1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

moja juu ya tano ya watakuwa wazito zaidi ifikapo mwaka 2025

John Juma1 Aprili 2016

Marekani na Uchina ndio zinaongoza miongoni mwa nchi zenye watu walio na uzito kupindukia, Uingereza ikiongoza mataifa ya Ulaya. Japan ndilo taifa tajiri ambalo lina watu wachache walio na uzito wa kupindukia.

https://p.dw.com/p/1IO6J
Watu wenye uzito uliozidi.
Watu wenye uzito uliozidi.Picha: Imago

Zaidi ya watu milioni 640 wameongeza unene uliopindukia mwilini yaani 'obesity'. Hii inamaanisha kuwa dunia inao watu wanene kupindukia kuliko watu walio na uzito wa kawaida. Hii ni kulingana na utafiti ulioonyesha kuwa mmoja kati ya wanaume 10 anao unene uliokithiri na mmoja kati ya wanawake 7 vilevile.

Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, idadi ya watu wanene wenye uzito wa kupindukia imeongezeka sana. Watu walio na viwango vya vipimo 30 na zaidi vya kisayansi vinavyolinganisha urefu na uzito wa binadamu yaani kwa kimombo Body Mass Index (BMI), wameongezeka kutoka watu milioni mia moja na tano mnamo mwaka 1975 hadi watu milioni 641 mnamo mwaka 2014.

Matembezi kama mazoezi.
Matembezi kama mazoezi.Picha: AP

Uzito uliopindukia ni hatari kiafya

Utafiti huo uliofanywa na watafiti 700 na kujumuisha shirika la Afya Duniani, ulihusisha watu wazima milioni ishirini kutoka jumla ya mataifa 186. Hata hivyo wengi wa wanaokumbwa na hali hii wanatoka katika mataifa yaliyo tajiri, kwani watu wengi katika mataifa masikini wana uzito wa chini. Ripoti ya utafiti huo imeongeza kuwa moja juu ya tano ya watu wazima watakuwa na uzito wa kupindukia ifikapo mwaka 2025.

Profesa Majid Ezzati kutoka chuo cha afya ya umma mjini London amesema uzito wa kupindukia unakumba idadi kubwa ya watu ulimwenguni kote ni tishio kwa afya zao. Ameongeza kuwa suala hilo haliwezi kusuluhishwa tu kimatibabu, au kupunguza bei za dawa za kudhibiti uzito wa kupindukia wala kuongeza barabara za matembezi na watu kuendesha baisikeli ili kupunguza uzito, bali sharti kuwe na mikakati kabambe duniani ikiwemo kupunguza bei za vyakula vinavyokuza lishe bora na kuongeza bei za vyakula vinavyozidisha uzito mwilini mfano sukari na vyakula vinavyoundwa viwandani.

Mtoto aliyezidisha uzito.
Mtoto aliyezidisha uzito.Picha: picture alliance/dpa

Nchi zilizoathiriwa sana

Marekani ndio inaongoza miongoni mwa mataifa yenye watu walio na uzito wa kupindukia ikifuatwa na Uchina huku Uingereza ikiongoza miongoni mwa mataifa ya Umoja wa Ulaya. Miongoni mwa mataifa yenye uchumi mkubwa Japan ndilo taifa ambalo lina watu wachache walio na uzito wa kupindukia.

Uzito ulio sawa hubainishwa kisayansi kwa kupima uzito wa mtu kwa kilo kisha kuugawa na urefu wake kwanzia mguu hadi kichwani. Uzito huo wa BMI unaozidi 25 huwa umepita kiwango na zaidi ya 30 ni wa kupindukia, huku unapofika 40 na zaidi huitwa uzito wa ugonjwa ka kimombo 'morbidly obese'. Walioko katika hali hii hupata taabu kupumua na kutembea na hukumba asilimia moja ya wanaume na asilimia 2 ya wanawake.

Hata hivyo uzito uliopungua pia umetajwa kuwa changamoto katika baadhi ya mataifa, mfano robo ya watu katika bara Asia wamepungukiwa uzito. Katika Afrika ya Kati na Mashariki asilimia 12 ya wanawake na 15 ya wanaume wanao uzito uliopungua viwango vinavyohitajika.

Mwandishi: John Juma/ RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef