Waandishi habari waliofariki ajalini waagwa Mwanza
12 Januari 2022Asubuhi kulipambazuka huku kukiwa kumetawaliwa na ukimya katika maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza kufuatia vifo hivyo vya waandishi wa habari walioagwa hii leo na mamia ya watu waliojitokeza katika uwanja wa mpira wa miguu wa Nyamagana wakiongozwa na waziri wa habari, mawasiliano na teknolojia ya habari Nape Nnauye.
Wanahabari hao ni sehemu ya watu 14 waliofariki dunia baada ya gari la waandishi wa habari iliyokuwa kwenye msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RC), Robert Gabriel kugongana na gari ya abiria aina ya Toyota Hiace katika eneo la Nyamikoma, Wilaya ya Busega katika Mkoa wa Simiyu.
Waandishi wa habari walipoteza maisha katika ajali hiyo ni Husna Mlanzi kutoka kituo cha televisheni cha ITV, Vanny Charles (Icon), Antony Chuwa, Johari Shani (Uhuru Digital) na Abel Ngapemba ambaye ni Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Waajiri wapewa siku saba kulipa stahiki za marehemu
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye na viongozi wengine wamewaongoza waombolezaji wakiwemo wanahabari, ndugu na jamaa wa familia waliofiwa kutoa heshima za mwisho kabla ya kila mwili kuzikwa katika eneo lake.
Waziri Nape ametumia jukwaa hilo kuagiza viongozi wa serikali kuweka mazingira bora yatakayowawezesha wanahabari kufanya kazi kwa usalama, huku akiwataka pia waajiri wanaodaiwa na waandishi wa habari waliofariki katika ajali ya gari wilayani Busega kulipa stahiki zao.
"Nimepewa salamu hapa kuwa miongoni mwa waliolala kwenye majeneza hapa mbele yangu hawajalipwa stahiki zao; natoa siku saba kwa waajiri wote wanaodaiwa kulipa stahiki zote za marehemu na kutoa taarifa ofisi ya mkuu wa mkoa," alisema Nape.
Awali, wawakilishi wa waandishi wa habari waliotoa salamu walimuomba waziri huyo kushughulikia changamoto ya waandishi kutolipwa stahiki zao huku wakifichua kuwa baadhi ya marehemu hawajalipwa kwa miaka miwili iliyopita.
Waliozungumza kwa niaba ya wanahabari ni Mwenyekiti wa Kluabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko na Mkurugenzi mtendaji wa Klubu ya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan.