Wasemamavyo wahariri wa Ujerumani Jumatatu | Magazetini | DW | 06.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Wasemamavyo wahariri wa Ujerumani Jumatatu

Miito kwa Waislamu nchini Ujerumani kupaza sauti dhidi ya vitendo vya ukatili vya kundi la Dola la Kiislamu, Gharama za umeme na kufufuliwa tena mradi wa ndege ya uchunguzi isiyo na rubani magazetini

Mhariri wa gazeti la Stuttgarter Nachrichten, ameandika juu ya kupanda kwa bei za nishati ya umeme hapa Ujerumani, akisema mambo mengi yanakosekana katika utekeleezaji wa mkakati wa mabadiliko ya vyanzo vya nishati. Mtu anapata hisia kwamba wadau wa sekta ya nishati wameelekeza nguvu zaidi katika vyanzo vya nishati jadidifu. Mambo mengine mengi ambayo yalikuwa yanazungumziwa sasa hivi yamewekwa katika kaburi la sahau, kama vile uhifadhi wa nishati katika majengo. Kama majumba yangewekewa vifaa vya kuzuwia joto kutoka nje, kiwango kikubwa cha nishati kingeokolewa. Lakini viwango vya ukarabati vinaendelea kuwa nyuma kabisaa ya lengo, na sera ya taifa haijaweka vivutio kwa wawekezaji.

Baada ya wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu kumchinja dereva Taxi Muingereza Alan Henning, miito inazidi kutolewa hatua zaidi zichukuliwa kukomesha unyama wa kundi hilo. Wahari wa magazeti ya Mannheimer Morgen na Mittelbayerische Zeitung wamezungumzia ukatili wa kundi hilo. Lakini Mhariri wa gazeti la Mittelbayerische ametoa wito kwa Waislamu wa Ujerumani akihoji:

Wiki kadhaa zilizopita, Waislamu waliandamana kuonyesha mshikamano na Wapalestina kufuatia mashambulizi ya Israel dhidi ya ukanda wa Gaza. Kwa nini hii leo, baada ya mauaji kadhaa ya kinyama, tena mbele ya kamera, na kitisho cha mauaji ya halaiki, hakuna maandamano ya kuwapinga wale wanaotumia dini kama kisingizio cha kusababisha machafuko na ukatili? Ndiyo maana Waislamu nao wanatakiwa waonyeshe ghadhabu zao. Uislamu kama zilivyo dini nyingine, unatoa muongozo wa namna watu wanavyoweza kuisha pamoja, kuishi maisha yaliyokamilika na yenye furaha. Kama ilivyo chuki dhidi ya Wayahudi, chuki dhidi ya Uislamu pia ni tatizo la kijamii. Ikiwa Uislamu ni sehemu ya maisha nchini Ujerumani, basi unapaswa pia kuwa sehemu ya suluhisho la matatizo yanayoikabili jamii ya taifa hili.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen ameripotiwa kuwa na mipango ya kuufufua tena mpango wa ndege ya uchunguzi isiyo na rubani, Euro-Hawk, ambao uliwekwa kapuni na mtangulizi wake Thomas die Maiziere mwaka jana, baada ya kukumbwa na matatizo kadhaa. Juu ya kufufuliwa upya kwa mpango huo, mhariri wa gazeti la Hannoverschen Allgemeine ameandika:

Tatizo la waziri Thomas de Maiziere katika mwaka uliyopita ni kwamba hakulichukulia kwa uzito suala la ndege hiyo. Alitoa majukumu hayo kwa katibu mkuu wake, ambaye hivi sasa amefukuzwa na waziri Ursula von der Leyen. Die Maiziere alikuwa akifanya maamuzi kwa kufuata nyaraka, badala ya kuliangalia suala hilo kwa kina na kutafuta njia za kuiidinisha ndege ya Euro-Hawk nchini Ujerumani. Halikupaswa kuwa jambo lisilowezekana, kwa sababu ndege hiyo inafanyakazi nchini Marekani na hata Italia kwa miaka kadhaa bila kupata ajali. Pamoja na mada nyingi na jumbe za nje anazojishughulisha nazo waziri von der Leyen, anapaswa kulifanya suala hilo kuwa la kipaumbele. Pengine anaweza kuwa na mafanikio kuliko mtangulizi wake, ambaye alidhihakiwa isivyo haki kwa kuitwa majina.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/Deutsche Zeitungen
Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman