Wanajeshi wa MONUSCO wapiga doria Kongo | NRS-Import | DW | 02.08.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Wanajeshi wa MONUSCO wapiga doria Kongo

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanapiga doria katika eneo jipya la usalama mashariki mwa nchi hiyo. Muda uliotolewa kwa waasi kusalimisha silaha zao ulipita jana. (01.08.2013)

United Nations troops patrol on the road to Sake, 27kms from the provincial capital of Goma, in the Democratic Republic of the Congo, on 04 November 2008. The United Nations and international aid organization are fighting an uphill battle to get help to over 250,000 people that are thought to have been forced from their homes and villages. EPA/STEPHEN MORRISON +++(c) dpa - Report+++

UN Blauhelme Kongo Miliz

Makundi ya waasi katika viunga vya mji wa Goma walipewa hadi saa kumi jana jioni kusalimisha silaha zao kwa tume ya Umoja wa Matiafa ya kulinda amani nchini Kongo, MONUSCO, na wajiunge na mpango wa kuwahamasiha dhidi ya uasi. Tangu muda huo kupita jana, hadi sasa haijabainika ni wapiganaji wangapi waliouitikia mwito wa kuwasilisha silaha, ambao kundi la waasi wa M23 lilisema hauna maana yoyote.

Umoja wa Mataifa haukudokeza kama harakati ya kijeshi imeshaanza au ilikuwa imepangwa katika eneo hilo linalokabiliwa na machafuko. "Wanajeshi wa MONUSCO wanapiga doria wakiwasaidia wanajeshi wa Kongo. Hii itakuwa operesheni itakayoendelea kuwalinda raia katika maeneo yenye wakazi wengi," amesema Kieran Dwyer, msemaji wa tume hiyo ya amani.

Eneo la usalama linaujumuisha mji wa Goma na vitongoji vya kaskazini mwa mji huo, ukiwemo mji wa Sake. Mjini Goma, kamanda wa MONUSCO, Jenerali Carlos Alberto Dos Santos Cruz alifafanua jana kwamba muda wa saa 48 uliotolewa ulikuwa fursa kwa waasi kushiriki kwa hiari katika mchakato wa kutafuta amani.

Brasilianischen General Carlos Alberto dos Santos Cruz, neuer Kommandant der Monusco in der Demokratische Republik Kongo, UNO Copyright: Spensy Pimentel/ABr, Das Bild ist von der brasilianischen Agentur Agência Brasil und steht der Presse im Allgemein zur Verfügung. Zugeliefert von DW/Alex Schossler

Jenerali Carlos Alberto dos Santos Cruz

"Fursa hii imetolewa kwa sababu lengo ni kuhakikisha wakaazi wako salama katika eneo hili. Kwa kuwa kuna kambi za wakimbizi wa ndani kando ya barabara mjini Goma na Sake, tuna zaidi ya watu milioni moja, na tunahitaji kuweka mazingira kuwawezesha watu kuwa na maisha ya kawaida bila machafuko." Cruz aidha alisema mpango huo haukuwa ukiyalenga makundi maalumu katika eneo hilo, ambako makundi yapatayo 30 yaliyojihami na silaha yanaendesha shughuli zao. Wanadiplomasia wanasema machafuko mapya nchini Kongo yamesababisha vifo vya mamia ya raia.

Umoja wa Mataifa kuchukua hatua

MONUSCO imesema kama makundi kama M23 hayatawasilisha silaha zao, yatachukuliwa kama kitisho cha machafuko dhidi ya raia na tume hiyo itachukua hatua zote zinazostahili kuwapokonya silaha. Lakini msemaji wa kundi la M23, Bertrand Bisimwa, amesema hatua hiyo haiwahusu, kwa sababu wapiganaji wao hawako eneo la kusini mwa mji wa Goma, ambako mapigano mengi yamekuwa yakiendelea katika siku za hivi karibuni.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa ulitangaza jana umeamuru ndege zisizokuwa na rubani kwa ajili ya uchunguzi zitumwe mashariki mwa Jamhuri ya Kimokrasia ya Kongo kutoka kwa kampuni moja ya Italia, kusaidia katika kufanya doria katika eneo hilo.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekabiliwa na machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji mnamo mwaka 1960. Machafuko nchini humo mara kwa mara huchochewa na utajiri mkubwa wa madini yanayowavutia majirani zake.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com