Wasifu wa Watunzi | Noa Bongo | DW | 22.02.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Noa Bongo

Wasifu wa Watunzi

Ufuatao ni wasifu wa watunzi wa hadithi za mchezo wa Karandinga.

Carla Fernandes (privat)

Carla Fernandes

Carla Fernandes alizaliwa nchini Angola na ameishi Ureno. Baada ya kuhitimu Shahada yake ya Masomo ya Kutafsiri, alijiunga na Idhaa ya Kireno ya DW, ambako alikuwa akihusika zaidi na kuviandaa vipindi vya Noa Bongo, Jenga Maisha Yako katika lugha ya Kireno. ''Inaihusisha Jamii'' ni mchango wake wa kwanza katika michezo ya Karandinga, akiwa ni mtunzi wa hadithi hiyo. Kwa sasa Carla amerudi Ureno ambako amehitimu Shahada ya Uzamili ya Mawasiliano, Utamaduni na Teknolojia ya Habari. Ameendelea kufanya kazi kama mwandishi habari, mtayarishaji wa vipindi vya redio na ni mwanablogu. Pia ameanzisha blogu anayoweka zaidi vipindi vya redio. Blogu inaitwa ''Radio AfroLis'' na anazungumzia zaidi masuala yanayohusiana na jamii za asili za Afrika zinazoishi mjini Lisbon.

 

Hurcyle Gnonhoué (H. Gnonhoué)

Hurcyle Gnonhoué

Hurcyle Gnonhoué ni mtunzi na mwandishi wa riwaya kutoka Benin. Baadhi ya kazi zake zimechapishwa katika mkusanyiko wa hadithi fupi nchini Benin. Hadithi yake ya 'Les Pondeuses de boucs' ilichezwa wakati wa Tamasha la Kimataifa la Michezo ya Kuigiza la Benin-FITHEB. Hurcyle pia alifanya kazi kama mwandishi wa habari za kiutamaduni kwenye tovuti ya Bénincultures. Baada ya kujifunza masomo ya Fasihi nchini mwake, kwa sasa anamalizia Shahada yake ya Uzamili kuhusu Sanaa ya Kuigiza katika chuo kimoja nchini Ufaransa. ''Jinamizi la Mauaji'' ni hadithi yake ya kwanza aliyoitunga katika mfululizo wa michezo ya Karandinga.

 

Portrait Wanjiku Mwaura (DW/P. Böll)

Wanjiku Mwaura

Wanjiku Mwaura kutoka Kenya ni mshairi na mwandishi habari. Lugha na hasa kwa kupenda mashairi, Wanjiku ameigiza katika Majukwaa ya Kenya na nje ya nchi hiyo, kama vile Afrika Kusini na Ujerumani. Mashairi yake yamechapishwa kwenye majarida mbalimbali kama vile '' The Flow of My Soul''. Katika Karandinga, aliandika hadithi ya ''Bonyeza Kiunganishi''. Kabla ya kujiunga na Idhaa ya Kiingereza ya DW kwa ajili ya Afrika kama mhariri wa mitandao ya kijamii mwaka 2016, alikuwa akiigiza katika michezo mbalimbali ya redio ya DW.

 

Autor Sonwabiso Ngcowa (DW/G. Hilse)

Sonwabiso Ngcowa

Sonwabiso Ngcowa kutoka Afrika Kusini kwanza alipenda sana kusimulia hadithi wakati alipokuwa akisikiliza michezo ya redio akiwa mtoto. Alifanya kazi kwenye benki kwa miaka kadhaa kabla ya kufuata ndoto yake anayoipenda ya uandishi na hatimaye kuwa mwandishi na mshairi. Hadithi zake fupi za kwanza zilihusu mada muhimu kama vile ndoa za utotoni. Kitabu chake cha kwanza cha riwaya ''In Search of Happinness'' kinasimulia hadithi ya msichana ambaye anatokea kumpenda msichana mwingine Kitabu chake cha pili katika lugha ya Xhosa (lugha mama) chenye mkusanyiko wa hadithi fupi. Na kitabu chake cha tatu ni mkusanyiko wa mahojiano na ''born-frees'' nchini Afrika Kusini. Karandinga ilimuwezesha Sonwabiso kurejea katika hamu aliyokuwa nayo utotoni: michezo ya redio-lakini safari hii kama mtunzi. Ameandika hadithi ya ''Siri ya Mifupa''.

 

Pinado Abdu-Waba

Pinado Abdu-Waba

Pinado Abdu Waba kutoka Nigeria alianza safari yake ya kwanza kama mwandishi wa habari wakati akisomea Mawasiliano ya Umma huko Zaria, ambako alifanya kazi kwa muda mfupi katika redio ya chuo hicho ya ABU FM. Kisha aliendelea kufanya kazi kama mwandishi wa televisheni, na kisha kuhamia kwenye magazeti kama mmoja wa timu ya wahariri katika gazeti moja la kila siku. Ubunifu wa kuandika, siku zote limekuwa jambo analolipenda tangu akiwa na umri mdogo, lakini safari yake rasmi ilianza baada ya kujiunga na BBC Media Action iliyo chini ya Shirika la Utangazaji la Uingereza-BBC, kuandika na kutengeneza mfululizo wa vipindi vya redio, pamoja na kipindi cha majadiliano kuhusu maendeleo, katika lugha za Kiingereza na Kihausa. Vipindi hivyo viligusia maslahi yake, ikiwemo Utawala Bora, Afya ya Uzazi, Usalama wa Chakula pamoja na Utengenzaji wa Mali. Pina alijiunga na Idhaa ya Kihausa ya DW mwaka 2010 kama mhariri, ambako pia anaandaa vipindi vya Vijana na Uchumi. Hadithi ya "Chimbuko la Itikadi Kali" ni mchango wake wa kwanza katika utunzi kwenye mfululizo wa vipindi vyetu vya Karandinga.

 

 Autor James Muhando aus Kenia (DW/A.Gensbittel)

James Muhando

James Muhando ni Mkenya, ambaye kitaaluma ni msanii anayefanya kazi katika tasnia ya utunzi wa hadithi tangu mwaka 1999. Mwigizaji huyu na mtunzi alianza kuigiza jukwaani, lakini baadaye alijiunga na Shirika la Utangazaji la Kenya-KBC, kama mwandishi na muigizaji wa redio na televisheni. James ambaye anatamani sana kuwa mtayarishaji wa vipindi wa redio na televisheni, alijiunga na kitengo cha michezo ya kuigiza cha DW cha Noa Bongo Jenga Maisha Yako mwaka 2008 kama muigizaji na hatimaye kuwa miongoni mwa waandishi wa hadithi za michezo hiyo. Ameandika mojawapo ya hadithi katika mchezo wa "Karandinga: Wawindaji Haramu" na pia ni mtunzi wa hadithi za "Anasa ya Kuazima" na "Kizazi Njiapanda" awamu ya pili, tatu na ya nne. Aidha, James anasaidia utengenezaji wa vipindi vya redio vya michezo ya Karandinga kama mwaandaaji msaidizi mjini Nairobi, Kenya na pia alikuwa mwaandaaji msaidizi katika michezo ya Kizazi Njiapanda, mjini Dar es Salaam, Tanzania.

 

Chrispin Mwakideu DW Kommentarbild (DW)

Chrispin Mwakideu

Chrispin Mwakideu kutoka Kenya ni mchezesha vikaragosi, muigizaji na mtunzi aliyesomea. Kwa zaidi ya miaka 10 amekuwa akijihusisha na "Maendeleo ya Sanaa", kwa kutumia vikaragosi pamoja na michezo ya kuigiza kukabiliana na masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Kwa upande wake, uandishi wa michezo ya kuigiza ya redio yenye kuelimisha ni safari nzuri ya kusisimua. "Kama mtunzi, sijisikii tu kama sehemu ya hadithi ninayoandika, bali pia ninajifunza mambo mengi katika mchakato", anasema. Chrispin ni mtunzi wa hadithi ya "Unyakuzi wa Ardhi ya Chongwe" katika michezo ya Karandinga. Pia ameandika awamu ya kwanza ya mchezo wa redio wa Kizazi Njiapanda. Pia aliandika mfululizo wa hadithi za michezo ya Noa Bongo Jenga Maisha Yako kuhusu Ushiriki katika Siasa, Malaria na "Soka Barani Afrika ­– ni zaidi ya mchuano".

 

Mukoma wa Ngugi

Mukoma wa Ngugi

Mukoma wa Ngugi alizaliwa Evanston, Illinois Marekani na alikulia Kenya kabla ya kurejea tena Marekani. Ni mtoto wa mtunzi wa vitabu barani Afrika anayetambuliwa ulimwenguni kote, Ngugi wa Thiong'o na anafanya kazi kama Profesa Msaidizi wa Kiingereza katika Chuo Kikuu cha Cornell. Ni mtunzi wa hadithi za riwaya za Mrs. Shaw, Black Star Nairobi, Nairobi Heat na pia ametunga kitabu kimoja cha mashairi. Katika michezo mipya ya redio ya "Karandinga:, Mukoma ametunga hadithi ya Dawa za Kutibu, Dawa za Kuua".

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com