1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi wa kuzuka mzozo wa kibinadamu waongezeka Tigray

17 Novemba 2020

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wa kuibuka mzozo kamili wa dharura ya kibinaadamu katika wakati ambapo maelfu ya raia wakikimbia mapigano katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia, na kwenye eneo la mpaka na Sudan

https://p.dw.com/p/3lQIG
Konflikt in Äthiopien - Flüchtlinge im Sudan
Picha: Marwan Ali/AP Photo/picture alliance

Umoja wa Mataifa unatoa tahadhari hiyo, wakati waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed akitishia awamu ya mwisho ya mashambulizi kwenye jimbo hilo.

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR, Babar Baloch ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba kuna wasiwasi wa kuibuka mzozo kamili wa kibinaadamu kufuatia machafuko hayo.Vikosi vya Ethiopia vyaukomboa mji mwingine mkoani Tigray

Baloch amesema kiasi cha watu 4,000 wanakimbia na kuvuka mpaka kila siku. Hadi sasa zaidi ya watu 27,000 wameingia Sudan tangu kuanza kwa machafuko wiki mbili zilizopita katika jimbo la Tigray.

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephanie Dujarric amezungumzia kitisho hicho mapema leo na kuurejea mwito wa suluhu ya amani.

Äthiopien I Situation in der Region Tigray
Wanajeshi wa vikosi vya AmharaPicha: Tiksa Negeri/REUTERS

"Wenzetu wa masuala ya kiutu wanarudia tena kutoa mwito kwa pande zote kwenye mzozo huo kusitisha mapigano ili kuzuia majanga zaidi na mateso kwa raia. Tuna wasiwasi pia kuhusu kuongezeka kwa wasiwasi wa kiusalama katika majimbo ya magharibi na kusini mwa Oromia. Hivyo, pande zote zinatakiwa kuwalinda raia na kufuata sheria za kimataifa za kibinaadamu", alisema Dujarric .

Huku miito kama hiyo ikiendelea, waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema kutakuwa na awamu ya mwisho ya mashambulizibaada ya wanamgambo na wanajeshi wa Tigray kukataa mwito wa kujisalimisha, huku kiongozi wa jimbo hilo Debretsion Gebremichael akiliambia shirika la habari la Reuters kwamba bado mapigano yanaendelea kwenye eneo linalouzunguka mji wa Alamata ambalo vikosi vya serikali vimesema viliudhibiti jana Jumatatu.

Katika hatua nyingine, Ethiopia imezizuia akaunti za benki zinazomilikiwa na taasisi za wafuasi wa chama cha Peoples Liberation Front cha Tigray, TPLF hii ikiwa ni kulingana na kituo cha televisheni chenye mahusiano na serikali cha Fana hii leo.

Aidha, kamati inayoandaa tuzo ya Amani ya kimataifa ya Nobel ya Norway ambayo mwaka jana ilimtunuku waziri mkuu Abiy kutokana na juhudi zake za kuleta amani kati ya Ethiopia na Eritrea imesema leo kwamba ina wasiwasi mkubwa na mzozo huo wa Tigray na kutaka pande zote kusitisha mapigano.

Kamati hiyo ya yenye makao yake, Oslo, chini Norway na ambayo huwa ni nadra sana kutoa maoni juu ya waliowahi kuwa washindi wa tuzo hiyo, imesema inaufuatilia kwa karibu mzozo huo na ina wasiwasi mkubwa.