Wafungwa wengine 70 watoroka Kongo | Matukio ya Afrika | DW | 19.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Wafungwa wengine 70 watoroka Kongo

Zaidi ya wafungwa 70 wametoroka katika gereza lililoko Kusini Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Ijumaa(19.05.2017), ikiwa ni siku mbili baada ya wafungwa wengine kutoroka katika gereza la Makala

Mwanaharakati wa nchini humo ametoa taarifa hizo ikiwa ni siku mbili tu baada ya maelfu ya wafungwa kutoroka katika gereza la Makala lililopo kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Kinshasa.

Kutoroka kwa wafungwa kwa kiasi fulani ni kawaida nchini Jamhuri wa Kidemokrasi ya Kongo, lakini matukio mfululizo ya hivi karibuni ya kutoroka kwa idadi kubwa ya wafungwa wengi yanaonyesha wazi kuzorota kwa hali ya utulivu kunakosababishwa na hatua ya Rais Joseph Kabila kukataa kuondoka madarakani baada ya mamlaka yake kumalizika mnamo mwezi Disemba mwaka jana.

Hatua ya Kabila ya kusalia madarakani imechangia kuongezeka kwa maandamano yaliyosababisha vifo na ghasia za wanamgambo, hali inayozua wasiwasi kwa nchi hiyo kurejea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha muongo mwingine wa mauaji ya mamilioni ya raia.

Rais wa asasi za kiraia jimbo la Kati nchini humo ambaye pia ni mbunge, Valentin Vangi amesema kwamba wafungwa 73 kati ya 77 wa gereza lililopo kwenye mji wa Kasangulu walitoroka majira ya saa 8 za alfajiri. Vangi ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba waliparamia ukuta na wakati mlinzi wa gereza alipokwenda kuwarifu polisi na kuacha mlango wazi, wafungwa walitumia mwanya huo kutoroka.

Wafuasi wa madhehebu ya Bundu Dia Kongo, BDK walivamia gereza la makala siku ya Jumatano(17.05.2017), na kusaidia kutoroka kiongozi wao Ne Muanda Nsemi na wafuasi wengine wa madhehebu hayo. Serikali ilisema watu kadhaa waliuwawa wakati wa makabiliano wa wafungwa na polisi. 

Emmanuel Cole wa mfuko wa Bill Clinton kuhusu amani mjini kinshasa amesema zaidi ya wafungwa 4,600 wanaweza kuwa wametoroka, idadi hiyo ikiwa ni nusu ya wafungwa wote. Cole alitoa ripoti hiyo baada ya uchunguzi uliofanywa na wachunguzi wa mfuko huo kwenye gereza hilo.

Jean Claude Vuemba, mbunge kutoka Kasangulu ameiambia Reuters kwamba wafungwa 73 walitoroka, lakini 10 kati yao walikamatwa tena mapema mchana wa Ijumaa. Msemaji wa polisi hakupatikana mara moja kuzungumzia tukio hilo. 

Kiongozi wa BDK Nsemi alikamatwa mnamo mwezi Machi kwa madai ya kupanga mashambulizi kufuatia mwito kwa raia wa Kongo wa kumpinga rais Kabila. Aidha, kundi hilo linataka kurejeshwa kwa utawala wa ufalme wa Kongo uliokuwepo enzi ya ukoloni.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/DPAE.
Mhariri: Yusuf Saumu


 

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com