Wataalamu: Iraq bado ina changamoto licha ya ushindi dhidi ya kundi la IS | NRS-Import | DW | 04.09.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

NRS-Import

Wataalamu: Iraq bado ina changamoto licha ya ushindi dhidi ya kundi la IS

Iraq bado ina changamoto nyingi licha ya ushindi wa majeshi yake dhidi ya kundi la wapiganaji wanaojiita Dola la Kiislamu, IS, ilioupata kwa ushirikiano mkubwa wa Marekani kwa upande mmoja na Iran kwa upande mwengine,

washirika wake ambao wenyewe hawatazamani usoni kwa jinsi uhasama wao unavyozidi kukuwa hasa wakati huu, ambapo Marekani inaongozwa na Donald Trump mwenye siasa kali kuelekea Iran.

Wataalamu wanasema kwamba bado jeshi la nchi hiyo lina kazi kubwa ya kuilinda Iraq dhidi ya makundi ya kigaidi, huku ikihitaji msaada wa mahasimu hao wawili, Iran na Marekani, kwa wakati mmoja.

Juhudi za taifa la Iraq dhidi ya wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, zinaonekana kupiga hatua kubwa, hasa baada ya ushindi wa hivi karibuni wa wanajeshi wake kutwaa maeneo ya katikati mwa wilaya ya mji wa Tal Afar.

Licha ya juhudi hizo zinazoonekana kusambaratisha nguvu ya wapiganaji wa IS, wataalamu wanasema bado jeshi la Iraqi linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kibarua kikubwa cha kuilinda nchi yao dhidi ya makundi haramu.

Mwaka wa 2014, wapiganaji wa IS walidhibiti eneo la kaskazini mwa Iraq, na kuwashinda nguvu polisi na wanajeshi.

Hii ikaongeza nguvu ya wapiganaji hao na kuwawezesha kuteka karibu thuluthi ya maeneo ya taifa hilo ikiwemo mji wa Mosul uliokombolewa tena na majeshi ya Iraq mwezi Julai.

Lakini kulingana na Waziri Mkuu Haider al-Abadi aliyeingia madarakani miezi mitatu baada ya mzozo wa kijeshi wa mwaka 2014, taifa hilo limerudisha hadhi yake ya zamani na lipo thabiti na imara.

Chini ya amri ya kiongozi huyo anayeungwa mkono na vikosi vya marekani, jeshi la Iraq limefanikiwa kuikomboa miji ya Tikrit, Ramadi, Fallujah na Mosul.

Alkhamis hii, Waziri Mkuu Abadi alitangaza kukombolewa kwa mji wa Tal Afar na maeneo ya karibu ya mji huo, hatua ambayo inauweka mkoa mzima wa Nineveh chini ya udhibiti wa serikali.

Irak Bodenoffensive auf die Stadt Tal Afar (Reuters)

Makabiliano makali kati ya jeshi la Iraq na wapiganaji wa IS

Tathmini ya siasa za Iraq 

Wataalamu wanasema ufanisi wa jeshi la Iraq umetokana na ushirikiano wao mzuri na mafunzo waliyopata kutoka kwa vikosi vya majeshi ya kigeni.

Wakati wa vita vya kupigania mji wa Mosul, ambavyo vimetajwa kuwa vita vikali sana kuwahi kutokea tangu Vita vya Pili vya Dunia, jeshi la Iraq lilipata pigo kubwa.

Lakini sasa wamefanikiwa kuwaondoa wapiganaji wa IS katika maeneo yote ya Iraq isipokuwa mji wa Hawija uliopo kilomita 300 kaskazini mwa mji mkuu wa Baghdad na ambao unakaribiana na mpaka wa Syria.

Na kulingana na mtaalamu wa maswala ya jeshi, Jessem Hanoun, ushindi huo wa wanajeshi unarudisha imani ya wananchi kwao na pia katika rubaa za kimataifa.

Mwezi uliopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Ibrahim al Jafari, alionya kuwa ushindi huo wa Iraq sio mwisho wa vita dhidi ya wapiganaji wa IS. Alisema Iraq itaendeleza ushirikiano wake wa kijeshi na miungano hiyo ya kigeni, kwani inahitaji usalama wa kutosha kujilinda dhidi ya makundi ya kigaidi yaliyopo, matamshi yanayowiana na mtaalamu wa maswala ya kijeshi, Jessem Hanoun, anayesema jeshi la Iraq linahitaji pakubwa usaidizi huo kukabiliana na wapiganaji wa IS ambao huenda wakajitokeza upya.

Je, ushirikiano huo utaendelea vipi Iraq? Swala hili ni gumu kwa pande zote mbili, yaani Iraq na Marekani, ambayo mwanzoni mwaka 2011 iliviondoa vikosi vyake ikiwa ni miaka 8 baada ya uvamizi wake mwaka wa 2003.

Ushirikiano wa Waziri Mkuu Abadi na Marekani unaibua changamoto kuhusu hatima ya kundi linalounga mkono jeshi la Iraq, liitwalo Hashed al Shaabi dhidi ya wapiganaji wa IS, ambao wanadhibitiwa na wanamgambo wa Kishia wanaoungwa mkono na Iran.

Viongozi wengi wa Kishia wametoa wito wa kundi hilo la Hashed lililoko chini ya uongozi wa Waziri Mkuu kubakia katika hali yake ya sasa.

Kulingana Profesa Mohammad Mahmoud wa Taasisi ya Historia ya Kimataifa ya Geneva, makundi yanayounga mkono jeshi la Iran yamechangia kuleta matatizo katika siasa za Iraq kuanzia miaka ya 1930.

Madai ya utesaji uliofanywa vikosi vya serikali na wapiganaji wa Hashed wakati wa makabiliano na kundi la IS yatatatiza juhudi za kurudisha imani ya Wasunni walio wachache na waliokuwa nje ya madaraka tangu kuangushwa  kwa Saddam Hussein mwaka wa 2003.

Mwandishi: Fathiya Omar/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com