Vyombo vya habari vyazuiwa kuzungumzia siasa Kameroon
26 Septemba 2013Wakati kampeni zinaanza kupamba moto , serikali ya Cameroon imesitisha vipindi 130 vya vyombo vya habari na mijadala ambayo inahusisha siasa katika vituo vya radio na televisheni nchini humo.
Waandishi habari wanasema kuwa hawawezi kukiuka amri hiyo kwa kuhofia vituo vyao kufungwa. Hii inakuja baada ya kufungwa na kusitishwa kufanyakazi kwa radio , Televisheni na magazeti 11.
George Etame mwenye umri wa miaka 45 anasafisha banda lake la kuku katika mji wa Sao nje kidogo ya mji wa Yaounde, mji mkuu wa Cameroon. Kwa muda wa siku 10 sasa, hajaweza kusikiliza kipindi chake akipendacho sana katika radio ambacho kinajadili masuala ya siasa katika lugha ya kwao ya Kiewondo.
"Kila mara nasikiliza vipindi vya radio vinavyohusu masuala ya siasa. Lakini kwa muda sasa , kila nikifungulia radio, nasikia muziki tu. Sijui kwanini".
Etame George anasema ana alikuwa akitegemea kipindi cha radio kumpa habari juu ya wanasiasa wanaoshiriki katika uchaguzi wa mabaraza ya miji pamoja na wabunge pamoja na sera zao.
"Nataka kupiga kura. Lakini sifahamu mtu wa kumpigia kura kwasababu hakuna mwanasiasa aliyefika hapa kutufahamisha kile atakachokifanya iwapo atachaguliwa".
Ufugaji wa kiwango kidogo wa kuku ni miongoni mwa Wacameroon wengi ambao wamekosa mipango ambayo inahusiana na masuala ya kisiasa kufuatia kusitishwa kwa vipindi kama hivyo katika redio zote za umma na za binafsi pamoja na vituo vya televisheni nchini humo.
Kituo cha taifa cha matangazo cha CRTV kimekuwa mara kadha kikiwakumbusha wananchi juu ya kusitishwa na kile kinachotarajiwa dhidi ya vyombo vya habari vitakavyopinga amri hiyo.
Waziri wa mawasiliano amesitisha utengenezaji wa vipindi vyote vya kisiasa wakati nchi hiyo ikijitayarisha na uchaguzi wa mabaraza ya miji na wabunge katika uchaguzi wa Septemba 30.
Mkaguzi mkuu katika wizara ya mawasiliano nchini Cameroon , Dr. Felix Zogo amesema kuwa vipindi hivyo vimezuiwa katika juhudi ya kulinda vyama vya siasa ambavyo havina uwezo wa kupata nafasi katika vyombo vya habari kuweza kufunikwa katika kampeni na vyama vyenye uwezo wa kupata nafasi katika vyombo vya habari vinavyoendeshwa na vyama hivyo.
"Tuna vyama 43 vya siasa vinavyopambana kwa hiyo mwandishi habari anakuwa na wapinzani 20 mahali fulani ama studio kuzungumza nao. Ni vigumu na ndio sababu ilikuwa bora kusitisha vipindi vyote ambavyo vinashughulika na masuala ya siasa ili kuhakikisha usawa".
Kumekuwa na maelezo tofauti kutoka kwa wanahabari nchini Cameroon. Serge Pouth , mwandishi habari wa shirika la utangazaji la taifa ambaye anatangaza vipindi vya siasa ana mawazo kuwa waandishi habari wanapaswa kufanyakazi kitaalamu zaidi katika kazi yao ili kuepuka hali kama hizo.
Mwandishi: Moki Kindzeka / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Josephat Charo