1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vital Kamerhe aachiliwa huru

24 Juni 2022

Chama cha UNC cha Vital Kamerhe, aliyekuwa mkuu wa ofisi ya Rais Félix Tshisekedi, kimeridhika na kupongeza uwepo wa utawala wa sheria katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4DBSe
Kongo Oppositionsführer Vital Kamerhe
Picha: Imago/Belga/T. Roge

Baada ya kukutwa na hatia ya ubadhirifu wa fedha za umma, Kamerhe alihukumiwa kwanza kifungo cha miaka 20 jela, adhabu hiyo ikapunguzwa kutoka na rufaa hadi miaka 13 kabla ya kufutwa kabisa na Mahakama Kuu na kurudishwa kwenya Mahakama ya Rufaa ambako ameachiliwa huru. Lakini upinzani sasa umeomba Rais Tshisekedi afunguliwe mashtaka kutokana na ubadhirifu huo. 

Furaha ni kubwa sana kwenye ofisi za UNC ambapo viongozi na wanachama wote kwa ujumla walikuwa hawajakubaliana na hukumu ya kiongozi wao, tangu mwanzo wa kesi hiyo  waliendelea kusisitiza kuwa Vital Kamerhe hakuwa na hatia yoyote wakiamini kuwa amekumbwa na kesi ya kisiasa.

Lakini leo wanachokiamini ni kwamba mahakama ya Kongo hatimaye imeamua kufuata sheria. Jambo la furaha sana alilolieleza mbunge Juvenal Munubo ambae ni moja wa viongozi wa UNC, akisifu sasa kuwepo utawala wa sheria hapa nchini Kongo.

"Tuna furaha kubwa sana kwa kuachiliwa kiongozi Vital Kamerhe. Ni mtu ambaye alishtakiwa kwa mashtaka makubwa, alikuwa jela, ameachiliwa. Inaonekana kama ni mtu ambaye ataweza tena kuleta mchango wake kwa ujenzi wa nchi. Tuko kweli katika nchi ya sheria, siyo ndoto hapana. Tuko ndani kabisa ya demokrasia na hapo tunashukuru sana Rais Tshisekedi kwani ni yeye ameongoza nchi wakati ambao mabadiliko yameonekana ndani ya sekta ya sheria." Juvenal Munubo

Upinzani unasemaje?

DR Kongo Treffen Bintou Keita und Félix Tshisekedi
Rais Félix TshisekediPicha: Giscard Kusema/Kommunikationsdienst DR Kongo

Jambo ambalo upinzani bado haujalielewa kwani ukweli ni kwamba Wakongomani hawajaona matokeo ya kazi zilizofanywa kupitia mamilioni ya fedha hizo. Robert Maungano Kihyoka ambae ni mmoja wa viongozi wa muungano wa upinzani wa Lamuka mashariki mwa Kongo ameelezea DW kwamba ni lazma kesi mpya kufunguliwa ili Rais Félix Tshisekedi pia asikilizwe.

"Ndugu Vital Kamerhe amemtaja ndugu Félix. Ni kusema Félix naye anahusika ndani ya uwizi huu ambao Vital Kamerhe alikuwa akishtakiwa. Kwa hiyo, tunawaomba sasa majaji wamuite Félix naye aje kutueleza fedha hizi zimeenda wapi na namna gani alishirikishwa ndani ya wizi huo wa fedha za wakongomani." Robert Maungano Kihyoka.

Baada ya kesi iliyosomwa kuwa ya siku mia moja, mahakama ya Kongo iliamua kuwa Vital Kamerhe amefanya ubadhiri wa zaidi ya dola milioni 57 za Kimarekani zilizokusudiwa kununua nyumba. Mshtakiwa mwenzake Sammih Jamal, mfanyabiashara raia wa Lebanon pia ameachiliwa huru.

Baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa kuachiliwa kwake Kamerhe kuna maslahi ya kisiasa. Lakini Willy Wenga, mtaalam wa masuala wa kisheria amesema kuwa hata kama kesi ikiwa na maslahi ya kisiasa, hatimaye ukweli utatambuliwa.

 

Jean Noel Ba-Mweze, DW, Kinshasa.