1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakulima wa kakao Ghana wahifadhi misitu

7 Septemba 2018

Serikali ya Ghana, pamoja na mashirika ya kilimo cha zao la kakao yamesema sera inayowezesha wakulima kumiliki miti ya mbao iliyomo kwenye mashamba yao ya kakao huenda ikawasaidia wakulima kuboresha mashamba

https://p.dw.com/p/34UW9
Ghana Kakao-Anbau
Picha: picture-alliance/robertharding

Miti hukua yenyewe kwenye mashamba mengi ya kakao, na kuweka vivuli kwenye mimea hiyo inayohitaji uangalizi mkubwa. Lakini ni mali ya serikali, na si wakulima, hii ikiwa ni kulingana na sheria za misitu za taifa hilo la Afrika Magharibi.

Makampuni huilipa ada serikali ili kupasua mbao, wakati wakulima wa kakao wakiwa wanaathirika, kwa kuwa miti ya zao hilo mara nyingi huharibika wakati wa mchakato wa kupasua mbao, hivyo kushindwa kuzalisha lakini pia kwa kuwa hupigwa jua.

Lakini kifungu ambacho hata hivyo wengi hawakijui kilichoingizwa kwenye sheria hiyo ya misitu kinaruhusu wakulima kusajili umiliki wa miti ya mbao waliyoipanda wao wenyewe.

Ingawa sheria hiyo sio mpya, haijawahi kujaribiwa hadi mwaka huu, chini ya mradi wa majaribio unaoungwa mkono na wakfu wa zao la kakao duniani, World Cocoa Foundation, WCF, katika mkoa wa Amenfi Magharibi.

Ghana Kakao-Anbau
Mkulima wa Kakao nchini GhanaPicha: picture-alliance/robertharding

Meneja wa tume ya misitu aliyeko katika mji mkuu wa mkoa huo wa Asankragua, Alex Tweneboa-Kodna amesema "Tunawaelimisha wakulima kuhusu haki zao. Hawakujua hili linawezekana."

Mradi huo umewasaidia wakulima 150 kusajili umiliki wa miti ya mbao kwenye mashamba yao. Wakfu huo wa WFC umesema unelanga kusambaza mkakati huo kote nchini Ghana, taifa ambalo ni la pili kwa uzalishaji wa zao la kakao kwa wingi duniani, baada ya Ivory Coast.

Nana Archer, mshiriki katika mradi huo aliyepo Nkwantanum, ambako kunakaliwa na jamii masikini ambayo pia inazalisha kakao amesema "Tulifurahishwa sana tuliposikia kuhusu mradi huu".

Akiwa amesimama kwenye uwanja wake, ambao umezungukwa na kuku wanaookota chakula ardhini, mkulima mmoja mwenye miaka 53 alikuwa akionyesha cheti chake alichopewa na tume ya  misitu kilichoonyesha alipanda na kusajili miti 30 ya kivuli.

Kulingana na utafiti uliofanywa na shirika la kimataifa lisilo la kibiashara la nchini Marekani, la Winrock International umeonyesha kuwa mara nyingine wakulima waliiharibu kabisa miti hiyo ya kivuli ili wafanyabiashara wanaotafuta miti ya mbao wasifike kwenye mashamba yao. Lakini hali hii inaweza kubadilika, iwapo wakulima wataanza kusajili miti waliyoipanda.

Archer anasema kwamba iwapo wafanyabiashara hao watarejea, atawaonyesha cheti alichopewa na tume ya misitu ili kuwazuia kukata miti yake.

Ghana Kakao-Anbau- Alter mann der Gemeinde Abamkrom
Zao la kakao ni maarufu sana Afrika MagharibiPicha: picture-alliance/robertharding

KICHOCHEO CHA UKATAJI MITI.

Kilimo cha kakao kimekuwa kichocheo kikuu cha ukataji miti nchini Ghana, hii ikiwa ni kulingana na serikali. Wakati wakulima wanapokosa mazao ya kutosham kutokana na miti ya kakao kushindwa kuzalisha vizuri ama kuwa dhaifu, wakulima huanza kukata miti ili kutafuta maeneo mapya ya kilimo.

Kupanda kwa mara nyingine miti ya mbao kwenye mashamba ya kakao kunaweza kusaidia kurejesha upya misitu pamoja na kupunguza shinikizo la ukataji zaidi wa miti kwa kuongeza mavuno, hii ikiwa ni kulingana na utafiti wa Winrock.

Hadi sasa, wakulima wanaweza tu kusajili miti waliyoipanda, lakini wanaharakati wanaisisitizia serikali kutumia sheria hiyo pia kwenye miti ya asili, amesema Sander Muilerman wa WCF. 

Wakulima pia huhihitaji kupata uthibitisho kutoka kwa wamiliki wa ardhi ili kusajili miti yao, utaratibu ambao mara nyingine huwa ni mgumu kwao. 

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rhman