1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaJamhuri ya Afrika ya Kati

Watu 58 wapoteza maisha ajali ya boti Afrika ya Kati

Bruce Amani
21 Aprili 2024

Takribani watu 58 wamekufa katika ajali ya boti nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

https://p.dw.com/p/4f1Gj
Juhudi za uokoaji kwenye mkasa wa kuzama kwa boti nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Juhudi za uokoaji kwenye mkasa wa kuzama kwa boti nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Picha: JeffersonCF/Xinhua/picture alliance

Boti iliyokuwa imejaa watu kupindukia ilivunjika katika vipande muda mfupi baada ya kung'oa nanga kwenye Mto Mpoko karibu na mji mkuu Bangui. Maafisa wameviambia vyombo vya habari nchini humo kuwa wanawake wengi na watoto ni miongoni mwa waliofariki katika mkasa huo wa Ijumaa.

Karibu abiria 300 walikuwa wakielekea kwenye mazishi. Watu kadhaa bado hawajulikani waliko. Kwa mujibu wa ripoti za Idara ya kuyashughulikia majanga, wafanyakazi wa uokozi waliwasili katika eneo la ajali dakika 40 baada ya boti hiyo kuzama.

Serikali haikuzungumzia tukio hilo jana lakini katika hotuba iliyorekodiwa Ijumaa na kurushwa hewani siku moja baadae, msemaji wa serikali Maxime Balalou aliripoti kuwa idadi ya awali ya vifo ilikuwa watu 30.

Serikali imetangaza kuanzisha uchunguzi na kuweka utaratibu wa kuzisaidia familia za waathirika. Usafiri wa majini hutumika zaidi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa sababu  barabara nyingi ziko katika hali mbovu. Lakini boti nyingi zimetengenezwa kwa mbao na hazitunzwi vizuri.