Wanajeshi wa zamani warudi kambini Afrika ya Kati | Matukio ya Afrika | DW | 13.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Wanajeshi wa zamani warudi kambini Afrika ya Kati

Wanajeshi kadhaa waliojiunga na wanamgambo wa Kikristo kumpinga Muislamu wa kwanza kuwa rais katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Michel Djotodia, wamerejea kambini leo baada ya usimamishaji mapigano na Djotodia kujiuzulu.

Wizi wa ngawira wakisaidiana katika mji wa Bangui baada ya machafuko kuzuka.

Wizi wa ngawira wakisaidiana katika mji wa Bangui baada ya machafuko kuzuka.

Wanajeshi hao, ambao takriban wote walikuwa wamevalia nguo za kiraia wakihofia kutambuliwa wakati walipolikimbia jeshi, walionekana leo wakijiandikisha upya kazini, kutokana na wito uliotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Majeshi, Jenerali Ferdinand Bomboyeke, ambaye aliwataka kurudi kambini.

Tukio hilo linafuatia usimamishaji mapigano jana kati ya makundi hasimu ya wanamgambo baada ya kujiuzulu Djotodia, ambaye sasa anasemekana ameomba hifadhi nchini Benin. Wanamgambo hao walionekana wakikumbatiana katika vitongoji vya mji mkuu Bangui .

Kapteni Souleyman Daouda, afisa wa wanamgambo wa Seleka waliomuangusha rais wa zamani Francois Bozize mwezi Machi mwaka jana na kumuweka madarakani Djotodia, alisikika akisema kwamba huu ni wakati wa furaha. Djotodia na waziri wake mkuu Nicolas Tiangaye walijiuzulu kutokana na shinikizo la kimataifa.

Mahasimu waafikiana

Wakimbizi wa ndani wakisaidiana wenyewe kwa wenyewe mjini Bangui.

Wakimbizi wa ndani wakisaidiana wenyewe kwa wenyewe mjini Bangui.

Pande mbili hasimu zilifikia makubaliano katika kitongoji cha Bimbo katika mji mkuu Bangui mwishoni mwa juma kutokana na upatanishi wa wanajeshi wa kusimamia amani wa ufaransa na mataifa ya Afrika.

Mwanajeshi mmoja aliyejiunga na wanamgambo wa Kikristo, Davy Louis Parfait, alisema pamoja na kuwa aliwauwa waasi wa Seleka lakini kufikia hatua ya kusimamisha mapigano ni faraja kubwa kwake.

Rais wa mpito Alexandre-Ferdinand Nguedent aliyeteuliwa na bunge la nchi hiyo lililokutana katika kikao maalum katika mji mkuu wa Chad N'Djamena, alifika kwenye uwanja wa ndege wa Bangui, mahala kulikojazana umati wa karibu watu 10,000 waliokimbilia kunusuru maisha yao, na kuwataka warudi kwenye makaazi yao.

Kinachosubiriwa hivi sasa baada ya Djotodia kujiuzulu, ni mpango wa maafisa wa serikali mpya kuandaa uchaguzi utakaokuwa huru na wenye uwazi na wa kidemokrasia, ili kuikwamua Jamhurui ya Afrika kati kutokana na mgogoro huu wa kisiasa.

Majadiliano rasmi kuanza

Rais aliyeodoka madarakani, Michel Djotodia (kushoto) akizungumza na wajumbe wa kikao kilichoamua ajiuzulu.

Rais aliyeodoka madarakani, Michel Djotodia (kushoto) akizungumza na wajumbe wa kikao kilichoamua ajiuzulu.

Baraza la Taifa la Mpito ambalo ni bunge la muda, limetangaza kwamba litaanza majadiliano leo pamoja na wanasiasa na wajumbe wa jumuiya za kiraia katika jaribio la kumchagua atakayechukua nafasi ya Djotodia na kuliongoza taifa hilo hadi uchaguzi.

Rais wa mpito hatokuwa mgombea katika uchaguzi ujao. Ufaransa mkoloni wa zamani Jamhuri ya Afrika ya Kati inaongoza jitihada za kimataifa kumaliza mgogoro huo, na inataka uchaguzi ufanyike mwishoni mwa mwaka huu .

Baada ya matukio ya mwishoni mwa juma, hali kwa wakati huu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ni ya utulivu, licha ya visa vidogo vidogo vya uporaji mali katika baadhi ya vitongoji vya mji mkuu Bangui.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/ AFP/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba