1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa makazi wazidi makali duniani

Iddi Ssessanga
9 Juni 2023

Shirika la makazi la Umoja wa Mataifa, UN-Habitat limesema idadi ya wakazi wa maeneo ya mabanda inatazamiwa kufika bilioni 3 kufikia 2050 huku mzozo wa makazi ukizidi kuwa mkali duniani.

https://p.dw.com/p/4SOdz
Kenia Nairobi Kibera Slum
Picha: Donwilson Odhiambo/SOPA Images/ZUMA Press Wire/picture alliance

Beatrice Oriyo alicheka kwa sauti kubwa alipoulizwa kama kulikuwa na uwanja wa michezo ambapo watoto wake watatu wangeweza kucheza karibu na nyumba yake huko Kibera, makazi yasiyo rasmi zaidi ya Nairobi.

"Hakuna kitu kama hicho hapa," Oriyo mwenye umri wa miaka 34 aliuambia Wakfu wa Thomson Reuters kwa njia ya simu kutokea nyumba ya mabati yenye chumba kimoja anayopanga kwa Shilingi 6,000 za Kenya, sawa na dola 43.18 kwa mwezi.

"Hatuna hata choo chetu - tunalazimika kulipa kila wakati tunapotumia vyoo vya umma. Tunaoga katika chumba sawa ambacho ndiy jiko letu, sebule na chumba cha kulala. Wazo la uwanja wa michezo hapa ni sawa na mzaha. " alisema.

Zaidi ya watu bilioni moja duniani wanaishi katika makazi duni yenye msongamano wa watu kaktika mitaa kama vile Kibera, ambako wanaishi maisha ya hatari, wakihangaika kupata huduma za msingi kama vile makazi ya kutosha, maji, usafi wa mazingira, nishati na ukusanyaji wa taka, lilisema shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya miji. , UN-Habitat.

Soma pia: Kenya: Mahakama yasimamisha bomoabomoa Kariobangi

Idadi hii inakadiriwa kufikia watu bilioni tatu ifikapo mwaka 2050 - kadiri idadi ya watu inavyoongezeka na watu wengi zaidi kuhamia mijini kutafuta fursa bora - hali inayowasilisha changamoto kubwa kwa serikali nyingi duniani kote.

Kenia Nairobi Kibera Slum
Muonekano wa juu wa mtaa wa Kibera, ambao ndiyo eneo kubwa zaidi la mabanda barani Afrika, na mmoj ya makubwa zaidi duniani.Picha: Simone Boccaccio/ZUMA Wire/IMAGO

UN-Habitat inakadiria kuwa asilimia 50 ya ukuaji huu wa watu wa makazi duni itajikita zaidi katika nchi nane: Nigeria, Ufilipino, Ethiopia, Tanzania, India, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Misri na Pakistan.

"Mustakabali wetu ni wa mijini," Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Habitat Maimunah Mohd Sharif aliwaambia waandishi wa habari kando ya Mkutano wa Baraza la UN-Habitat, uliofanyika kwa siku tano na kuwaleta pamoja mawaziri, maafisa wakuu na mashirika ya kiraia ili kuimarisha dhamira ya kujenga miji endelevu zaidi.

"Zaidi ya nusu ya watu duniani wanaishi katika majiji na miji. Idadi hiyo itaongezeka hadi asilimia 70 ifikapo mwaka 2050. Kwa hiyo, kukabiliana na umaskini wa mijini na ukosefu wa usawa ni jambo la dharura zaidi kuliko hapo awali," alisema.

Hakuna faragha, hakuna usalama

Zaidi ya nusu ya wakazi wa mijini nchini Kenya wanaishi katika makazi yasiyopangwa na yaliorundikana kama vile Kibera, inasema Benki ya Dunia. Mtaa huo wa vichochoro vyembamba vilivyowekwa lami ni makazi ya watu wasiopungua 250,000 - wengi wao wakiishi karibu pamoja katika vibanda vya chumba kimoja visivyo na madirisha.

Wakazi wengi ni wahamiaji kutoka maeneo ya mashambani na wanapata chini ya dola 2 kwa siku katika kazi za kipato cha chini kama madereva wa teksi za pikipiki, walinzi, wafanyakazi wa nyumbani au vibarua wa kawaida. Hawana uwezo wa kumudu makazi bora jijini Nairobi.

Megastädte in Afrika | Lagos in Nigeria
Muonekano wa juu wa mtaa mkubwa wa mabanda wa Makoko, kwenye kingo cha jiji la biashara la Nigeria, Lagos, ambao unakadiriwa kuwa na watu 250,000 wanaoishi katika umakini mkubwa.Picha: Sadak Souici/Le Pictorium Agency/ZUMA Press/picture alliance

Vyoo ni vile vya shimo vya pamoja ambavyo mara nyingi hufurika wakati wa msimu wa mvua, kuna maji kidogo ya bomba, hivyo wakazi wanategemea maji ya gharama kubwa yanayosamabazwa na magari ili kujaza ndoo na vyombo vyao kila siku.

Mifereji na ukusanyaji duni wa takataka vinamaanisha mafuriko ni jambo la kawaida - sio tu kwa kuharibu nyumba na mali, lakini pia kuchafua maji ya kunywa na hata kusababisha vifo kupitia kuporomoka kwa majengo, kupigwa na umeme na kuzama.

Soma pia: Corona: Wakaazi katika mitaa ya mabanda wahofu kuambukizwa

Kukiwa na viwango vya juu vya umaskini na ukosefu wa ajira kwa vijana, uhalifu kama vile unyanganyi, wizi na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake umeenea. Wakazi katika makazi yasiyo rasmi pia wako katika hatari ya kufukuzwa kwa nguvu na mamlaka, na matukio ya tingatinga kuja na kubomoa makazi ya watu ni ya kawaida.

"Si rahisi kuishi hapa," Mercy Achieng, mama asiye na mwenzi mwenye umri wa miaka 41, ambaye hupata shilingi 500 kila wiki kwa kufua nguo, alisema kwa njia ya simu kutoka Kibera, umbali wa dakika 30 tu kutoka uwanja wa ekari 140 uliopambwa vizuri wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa katika eneo la watu wa tabaka la juu la mji mkuu Nairobi.

"Ni jumuiya nzuri na sote tunajuana na kusaidiana, lakini hakuna faragha, hakuna usalama na hakuna ulinzi. Mwenye nyumba anaweza kutufukuza, au tingatinga zinaweza kuja."

Haiti Port-au Prince | Frau mit Kind im Slum Cite Soleil
Mwanamke akiwa amembeba mtoto wake mbele ya nyumba yake katika mtaa wa mabadanda wa Cite Soleil, katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince.Picha: Odelyn Joseph/AP/Dpa/picture alliance

Uboreshaji wa mitaa ya mabanda

Maafisa wa UN-Habitat walisema ingawa ukosefu wa nyumba hapo awali ulionekana kuwa tatizo linalozikabili nchi zinazoendelea, limekuwa janga la kimataifa huku nchi nyingi tajiri kama Marekani, Uingereza na Ujerumani zikikabiliwa na uhaba huo.

"Mgogoro wa makazi duniani upo katika maeneo yote ya dunia leo," alisema Edlam Yemeru, mkuu wa kitengo cha maarifa na ubunifu wa UN-Habitat. "Ingawa dalili zinatofautiana, karibu nchi zote zinapambana na uharaka wa kuhakikisha kuwa raia wao wanapata makazi ya kutosha."

Takwimu kutoka Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo zinaonyesha kuwa gharama za nyumba zimepanda kwa kasi zaidi kuliko mapato na mfumuko wa bei katika nchi nyingi wanachama katika miaka ya hivi karibuni.

Soma pia: Kina mama wajitolea kuimarisha usalama mitaani Kenya

Rais wa Kenya William Ruto, aliyeingia madarakani mwaka jana, amefanya makazi ya gharama nafuu kuwa kitovu cha ajenda ya maendeleo ya serikali yake na kutangaza mipango ya kujenga nyumba 250,000 kila mwaka kwa ajili ya watu wenye kipato cha chini, ikiwa ni pamoja na wale walio katika makazi yasiyo rasmi kama Kibera.

"Kwa kutambua kwamba zaidi ya nusu ya wakazi wa Kenya wataishi katika maeneo ya mijini ifikapo 2050, tumeliingiza suala la makazi kwa wote kama nguzo muhimu ya ajenda ya kitaifa ya mabadiliko ya kiuchumi kutoka chini kwenda juu," Ruto aliwaambia wajumbe katika Baraza UN-Habita siku ya Jumatatu.

Honduras Polizisten
Polisi wakindia doria katika mtaa wa mabanda wa Colonia Divanna, katika mji mkuu wa Honduras, Machi 17, 2023.Picha: Orlando Sierra/AFP

Alisema hii itajumuisha majengo rafiki kwa mazingira, maeneo ya kijani, matumizi ya nishati inayotoa gesi kidogo ya kaboni, ikiwemo usafiri unaotoa kaboni kidogo, pamoja na kilimo cha mijini na usimamizi wenye ufanisi wa taka.

Lakini ufadhili wa mpango wa nyumba za bei nafuu - ambao ungetoza ushuru wa asilimia 3 kwenye mishahara ya wafanyakazi huku waajiri wakichangia kiasi sawa - umekosolewa vikali na upinzani na kuzua maandamano ya vyama vya wafanyakazi.

Joseph Muturi, mwenyekiti wa Slum Dwellers International – mtandao wa watu maskini wa mijini kutoka zaidi ya nchi 18 – alisema serikali zinahitaji kuzingatia uboreshaji wa makazi duni, badala ya kuwahamishia wakaazi wa makazi duni kwenye miradi ya makazi nje ya miji.

Soma pia: Papa atembelea mtaa wa mabanda Kenya

Mifano ya awali ya uhamishaji wa familia kutoka makazi duni kwenda makazi mapya yenye huduma duni kwenye kingo za miji iliwaacha wakiwa wametengwa na wakiwa na nafasi chache za kazi na kuwalazimisha hatimaye kurejea kwenye maeneo ya mabanda, alisema.

"Huwezi kuwahamisha wakaazi wa vitongoji duni mbali na miji. Wana haki ya kushiriki kama raia wa miji hii kama kila mtu mwingine," Muturi alisema.

Wasichana wa mitaa ya mabanda na madhila yanayowakabili

"Unapohamisha watu, pia unaua mfumo wa kijamii ambao jumuiya hizi zimeusuka kwa miongo mingi - suluhu bora ni uboreshaji wa makazi duni ndani ya eneo hilo. Inabidi ushirikiane na wakazi wa makazi duni, kutoa umiliki wa uhakika na huduma wanazohitaji."

Chanzo: Wakfu wa Thomson Reuters