1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 49 wauawa kwenye shambulio la misikiti New Zealand

Sylvia Mwehozi
15 Machi 2019

Watu 49 wameuawa na wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa vibaya baada ya misikiti miwili kushambuliwa huko New Zealand wakati wa swala ya asubuhi leo Ijumaa. Waziri Mkuu wa nchi hiyo, amelitaja kuwa shambulio la kigaidi. 

https://p.dw.com/p/3F6t8
Neuseeland Schießerei in Moschee in Christchurch
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Baker

Vidio zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilizochukuliwa na mshambuliaji na kuziweka moja kwa moja mtandaoni wakati akifanya shambulizi, zilimuonyesha akiendesha gari hadi kwenye msikiti wa kwanza na kisha akaanza kuwamiminia risasi watu walokuwamo ndani. Shambulio hilo baya limetokea katika msikiti wa Al Noor katikati mwa Christchurch. Mshambuliaji alitumia dakika mbili ndani ya msikiti akimimina hovyo risasi na kisha baadae alitoka nje na kuwafyatulia risasi wapita njia. Shambulio la pili lilifanyika katika msikiti mwingine na kuwaua watu wengine 10.

Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern ameliita tukio hilo kuwa shambulio la kigaidi akisema watu wengi walioathirika ni wahamiaji na wakimbizi.

''Ni dhahiri kwamba tunaweza kulielezea tu kuwa shambulio la kigaidi. Kwa tunachokijua sasa, inaonekana kuwa shambulio hili lilipangwa vizuri. Vilipuzi viwili vimepatikana katika magari ya washukiwa na vimeharibiwa. Hadi sasa kuna watuhumiwa wanne waliokamatwa, lakini watatu wanahusishwa na shambulio hili, mmoja kati yao ametamka hadharani kuwa ni mzaliwa wa Australia. Hawa ni watu ninaoweza kuwaelezea kuwa na mitazamo mikali ambayo haikubaliki hapa New Zealand na hata duniani kote.''

Neuseeland Angriff auf Moscheen in Christchurch | Jacinda Ardern, Premierministerin
Waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern akizungumza kwa njia ya televisheniPicha: Reuters/TVNZ

Polisi wanawashikilia wanaume watatu na mwanamke mmoja baada ya shambulio hilo ambalo limeleta mshutuko katika taifa lenye watu karibu milioni 5 na mmoja wa watuhumiwa baadae amefunguliwa mashitaka ya mauaji. Mwanaume aliyedai kuhusikika na shamabulio hilo awali alichapisha ilani iliyo na kurasa 74 dhidi ya wahamiaji ambamo alielezea yeye ni nani na kwanini amefanya shambulio.

Katika ilani yake hiyo amejitambulisha kuwa kijana wa miaka 28 raia wa Australia na kuwa ni mbaguzi. Amesema ameichagua New Zealand kwa sababu ya eneo lake na kuonyesha kwamba hata maeneo ya mbali ya dunia hayakaribishi wakimbizi. New Zealand inachukuliwa kuwa nchi inayowakaribisha wahamiaji na wakimbizi. Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrison amethibitisha kuwa miongoni mwa washukiwa wanne waliokamatwa mmoja ni raia wa Australia.

Kamanda wa polisi Mike Bush amesema mtu huyo amefunguliwa mashitaka ya mauaji, akiongeza kwamba wamebaini vilipuzi katika mojawapo ya magari. Timu ya Kriketi ya Bangladesh imeepuka shambulio hilo baada ya basi walilokuwamo kuzuiliwa mita chache kabla ya kuufikia msikiti wa Al Noor ambako shambulio limefanyika. Wachezaji, makocha na maafisa wengine katika timu hiyo walikuwa wakielekea msikitini kwa ajili ya sala. Kufuatia hilo mchezo kati ya New Zealand na Bangladesh umeahirishwa. Viongozi kadhaa duniani wamelaani tukio hilo.

Reuters/AP