Wananchi Ivory coast wapiga kura | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.10.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wananchi Ivory coast wapiga kura

Zoezi la upigaji kura limeanza hii leo nchini Ivory Coast katika uchaguzi unaoashiria kumpa ushindi Rais wa sasa wa nchi hiyo Alassane Outtara kuongoza taifa hilo kwa muhula wa pili wa uongozi .

Rais wa sasa wa Ivory Coast Alassane Ouattara

Rais wa sasa wa Ivory Coast Alassane Ouattara

Ouattara ambaye uongozi wake umesaidia taifa hilo la Afrika magharibi kuwa moja ya mataifa yenye uchumi imara barani Afrika anakabiliwa na upinzani kutoka kwa makundi kadhaa, ingawa kuwepo kwa mgomo kutoka kwa baadhi ya vyama kunaweza kupunguza idadi ya wapiga kura.

Tume ya uchaguzi yatumia tekinolojia ya kisasa.

Zaidi ya wapiga kura milioni 6, wamejiandikisha kupiga kura katika vituo 20,000. Tume ya uchaguzi nchini humo mwaka huu imekuja na tekinolojia mpya ya kisasa itakayosaidia kurahisisha kutambua wapiga kura.

Uchaguzi huo uliokuwa umepangwa kuanza saa moja asubuhi leo, ulichelewa katika maeneo mengi baada ya kukawia kwa vifaa vya kupigia kura.

Saa moja baada ya muda rasmi wa kuanza kwa zoezi hilo la upigaji kura asilimia 57 ya vituo vya upigaji kura vilikuwa tayari vimefunguliwa.

Baadhi ya mashuhuda wamethibitisha zoezi hilo kwenda kwa amani katika mji mkuu wa biashara Abidjan na katika miji ya Man, Gagnoa na Korhogo.

Wakati hayo yakiendelea chama cha Rais wa zamani wa nchi hiyo Laurent Gbagbo kimetangaza kususia uchaguzi huo.

Hatua ya Rais Gbagbo kukataa kuutambua ushindi wa Ouattara katika uchaguzi wa mwaka 2010 ilisababisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Gbagbo kwa sasa anakabiliwa na kesi katika mahakama ya uhalifu ya kimataifa iliyoko The Hague, Uholanzi.

Endapo uchaguzi huo utakwenda kwa amani utasaidia kuvutia wawekezaji katika taifa hilo ambalo linaongoza kwa uzalishaji wa zao la kakao duniani.

Mwandishi: Isaac Gamba/RTRE

Mhariri : Gakuba Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com