1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanne zaidi waokolewa Thailand

Lilian Mtono
9 Julai 2018

Vijana wanne zaidi waliokuwa wamekwama kwenye pango la lililofurika maji kaskazini mwa Thailand, wameokolewa hii leo na kufanya idadi jumla ya waliookolewa hadi sasa kufikia wanane kati ya 13.

https://p.dw.com/p/315TD
Thailand Rettungsaktion Tham Luang Höhle
Picha: Reuters/Soe Zeya Tun

Vijana hao ambao ni wachezaji wa timu ya soka ya vijana waliokwama kwenye pango hilo kwa zaidi ya wiki mbili sasa walianza kutolewa pangoni humo jana jioni.

Matangazo ya moja kwa moja yaliyokuwa yakirushwa na kituo cha televisheni cha eneo hilo cha Thai PBS hii leo, yalionyesha magari ya kubeba wagonjwa na helikopta yakiwachukua vijana wengine watatu kutoka eneo hilo la pango na kuwapeleka hospitali, na muda mfupi baadae kijana mwingine pia alipelekwa hospitalini hapo. 

Msaidizi wa kamanda wa jeshi la maji nchini Thailand, amethibitisha taarifa za kuokolewa kwa vijana hao wanne na idadi hii ikimaanisha kwamba, bado vijana wengine watano wamekwama pangoni humo, baada ya wengine wanne kuokolewa hapo jana.

Kwenye ukurasa wake wa Facebook, jeshi hilo la maji limeorodhesha vijana hao wanane waliookolewa kutoka kwenye pango hilo, wakiwaandika kwa majina maalumu ya "Wild Boar", namba 1 hadi 8 ili kuficha utambulisho wa waliookolewa.

Thailand Höhle | Rettungsaktion Jugendliche
Picha inayoonyesha baadhi ya vijana waliokwama kwenye pango hilo, ambao tayari baadhi yao wamelokolewaPicha: Reuters/S. Z. Tun

Kaimu gavana wa jimbo la Chiang Rai, Narongsak Osatanakorn amesema mapema hii leo, baada ya operesheni hiyo kuanza kwamba awamu walitarajia habari njema baada ya muda mfupi, wakati vijana tisa wakiwa bado wamekwama kwenye pango hilo, ikiwa ni pamoja na kocha wao. Alisema operesheni ya leo ingefanyika kwa haraka zaidi kutokana na hofu ya mvua kubwa, ambayo mamlaka ya hali ya hewa ilitangaza kuwa itanyesha na kudumu kwa wiki nzima, kuanzia mchana wa leo.

Bado hawajaweza kukutana na familia zao.

Narongsak ambaye pia ni msimamizi wa operesheni hiyo amesema, vijana waliookolewa jana wanaendelea vizuri na asubuhi ya leo waliomba chakula. Bado wanafanyiwa uchunguzi wa kiafya katika hospitali hiyo iliyopo katika mji mkuu wa jimbo hilo na bado hawajaruhusiwa kukutana na jamaa zao.

Kulingana na gavana huyo, ndugu zao waliweza kuwaona kupitia vinavyotenganisha vyumba walimolazwa. 

Awali, mamlaka zilisema operesheni ya kuwaokoa vijana wote huenda ikachukua hadi siku nne, lakini mafanikio yaliyofikiwa jana Jumapili yaliibua matarajio kwamba inaweza kufanyika kwa muda mfupi. 

Operesheni ya jana, ilihusisha wataalamu wa kuogelea 13 kutoka nje, na watano wa jeshi la maji la Thailand. Wazamiaji wawili waliwasaidia vijana hao kuogelea, baada ya kujifunza tangu Julai 2, baada ya timu hiyo kugundua mahala walipo.

Vijana hao na kocha wao walienda kutembelea pango hilo la Tham Luang Nang Non Juni 23, baada ya mazoezi ya mpira, na kushindwa kutoka kutokana na mafuriko, baada ya mvua kubwa kunyesha. Kulianzishwa operesheni kubwa ya kimataifa ya kuwatafuta vijana hao na imechukua siku 10 hadi kuwaona wakiwa wamejificha eneo kavu ndani ya pango hilo.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/DPAE

Mhariri: Mohammed Khelef