hali ya janga," alisema muandishi mwenza Tim Lang, ambaye ni Profesa katika chuo kikuu cha Uingereza na kiongozi wa sera wa kamisheni ya EAT-Lancet iliofanya utafiti huo.

Lang amesema kulisha idadi inayoongezeka ya watu bilioni 10 ifikapo mwaka 2050, kwa lishe endelevu na ya kiafya haitawezekana bila kubadilisha namna tunavyokula, kuimarisha uzalishaji wa chakula na kupunguza uharibifu wa chakula chenyewe.

Stockbild Tiefkühlgemüse
Picha: Colurbox

Lang ameongeza kuwa chakula tunachokula na namna tunvayokizalisha inategemea pakubwa afya ya watu pamoja na sayari na kwa sasa mambo yanakwenda kombo.

Magonjwa hatari kama vile unene wa kupita kiasi, kisukari, na aina tofauti ya saratani yanahusishwa na lishe mbaya  ya chakula.

Watafiti wanasema lishe kama hizo zinachangia vifo zaidi na magonjwa kuliko hata magonjwa yanayotokana na kufanya ngono bila ya kutumia kinga, unywaji wa pombe, dawa za kulevya na hata uvutaji wa sigara vikichanganywa pamoja.

Watafiti wanashauri watu kukumbatia zaidi lishe bora kwa manufaa ya afya zao

Lakini mabadiliko hayo ya lishe yatahisiwa zaidi katika baadhi ya maeneo kuliko mengine.  Kwa mfano watu kutoka Amerika ya Kaskazini wanakula mara sita na nusu zaidi kiwango kinachopendekezwa cha nyama nyekundu, huku watu kutoka Kusini mwa Asia wakila nusu ya kiwango kilichopendekezwa.

Ein Paar mit einer Schüssel Salat
Picha: Colourbox

Na wakati huo, utafiti huo unaonyesha kuwa kufikia viwango vinavyopendekezwa vya vyakula vya wanga kama vile viazi na mhogo kutahitaji mabadiliko makubwa katika kanda ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako kwa wastani watu hula mara saba na nusu ya kiwango kinchopendekezwa.

Walter Willet kutoka chuo kikuu cha Harvard anasema zaidi ya watu milioni 800 hawana chakula cha kutosha huku watu wengi zaidi wakila chakula kisicho na lishe bora kinachosababisha vifo vya mapema na magonjwa hatarishi.

Walter amesema kama watu hawawezi kufanikisha mpango wa lishe bora duniani basi ni vizuri wajaribu kuukaribia.

Mwandishi: Amina Abubakar/DW page

Mhariri:Iddi Ssessanga