1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanamgambo waua watu 47 nchini Burkina Faso

19 Agosti 2021

Rais wa Burkina Faso Roch Marc Christian Kabore ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanzia Alhamisi, baada wanamgambo kuwaua watu 47 miongoni mwao raia 30 kufuatia shambulizi kaskazini mwa nchi hiyo. 

https://p.dw.com/p/3z9qb
Symbolbild I Sicherheitskräfte Burkina Faso
Picha: Ahmed Ouoba/AFP/Getty Images

Shambulizi hilo la jana Jumatano katika mji wa Gorgadji ndilo la hivi karibuni zaidi katika Eneo hilo linalokumbwa na machafuko kutoka kwa wanamgambo. Raia 30, wanajeshi 14 na askari watatu wa kujitolea kama sungusungu ni miongoni mwa waliouawa, kwa mujibu wa wizara ya habari ya nchi hiyo.

Shambulizi hilo lilitokea wakati wanajeshi na askari wa kujitolea walikuwa wakiwapa ulinzi raia waliotoka mji mwingine wa kaskazini mwa nchi hiyo Arbinda. Kufuatia majibizano makali ya risasi, wanajeshi wa serikali pamoja na askari wa kujitolea waliwaua wanamgambo 58 waliowataja kuwa magaidi. Watu wengine 19 pia walijeruhiwa. Kwa mujibu wa wizara ya habari, shughuli za uokozi na utoaji msaada zinaendelea.

Soma pia: Viongozi wa nchi za Afrika Magharibi wakaa kimya kimya na makundi ya wanamgambo

Soma pia: UN: Mamilioni wahitaji msaada wa kiutu Sahel

Eneo hilo ambalo liko karibu na mpaka wa Mali na Niger, hukumbwa na machafuko ya mara kwa mara kutoka kwa wanamgambo wenye itikadi kali za kidini ambao wamekuwa wakihangaisha utulivu katika kanda hiyo ya Sahel, Afrika Magharibi.

Hilo lilikuwa shambulizi la tatu dhidi ya wanajeshi wa Burkina Faso katika majuma mawili yaliyopita. Mnamo Agosti 14 wanamgambo walifanya shambulizi karibu na mpaka na Niger na kuua watu 30 miongoni mwao raia 11.

Kufuatia shambulizi la jana, Rais Roch Marc Christian Kabore ametangaza siku tatu za taifa kuomboleza kuanzia Alhamisi, ambapo bendera zitapeperushwa nusu mlingoti katika majengo ya serikali. Aidha kulingana na agizo la rais, hafla za sherehe zitapigwa marufuku katika kipindi hicho cha maombolezo.

Wanajeshi wa Burkina Faso wamezidisha operesheni na misako kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo kukabiliana na wanamgambo.
Wanajeshi wa Burkina Faso wamezidisha operesheni na misako kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo kukabiliana na wanamgambo.Picha: Ahmed Ouoba/AFP/Getty Images

Ufaransa na nchi za Sahel kutathmini vita dhidi ya makundi ya kigaidi

Tangu mwaka 2015, Burkina Faso ambalo ni taifa maskini katika kanda kavu ya Sahel, limekuwa likipambana dhidi ya mashambulizi hatari ya mara kwa mara kutoka kwa makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali za dini Jihad wanaohusishwa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS pamoja na mtandao wa Al-Qaeda.

Mnamo Juni 4 na Juni 5, watu waliokuwa na bunduki waliwaua watu 132, miongoni mwao watoto katika kijiji cha Solhan, kaskazini mashariki mwa Burkina Faso. Hilo lilikuwa shambulizi baya zaidi katika historia ya machafuko ya wanamgambo nchini humo.

Serikali imeimarisha operesheni na misako kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo karibu na mipaka yao na Niger na Mali.

Kulingana na makadirio rasmi ya serikali, zaidi ya watu 1,400 wameuawa na wengine milioni 1.3 kulazimishwa kuyakimbia makaazi yao kutokana na mashambulizi ya wanamgambo.

HRW: Makaburi ya halaiki yagunduliwa Burkina Faso

Machafuko katika kanda hiyo ya Sahel inadaiwa kuanza mnamo mwaka 2012, wakati wanamgambo wenye mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda waliibuka kaskazini mwa Mali. Hatua hiyo ilililazimisha jeshi la Ufaransa kuingilia kati kuwakabili na kuwatawanya. Lakini baadaye, wanamgambo hao walikusanyika tena na kuingia katika nchi jirani.

(AFPE)