1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Volkano huundwa vipi?

18 Januari 2022

Kwa kawaida volkano tunazoziona ndizo tunazozizingatia, lakini mlipuko mkali wa volkano chini ya maji uliotokea katika kisiwa cha Pasifiki nchini Tonga umesababisha watu kuangazia volkano zinazolipuka chini ya bahari.

https://p.dw.com/p/45hso
Tonga | Vulkanausbruch Unterwasservulkan
Picha: New Zealand High Commission/ZUMA Wire/imago images

Christoph Helo, mtaalamu wa volkano katika Chuo Kikuu cha Mainz nchini Ujerumani anasema theluthi mbili ya shughuli zote za volkeno hutokea kwenye kina kirefu cha bahari. Helo ameiambia DW kwamba Volkano nyingi katika sayari ya dunia ni volkano za chini ya maji na hilo sio jambo la ajabu. Helo ameongeza kuwa volkano za aina hiyo hulipuka kwa ukimya kwa hivyo hakuna anayefahamu mlipuko umetokea.

Mlipuko huo wa chini ya maji nchini Tonga ulisababisha mvua kubwa iliyosababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo ya mji mkuu lakini kwa ujumla, milipuko ya chini ya maji huja na kuondoka bila kelele nyingi. Tamsin Mather, mtaalamu wa volkano na profesa wa sayansi ya ardhi katika Chuo Kikuu cha Oxford anasema idadi kamili ya volkano hai chini ya maji haijulikani, lakini makadirio huanzia mamia hadi maelfu .

Je, volkano za chini ya maji zinaundwaje?

Helo ameiambia DW kwamba hakuna tofauti maalum katika muundo wa volkano za chini ya maji na zilizoko juu ya ardhi. Volkeno hutokea wakati mawe yaliyoyeyuka hutoka katika safu ya pili ya ndani ya dunia, hii ikiwa sehemu imara zaidi ya juu na kujitokeza kupitia gamba la dunia. Mather amesema volkano za majini zinahusishwa na shughuli endelevu za volkano kwenye miinuko ya kati ya bahari, ambapo vipande viwili vya gamba la dunia huvutana. Mather ameongeza kuwa mgongano wa vipande hivyo viwili kunaweza pia kusababisha volkano.

Helo amesema iwapo vipande vyote viwili viko chini ya bahari, volkano zitajitokeza chini ya maji na kuongeza kuwa baada ya muda zina uwezekano wa kukua na kutengeneza visiwa vya volkano. Shughuli za volkano katika kipande kimoja cha gamba pia zinaweza kusababisha kutokea kwa Volkano. Hili linaweza kutokea wakati kuna eneo la moto chini ya bahari na kusababisha visiwa vya volkano kama Hawaii.

Nini hutokea wakati volkano ya chini ya maji inapolipuka?

Tonga | Satellitenbild Vulkanausbruch
Mlipuko wa volkano ya chini ya maji nchini TongaPicha: CIRA/NOAA/REUTERS

Athari za mlipuko wa volcano chini ya maji hutegemea ukaribu wake na eneo la maji. David Pyle, mtaalam wa volkano na profesa wa sayansi ya ardhi katika Chuo Kikuu cha Oxford amesema iwapo mlipuko unatokea katika kina kirefu cha chini ya maji, basi uzito wa maji yaliyoinuka hutumika kama kizuizi cha shinikizo. Iwapo kipande cha mwamba ulioyeyuka kitaingia katika bahari kilomita mbili chini ya eneo la bahari, kitakutana na maji baridi ya bahari na kupoa kwa haraka. Maji hayo yatashika moto sana lakini hayategeuka kuwa mvuke.

Lakini kina cha maji kinapokuwa kifupi, mwamba ulioyeyuka unaanza kupasha maji moto ambapo baadaye hugeuka kuwa unyevu. Hii husababisha mabadiliko makubwa katika ukubwa. Pyle ameiambia DW kwamba milipuko ya mvuke husababisha uharibifu mkubwa kwasababu kiwango kidogo cha maji hugeuka kuwa mvuke mkubwa. Mbali na athari ya mvua kubwa, kiwango cha majivu yanayorushwa hewani wakati volkano ya chini ya maji inapolipuka katika maji ya kina kifupi, huenda kikasababisha athari mbaya kwa afya ya binadamu. Pyle ameongeza kwamba majivu hayo na gesi inayotolewa, sio tu kwamba vinachafua hewa lakini vinaweza kuathiri upatikanaji wa umeme na maji.

Ukosefu wa ufikiaji, ukosefu wa data

Labda ukweli kwamba kwasababu volkano za nyambizi ziko chini ya maji, inafanya utafiti wake kuwa mgumu, haishangazi.

Mather ameiambia DW kwamba ni sehemu chache tu zenye shughuli zilizoweza kufanyiwa utafiti wa kina kutokana na ugumu wa kuzifikia. Wanasayansi wanaofanya kazi kwenye ardhi wanaweza kujifunza kuhusu historia ya volcano kwa kutembelea tovuti ya volcano na kukusanya data. Hii inaweza kufanyika kwa kutumia mipangilio ya miamba ama kuchimba mashimo na kukusanya vifaa. Kwa volkeno za chini ya maji, wanasayansi kwa kawaida hutegemea uchunguzi wa baharini na teknolojia ya ramani kama sonar.