1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabukinabe wapiga kura kumchagua rais

29 Novemba 2015

Burkina Faso wanamchagua rais mpya na bunge leo Jumapili (29.11.2015) kwa matumaini ya kufungua ukurasa mpya katika mwaka ulioshuhudia machafuko ambapo umma wa taifa hilo la Afrika magharibi ulichukua hatua ya mapinduzi

https://p.dw.com/p/1HEAv
Burkina Faso, Wahlkampfplakat
Mabango ya uchaguzi wa rais na Bunge nchini Burkina FasoPicha: FP/Getty Images/I. Sanogo

Umma wa taifa hilo la Afrika magharibi ulichukua hatua ya kufanya mapinduzi na kumuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Blaise Compaore na kuzuwia mapinduzi ya kijeshi.

Usalama umeimarishwa wakati wapigakura wapatao milioni tano watakapokuwa wakipiga kura katika taifa hilo lenye wakaazi wapatao milioni 20 wakienda katika vituo vya kupigia kura kumchagua kiongozi mpya kwa mara ya kwanza katika muda wa karibu miongo mitatu.

Burkina Faso, Wahlkampfveranstaltung
Mkutano wa kampeni nchini Burkina FasoPicha: imago/Xinhua Afrika

Maafisa wameweka kati ya wanajeshi 20,000 na 25,000 kuzuwia kitisho cha shambulio la wapiganaji wa jihadi, kufuatia mashambulizi mawili dhidi ya kambi za jeshi la polisi katika mpaka wa magharibi wa nchi hiyo na Mali , nchi ambayo inakumbwa na ghasia.

"Kwa mara ya kwanza katika miaka 50 kuna hali isiyoeleweka ya uchaguzi ...hatufahamu mshindi kabla ya uchaguzi," amesema Abdoulaye Soma, mkuu wa chama cha wanasheria wa sheria ya katiba.

Hali imebadilika

"Hii ni hali nzuri na mabadiliko muhimu kutoka chaguzi nyingine ambazo tumezishuhudia hapo zamani."

Burkina Faso Präsidentschaftswahl Wahlwerbung
Matangazo kwa ajili ya uchaguzi wa rais nchini Burkina FasoPicha: DW/K. Gänsler

Rais wa zamani Blaise Compaore alilazimika kuikimbia nchi kufuatia maandamano ya umma mitaani mwezi Oktoba mwaka 2014 dhidi ya nia yake ya kubadilisha katiba kurefusha utawala wake uliodumu kwa miaka 27.

Serikali ya mpito iliwekwa hadi uchaguzi mpya utakapoweza kufanyika.

Lakini nchi hiyo ilitumbukia katika hali mpya ya sintofahamu mwezi Septemba mwaka huu, wiki kadhaa kabla ya uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika Oktoba 11, wakati viongozi wakuu wa kikosi cha jeshi ambao walikuwa karibu na Compaore walipojaribu kunyakua madaraka.

Kwa mara nyingine tena raia waliokuwa na hasira waliingia mitaani , na kuzuwia mapinduzi ya jeshi. Viongozi wao walikamatwa na kuwekwa kizuwizini na uchaguzi wa rais na bunge ulibadilishwa tarehe na kuwa Novemba 29.

Compaore , mwenye umri wa miaka 64, kijana mtanashati afisa wa zamani wa jeshi aliyefahamika kama "Beau Blaise", hivi sasa anaishi uhamishoni katika nchi jirani ya Cote d'Ivoire.´

Burkina Faso Spannungen Proteste gegen Präsidentengarde Armee
Maandamano ya umma yaliyoupndoa utawala wa rais Blaise Compaore mjini OuagadougouPicha: picture-alliance/dpa/A. Ouoba

Binafsi alinyakua madaraka mwaka 1987 wakati rafiki yake wa zamani mwanamapinduzi Thomas Sankara ... kiongozi mwenye heba barani Afrika ambaye aliingia madarakani na kufahamika kama "che Sankara"---alipopigwa risasi katika mapinduzi ambayo hivi sasa yanaaminika kwamba Compaore aliyaandaa.

Sankara aliweka msisitizo katika shule na afya na haki za wanawake katika nchi ambayo ni masikini hata kwa viwango vya Afrika.

Kuimarisha uhalali wa kiongozi ajaye wa taifa, wajumbe wa serikali ya mpito walipigwa marufuku kugombea kama wale ambao walikuwa wanaunga mkono juhudi za Compaore kuwania n muhula wa tatu, pamoja na wajumbe wa chama chake cha Congress for Democracy and Progress , CDP.

Chama kinachomuunga mkono Compaore cha CDP bado kimeweka wagombea wake katika uchaguzi wa bunge na kinatarajiwa kufanya vizuri katika maeneo ya nchi hiyo ambayo ni ngome inayomuunga mkono "Beua Blaise".

Burkina Faso Ouagadougou Übergangsregierung Präsident Michel Kafando
Rais wa serikali ya mpito Michel KafandoPicha: Reuters/J. Penney

Wagombea wanaomuunga mkono Compaore

Katika mbio za kuwania urais , wagombea saba kati ya 14 waliwahi kuwa karibu na Compaore, ikiwa ni pamoja na wawili ambao wanapewa nafasi ya kupata wadhifa huo--Roch Marc Christian Kabore na Zephirin Diabre.

Diabre mchumi , aliamua kuchukua kazi nje ya nchi hiyo lakini pia aliwahi kufanyakazi ndani ya nchi hiyo akiwa waziri wa uchumi na fedha. Katika wakati fulani alijiunga na mpango wa Umoja wa mataifa wa maendeleo akiungwa mkono na Compaore.

Thomas Sankara ARCHIV
Rais aliyepinduliwa na kuuwawa Thomas SankaraPicha: picture-alliance/dpa/AFP

Kabore alifanyakazi pamoja na Compaore kwa miaka 26-- akitumikia wadhifa wa waziri mkuu, spika wa bunge na mkuu wa chama cha CDP---kabla ya kutofautiana na Compaore na kisha kujitoa katika chama tawala miezi michache kabla ya kuporomoka kwa utawala wake.

Kabore tayari anajiona kama mshindi. "Itakuwa ushindi wa duru ya kwanza," ametabiri. "Umuhimu ni utawala bora pamoja na haki."

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Issac Gamba