1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafunzi karibu 80 watekwa Kaskazini Magharibi mwa Cameroon

Sylvia Mwehozi
6 Novemba 2018

Wanafunzi karibu 80 na wafanyakazi wa shule wametekwa, kwenye mkoa unaozungumza kiingereza nchini Cameroon. Tukio hilo limetokea mnamo rais Paul Biya akitarajiwa kuapishwa tena kwa muhula wa saba madarakani. 

https://p.dw.com/p/37iTn
Kamerun Nigeria Angst vor Boko Haram in Fotokol
Picha: KAZE/AFP/Getty Images

Gavana wa mkoa wa kaskazini magharibi Deben Tchoffo amesema wanafunzi hao waliotekwa usiku wa Jumapili, walikuwa na umri wa kati ya miaka 11 na 17 na walichukuliwa kutoka kijiji cha Nkwen kilicho karibu na mji wa Bamenda, sambamba na wafanyakazi akiwemo mkuu wa shule. "Licha ya kilichotokea, serikali haiwezi kurudi nyuma. Tutahakikisha watu wote na wanafunzi,  waliotekwa wanarejea katika madarasa na hatua kali zinachukuliwa na vikosi vya usalama kuhusiana na hilo", alisema gavana huyo. 

Mkanda wa vidio unaodaiwa kuwaonyesha wanafunzi waliotekwa, uliwekwa katika mitandao ya kijamii na kundi la wanaume wanaojiita Amba boys, ikimaanisha taifa la Ambazonia ambalo linataka kuanzishwa na kundi la wanaotaka kujitenga waliojihami kwa silaha, katika mikoa ya kaskazini magharibi na kusini inayozungumza Kiiingereza nchini Cameroon.

Kamerun Präsident Paul Biya
Rais wa Cameroon Paul Biya aliyeko madarakani tangu 1982Picha: picture-alliance/AP Photo/Lintao Zhang

Kwenye mkanda huo, wanaume hao waliojitambulisha kama watekaji waliwalazimisha wavulana kadhaa kutaja majina yao na ya wazazi wao. Wavulana hao wamesema pia walisema walichukuliwa na kundi la wanaume wenye silaha jioni ya Jumapili na hawajui wapi wanashikiliwa.

Wanaume hao wamesikika katika vidio hiyo wakisema watawaachia wanafunzi hao pindi lengo lao la kuanzisha nchi mpya litakapotimia. Hata hivyo uhalali wa vidio hiyo haukuweza kuthibitishwa, lakini wazazi wamesema kupitia mitandao ya kijamii kwamba walau wameweza kuwatambua watoto wao.

Mapigano baina ya jeshi na wanaotaka kujitenga yameongezeka baada ya serikali kukabiliana na maandamano ya amani yalofanywa na wafanyakazi wa kada ya ualimu na wanasheria kutoka mikoa inayozungumza kiingereza wanaopinga kutengwa na serikali ya Cameroon yenye idadi kubwa ya wazungumzaji Kifaransa.

Kamerun Polizisten in Buea
Polisi wakifanya doria kwenye jimbo linalozungumza kiingereza la Buea Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Mamia ya watu wameuawa mwaka jana. Kundi la wanaotaka kujitenga limeapa kurejesha utulivu kwenye mikoa hiyo kama sehemu ya mkakati wa kuanzisha taifa lao. Wamevamia raia wasiounga mkono hoja hiyo, wakiwemo walimu waliouawa kwa kukiuka maagizo ya kuzifunga shule.

Kumekuwepo na utekaji katika shule nyingine, lakini kundi la mateka lililochukuliwa Jumapili ni kubwa kulinganisha na matukio mengine. Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International limeitaka serikali ya Cameroon kufanya kila linalowezkana kuhakikisha wanafunzi hao wanapatikana.

Zahama hiyo nchini Cameroon inakuja baada ya rais Paul Biya kushinda uchaguzi mwezi uliopita kwa muhula wa saba na alitarajiwa kuapishwa siku ya Jumanne.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP

Mhariri: Bruce Amani