1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakulima wakabiliwa na ukame Kusini mwa Jangwa la Sahara

Grace Kabogo Mirriam Kaliza
6 Machi 2024

Idadi kubwa ya wakulima wadogo wadogo wanakabiliwa na ukame mkubwa unaosababisha mazao yao kunyauka katika maeneo mengi ya Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.

https://p.dw.com/p/4dDCU
Athari ya ukame katika mazao
Athari ya ukame katika mazaoPicha: DW

Ruzuku za serikali zinaweza kuwasaidia wakulima hao kwa kiasi kikubwa, huku mahitaji ya kupatikana ufumbuzi yakiongezeka, ingawa yanatekelezwa taratibu. 

Hatimaye mvua zimeanza kunyesha Malawi, baada ya wiki kadhaa za ukame, lakini bado ni ndogo na zimechelewa kwa mkulima kama Saidi M'madi. Mkulima huyo ameiambia DW kuwa mwezi Desemba walipoteza kila kitu, hivyo waling'oa mazao waliyopanda sababu yaliharibika na kuanza upya.

Matumaini pekee ya M'madi ni serikali kuendelea kuingilia kati kadri inavyoweza na kusaidia kutoa ruzuku kwa wakulima.

''Hatuna matumaini, wengi wetu tunategemea kilimo kidogo kwa ajili ya chakula, lakini sasa hatujui nini cha kutarajia au cha kufanya. Tunaiomba serikali kutusaidia na chakula, kama vile mwaka jana, sababu hatuna tena chakula.''

Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa na Kamati ya Kutathmini Athari nchini Malawi, MVAC, nchi hiyo kwa sasa inawasaidia watu milioni 4.4. Takwimu hizo zilizotolewa Agosti mwaka uliopita, zinaonyesha kuwa wale wanaosaidiwa na serikali ni takribani asilimia 22 ya wakaazi milioni 19.6 wa Malawi, hadi asilimia 15 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

FAO na WFP waeleza hofu kutokana na ukame

Baadhi ya watu nchini Zambia waliopokea msaada wa chakula kutoka shirika la mpango wa chakula WFP
Baadhi ya watu nchini Zambia waliopokea msaada wa chakula kutoka shirika la mpango wa chakula WFPPicha: Guillem Sartorio/AFP/Getty Images

Taarifa ya pamoja ya Shirika la Chakula na Kilimo, FAO, na Mpango wa Chakula Duniani, WFP imeeleza kuwa baada ya ukame wa mara kadhaa, Malawi sasa inakabiliwa na uhaba mkubwa zaidi wa chakula katika muongo mmoja, kwani asilimia 90 ya ardhi inayolimwa Malawi inategemea mvua.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema kwengineko katika nchi ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, mataifa mengi yanakabiliwa na viwango sawa vya ugumu wa maisha. FAO, na WFP yanakadiria kuwa watu milioni 27.4 wa kusini mwa Afrika, watakabiliwa na njaa katika miezi sita ijayo kutokana na mavuno duni, kufuatia ukame uliokithiri mara 14 ndani ya miongo miwili iliyopita, zaidi ya bara jingine lolote.

Mzozo wa ukame unatokea miaka miwili baada ya Faharasa ya Njaa Ulimwenguni kuzitathmini nchi 37 kati ya 54 za Kiafrika kama zilizofikia viwango vya njaa vinavyoelezewa kuwa "vikubwa" au vibaya zaidi. Kulingana na Umoja wa Mataifa, maeneo yanayokabiliwa na vitisho ni pamoja na Madagascar na Zimbabwe.

Katika nchi jirani ya Zambia, hadi asilimia 70 ya mashamba ya kilimo pia yameshuhudia ukame kama huo katika jimbo la Eastern Province. Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema ametangaza ukame kuwa janga la kitaifa baada ya wilaya 84 kati ya 116 kutopata mvua kwa zaidi ya wiki tano, akisema kuwa zaidi ya familia milioni 1 za wakulima wa Zambia zitaathirika.

Miito kwa serikali kuanzisha mipango ya uzalishaji wa mazao

Wakulima nchini Ivory Coast wakiandaa mashamba kabla ya mvua
Wakulima nchini Ivory Coast wakiandaa mashamba kabla ya mvuaPicha: DW

Profesa Zachary Kasomekera, mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Kilimo na Maliasili cha Lilongwe, LUANAR, ameiambia DW kuwa serikali zinapaswa kuanzisha mipango mikubwa ya uzalishaji wa mazao kwa mtindo ambao anauita "mashamba makubwa."

''Mtazamo wangu na msisitizo ni kwamba nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara zinapaswa kuyaweka maji kama kipaumbele. Ili unapokuwa na maji mengi unavuna, ukiwa na maji kidogo uyatumie.

"Tulikuwa na mafuriko, tulipoteza mali, tulipoteza maisha na hapa tulipo mwaka huu, tunakumbwa na ukame. Na ndio, harakati zinapaswa kuyafanya maji kuwa kipaumbele.''

Miongoni mwa wale wanaousaidia mpango huo ni shirika la FAO, ambalo linafanya kazi na serikali ya Malawi kukarabati miradi 34 ya umwagiliaji.

Mpango wa Pembejeo Nafuu AIP, ambao awali ulitambulishwa kama Mpango wa Ruzuku ya Pembejeo za Shamba, FISP, mwaka 2004, ulikusudia kuongeza tija ya kilimo na kuzisaidia kaya zenye uhaba wa kipato.

Lakini je, ni kweli Afrika inaweza kubadilika na kutegemea mvua, ilhali ruzuku ya serikali ndiyo njia pekee iliyosalia kwa wakulima wengi?