1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanasheria Tanzania wajitosa sakata la kukodisha bandari

8 Juni 2023

Chama cha wanasheria nchini Tanzania cha Tanganyika Law Society (TLS) kimejitosa katika sakata la umilikishwaji wa bandari baada ya serikali kuanzisha makubaliano ya awali na kampuni moja ya kigeni ya DP World.

https://p.dw.com/p/4SLpw
Sehemu ya bandari ya Dar es Salaam kama ilivyokuwa ikionekana Aprili, 2020 wakati ilipokuwa ikifanyiwa upanuzi.
Picha: Xinhua News Agency/picture alliance

Hatua hiyo inafuatia mjadala mkubwa unaoendelea nchini humo huku wengi wakionyesha wasiwasi kuhusiana na mazingira ya makubaliano hayo wakihofia huenda nchi hiyo ikabanwa katika siku za usoni. 

Kujitosa kwa TLS kunakuja wakati mjadala juu ya suala hilo, ukisubiriwa kujadiliwa na bunge ambalo ndilo lenye dhima ya kupitisha makubaliano hayo yatakayofahamika kama azimio la bunge kuhusu ukodishwaji wa bandari za Tanzania kwa mwekezaji wa kigeni.

Hivyo, chama hicho cha wanasheria kimeeleza jinsi kinavyoendelea kuufuatilia mjadala huo ambao kiini chake ni makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu usimamizi wa bandari  zilizoko nchini ikiwemo bandari kongwe ya Dar es salaam bandari ambayo inayaunganisha mataifa kadhaa ya jirani.

Makamu wa Rais wa TLS, Wakili Aisha Sinda, amesema kutokana na unyeti wa suala hilo na namna linavyoendelea kuvuta hisia za wengi, chama hicho kimelazimika kuunda jopo la wataalamu watakaokuwa na jukumu la kuupitia mkataba huo ambao nakala zake zimesambaa kwa umma.

Meli za makontena zikiwa zimetia nanga katika eneo la bandari ya Dubai linaloendeshwa na kampuni ya Dubai World.
Sakata la ukodishaji wa bandari limeibua mjadala mzito nchini Tanzania, wengi wakionyesha wasiwasi na makubaliano ya aina hiyo.Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Jebreili

Wajumbe wanaounda kamati hiyo ambao ni wanachama wa TLS ni wataalamu wa masuala ya sheria za mikataba ambao pamoja na mambo mengine watakuwa na kazi ya kupitia na kufanya uchambuzi wa kisheria juu ya makubaliano hayo.

Kamati hiyo iliyoundwa na Rais wa TLS, Wakili Harold Sungusia haijaelezwa ni lini inaanza kazi yake ingawa imesalia na siku tano kuanzia leo kabla ya kuwasilisha ripoti yake kwa Baraza la Uongozi la chama hicho.

Wengi wanasubiri kuona namna bunge hilo litakavyolijadili jambo hilo ingawa wakati mmoja kulijitokeza sura ya mgawanyiko miongoni mwa wabunge hao wakati walipokuwa wakiijadili bajeti ya wizara ya ujenzi na uchukuzi.

Miongoni mwao waligawanyika; kwa baadhi kutilia shaka namna mkataba huo ulivyoundwa na jinsi kampuni hiyo itakavyopewa idhini ya kusimamia bandari zilizoko nchini. Lakini wengine waliegemea upande wa serikali wakitoa heko kwa kuorodhesha ufanisi utakaojitokeza wakati ubinafsishaji huo utakapokamilika.

Sehemu kubwa ya wale wanaolijadili suala hilo wanaitupia macho bandari ya Dar es salaam ambayo licha ya kutoa huduma zake kwa sehemu kubwa ya Tanzania pia imekuwa kiunganishi muhimu kwa mataifa mengine kama vile Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Rwanda, Malawi, Burundi, Uganda na hata Zimbabwe.

Sikiliza Zaidi: 

Upi msimamo wa serikali juu ya uendeshaji wa bandari?