Washiya waadhimisha Ashura | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.01.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Washiya waadhimisha Ashura

Hatua kali za usalama kuepusha machafuko Kerbala na Najaf wakati huu ambao washiya wanaikumbuka siku aliyouwawa Imam Hussein katika jangwa la Kerbala

default

Washiya waadhimisha Ashura


Mapigano makali yameripuka leo mchana katika miji miwili ya kusini mwa Irak- Bassra na Nassiriyah,kati ya wafuasi wa madhehebu ya "Masiya" wa kishiya na vikosi vya usalama vya Irak.Mapambano hayo yamezuka katika wakati ambapo malaki ya washiya wanamiminika Kerbala-kusini mwa Baghdad kuadhimisha "maombolezi ya Ashoura",ambayo kilele chake kinafikiwa usiku wa leo kuamikia kesho.


Mjini Bassra "mapigano yameanza mchana kati ya vikosi vya usalama vya Irak na wafuasi wa kundi la madhehebu ya shiya wanaoongozwa na na Ahmad al-Hissani Al Yamani.Kiongozi huyo wa kidini anaejitaja kua "mjumbe wa Mahdi"-imam ambae washiya wanaamini siku moja atarejea tena duniani.


Mapigano kama hayo yameripuka pia Nassiriyah,kilomita 350 kusini mwa mjui mkuu wa Irak-Baghdad.Huko, wafuasi wanaojiita  pia wa madhehebu ya Messia wanaoongozwa na Al Yamani wamelishambulia jengo la polisi.Kwa mujibu wa mashahidi mashambulio yamekua yakiendelea mpaka jioni.


Mashambulio hayo yanajiri katika wakati ambapo washiya wanaadhimisha  Achoura-ambayo kilele chake kitafikiwa kesho jumamosi.


Malaki ya watu wakivalia nguo nyeusi wameminika Najaf na Kerbala,wakijipiga kifua hadi kutokwa na damu, kumkumbuka Imam Hussein, mjukuu wa Mtume Mohammad,aliyeuliwa mwaka 680 katika mapambano katika jangwa la Kerbala.


Zaidi ya waumini milioni mbili wanatazamiwa kuhudhuria Achoura mwaka huu.


Miji ya Kerbala na Najaf  inalindwa vikali.Askari polisi 24 elfu pamoja na askari kanzu wamewekwa katika maeneo hayo kulinda usalama.Hatua kali za usalama zimetangazwa pia katika mji mkuu Baghdad na katika maeneo mengine ambako maadhimisho ya Ashoura yanafanyika.


Waumini wote  wanaoingia Kerbala linakokutikana Quba la Imam Hussein wanasachiwa.Polisi 500 wakike wamewekwa maalum kwaajili ya kuwasachi mahujaj wakike.


Kuanzia jana usiku na kwa muda wa siku tatu,magari hayaruhisiwi kuzunguka mjini Baghdad ,katika eneo la kusini la Irak na katika jimbo la Diyala  pia.Katika mji wa Kirkouk marufuku hayo yanaanza leo usiku na uendelea hadi kesho usiku.


Tangu yaliporuhusiwa upya,baada ya kung'olewa madarakani Sadam Hussein,mwaka 2003,maadhimisho ya Ashoura sawa na maadhimisho mengine ya kidini ya washiya yamekua yakigubikwa na machafuko,mashambulio ya kuyatolea mhanga maisha na mapambano kwa mtutu wa bunduki.


Mwaka 2007 wafuasi karibu 300 wa kundi moja la Massiya wa kishiya, waliokua wakijiandaa kuushambulia mji wa Najaf,waliuliwa katika opereshini iliyoongozwa na wanajeshi wa Irak wakisaidiwa na wamarekani.


Mwaka jana,kumbukumbu nyengine za kidini,kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam wa mwisho wa washiya,Mahdi,zilichukua sura ya mapambano kati ya wanamgambo wa jeshi la Mehdi linaloongozwa na Moktadar el Sadr na polisi.Baada ya siku mbili za mapigano yaliyogharimu maisha ya watu 52,Moktadar el Sadr akatangaza mpango wa kuweka chini silaha unaoendelea kuheshimiwa mpaka hii leo.

►◄

 • Tarehe 18.01.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CuLa
 • Tarehe 18.01.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CuLa
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com