Wataliani kufanya uchaguzi Jumapili
23 Februari 2013Wataliani watapiga kura kesho Jumapili (24.02.2013) na Jumatatu (25.02.2013) wakati wakiendelea kukabiliana na kipindi kirefu cha mdororo wa uchumi katika muda wa miongo miwili pamoja na serikali kubana matumizi hali ambayo imesababisha malalamiko makubwa katika taifa hilo lenye uchumi wa tatu kwa ukubwa katika eneo la euro.
Matokeo ambayo yanatarajiwa ni serikali itakayoongozwa na vyama vya mrengo wa kati kushoto utakaoongozwa na kiongozi wa chama cha Democratic Pier Luigi Bersani, zamani akiwa mfuasi wa ukomunist ,mwenye tabia ya kujiamini na ambaye hivi sasa anakumbatia kwa kiasi kikubwa mawazo ya uchumi unaopendelea masoko.
"Nina imani kabisa kuwa nitashinda," Bersani amesema katika moja kati ya mahojiano yake kabla ya Jumamosi, ambapo wagombea hawaruhusiwi kufanya kampeni.
Masoko ya fedha yana shaka
Lakini matokeo bila shaka yanafahamika na iwapo Bersani ataunda muungano imara kwa kuwa na wingi katika mabaraza yote ya bunge ni jambo la kutia shaka sana, hali itakayoweka masoko ya fedha katika hali shaka shaka.
Waziri mkuu anayemaliza muda wake Mario Monti amekamilisha kampeni yake mjini Florence, akivishutumu vyama vya mrengo wa shoto kwa kuwa wafungwa wa nadharia yao isiyopindika na kumshutumu waziri mkuu wa zamani Silvio Berlusconi kwa kuwavunjia adabu wanawake.
Berlusconi atoa ahadi
Ahadi ya Berlusconi katika barua ambayo ilionekana kuwa rasmi ya kuwarudishia fedha zao Wataliani zilizokatwa kutokana na kodi ya umiliki wa mali iliyowekwa na Monti ilisababisha baadhi ya watu kuweka misururu mirefu katika ofisi za posta wakidai fedha zao.
Miji kadha barani Ulaya itakuwa inatega sikio kwa karibu iwapo Italia ikirejea katika miaka ya matumizi holela ya fedha za umma inaweza kuzusha maafa kwa mataifa ya eneo la euro.
"Tunaamini kuwa hali ya kitisho ipo kwamba baada ya uchaguzi wa Februari 24-25 huenda kukawa na upotevu wa msukumo kuhusu mageuzi muhimu ya kuongeza kasi ya matumaini ya ukuaji wa uchumi wa Italia," shirika la upangaji wa viwango vya uwezo wa kukopa la Standard & Poor's limesema katika ripoti yake wiki hii.
Kundi la utafiti lenye makao yake makuu mjini London la Capital Economics limeonya kuwa, "bunge ambalo litashindwa kupatikana wingi kwa upande mmoja linaweza kuirejesha Italia na eneo la euro katika mzozo".
Vituo vya uchaguzi
Vituo vya uchaguzi vitafunguliwa mapema asubuhi kesho Jumapili na kufungwa saa moja jioni saa za Ulaya ya kati. Siku ya pili ya uchaguzi Jumatatu uchaguzi utaanza saa 12 asubuhi na kumalizika saa tisa mchana, baada ya hapo matokeo ya awali yatatangazwa baadaye jioni ya Jumatatu.
Mario Monti , profesa muumini wa kanisa Katoliki ambaye anamaliza muda wake wa uongozi , ni chagua la wazi la kanisa hilo mjini Vatican katika uchaguzi huo. Lakini kujiegemeza kwake na muungano wa kati kushoto kunalifanya kanisa hilo kusita kidogo. Kura za Wakatoliki si za kupuuza katika siasa za Italia, ni mchekeshaji Beppe Grillo pekee ambaye amelipinga hadharani kanisa na amekataa mawazo yao.
Mwandishi. Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Grace Patricia Kabogo