Virusi vya Corona: Mripuko ulioanzia China na kuenea duniani
Chini ya mwezi mmoja, kirusi cha Corona kiliripuka kuwa janga kubwa la afya na kuwaua watu karibu 500 na kuwaathiri karibu wengine 6,000. Wanasayansi wanahangaika kutafuta chanjo ya kukabiliana nacho.
Virusi vya ajabu vyaibuka Wuhan
Disemba 31, 2019 China ililiarifu shirika la afya duniani WHO juu ya visa vya maambukizi ya virusi kwenye mji wa Wuhan ulio na wakaazi milioni 11. Mzizi wa kirusi haukujulikana na wataalamu wa maradhi duniani kote wakaanza kufanya kazi ili kukibaini. Chanzo kikabainika kuwa ni soko la vyakula vya baharini katika mji huo, na kufungwa kwa haraka. Watu 40 wakaripotiwa kuambukizwa.
Kirusi kikabainika kuwa ni Corona
Watafiti mwanzoni walisema ni kirusi cha SARS, ugonjwa hatari wa njia ya upumuaji uliozuka China mwaka 2002 na kuwaua karibu watu 800. Mnamo Januari 7, wanasayansi wa China walitangaza kubaini kirusi kipya. Kikirandana na kirusi cha SARS na dalili sawa za mafua, ni kirusi cha jamii ya Corona. Mwanzoni kikapewa jina la 2019-nCoV. Dalili zake ni pamoja na homa, kukohoa, ugumu wa kupumua na Nimonia.
Kifo cha kwanza China
Januari 11, China ikatangaza kifo cha kwanza kilichotokana na virusi vya Corona, alikuwa ni mzee wa miaka 61, ambaye alifanya manunuzi kwenye soko la Wuhan, alifariki kutokana na matatizo ya Nimonia.
Virusi vyaripotiwa nchi jirani
Siku zilizofuatia, nchi kama Thailand na Japan nazo zikaripoti visa vya maambukizi ya watu waliotembelea soko la Wuhan. Nchini China, kifo cha pili kikathibitishwa kwenye mji huo. Hadi kufikia Januari 20, watu watatu tayari walikuwa wamepoteza maisha nchini humo na wengine zaidi ya 200 kuambukizwa.
Maambukizi yake bado hayajulikani
Katikati ya Januari wanasayansi waliumiza vichwa kubaini jinsi gani corona inasambaa. Viikabainika kuwa vinaambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu. Lakini baadhi yake vinasambaa kupitia kikohozi na chafya. Viwanja kadhaa vya ndege duniani kote vilianza kuwachunguza abiria wanaowasili kutokea China. Januari 20 maafisa walithibitisha corona inaambukizwa moja kwa moja kupitia binadamu.
Mamilioni wakwama
Januari 23 China iliuweka mji wa Wuhan katika karantini ikiwa ni juhudi za kuzuia maambukizi zaidi. Usafirishaji ukasitishwa na wafanyakazi wakaanza ujenzi wa hospitali mpya ya kuwahudumia wagonjwa walioambukizwa, ambao tayari walifikia zaidi ya 800 hadi kufikia Januari 24 huku idadi ya vifo ikipanda hadi 26. Maafisa wakalazimika kuifunga miji mingine 13 na kuathiri angalau watu milioni 36.
Janga la kiafya la ulimwengu?
Visa zaidi na zaidi vikaripotiwa nje ya China ikiwemo Korea Kusini, Marekani, Nepal, Thailand, Hong Kong, Singapore, Malaysia na Taiwan. Wakati idadi ya maambukizi ikiongezeka, shirika la afya duniani WHO mnamo Januari 23 likasema "ni mapema" kuutangaza ugonjwa huo kuwa dharura ya ulimwengu.
Virusi vya Corona vyaingia Ulaya
Januari 24 maafisa wa Ufaransa wakathibitisha visa vitatu vipya vya virusi vya Corona ndani ya mipaka yake, na kuufanya ugonjwa huo kuingia mara ya kwanza barani Ulaya. Saa chache baadae Australia nayo ilithibitisha kuwa watu wanne wameambukizwa virusi vya corona.
Sherehe za mwaka mpya wa Luna zaongezwa siku.
Sherehe za mwaka mpya wa Kichina yani ´Lunar New Year´ zilianza Januari 25. Maafisa wakasitisha matukio muhimu katika jitihada za kuzuia maambukizi, wakati mamilioni ya Wachina wakisafiri katika sherehe za umma. Hadi kufikia mwishoni mwa Januari, miji 17 ya China iliyo na wakaazi zaidi ya milioni 50 ilikuwa imefungwa. Sherehe hizo zikarefushwa kwa siku tatu ili kudhibiti umati wa watu.
Mipaka na Mongolia, Hong Kong, na Urusi yafungwa
Cambodia ikatangaza kisa cha kwanza cha Corona, wakati Mongolia ikiuufunga mpaka wake na China na Urusi nayo ikaifunga mipaka yake kwenye mikoa mitatu iliyoko mashariki ya mbali. Idadi ya vifo ikaongezeka hadi kufikia 41 huku watu 1,300 wameambukizwa duniani kote hususan China. Wanasayansi wana matumaini ya kupata chanjo ya Corona ndani ya miezi mitatu.
Ujerumani yajiandaa kukabiliana na corona
Januari 27 waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas akatangaza kwamba wanawaondoa Wajerumani walioko Wuhan. Hapakuwa na ripoti za visa vya Corona Ujerumani lakini maafisa walijitayarisha kukabiliana navyo. Watafiti wa Kijerumani mjini Marburg walikuwa ni sehemu ya juhudi za kimataifa kutafuta chanjo ya Corona. Idadi ya waliofariki imefikia 81, huku 2,700 wakiwa wameambukizwa duniani kote.
Kisa cha kwanza chadhibitishwa Ujerumani
Januari 27 Ujerumani ikatangaza kisa cha kwanza cha Corona cha mtu wa miaka 33 mjini Bavaria aliyeambukizwa na mfanyakazi wa Kichina wakati wa mafunzo. Akawekwa kwenye karantini na uchunguzi kuendelea katika hospitali ya Munich. Siku iliyofuata, wafanyakazi wenzake watatu wakathibitishwa kuambukizwa. Idadi ya vifo China imefikia 132, walioambukizwa duniani kote wamefikia 6,000.
Nchi zaanza kuwaondoa raia wake Wuhan
Januari 28, Japan na Marekani zilikuwa nchi za kwanza kuanza kuwaondoa raia wake kutoka mjini Wuhan. Abiria wanne wa Japan wakapelekwa hospitali mara baada ya kuwasili. Australia na New Zealand nazo zikasema zitatuma ndege kwa ajili ya kuwaondoa raia wake. Visa vya maambukizi vikazidi kuongezeka zaidi ya virusi vya SARS vilivyoibuka mwaka 2002 na kuwaua watu zaidi ya watu 800.
WHO yaitangaza Corona kuwa dharura ya ulimwengu
Januari 30, shirika la afya duniani WHO, ikavitangaza virusi vya Corona kuwa janga la dharura la ulimwengu katika juhudi za kuyalinda mataifa yaliyo na mfumo dhaifu wa afya. Hata hivyo, mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus hakutangaza vizuzi vya biashara na kusafiri, akisema hiyo itakuwa ni "usumbufu usio wa lazima".
Raia waliondolewa Wuhan wawasili Ujerumani
Februari mosi, jumla ya watu 123 wakiwemo wajerumani 102 waliwasili uwanja wa ndege wa Frankfurt baada ya kuondolewa kutoka mjini Wuhan, kitovu cha maradhi hayo. Walipelekwa moja kwa moja hadi kwenye kambi ya jeshi ya Ujerumani ya Germersheim ambako waliwekwa karantini kwa siku 14. Watu wawili kati yao waliripotiwa kuambukizwa virusi hivyo.
Kifo cha kwanza nje ya China
Kifo cha kwanza kinachohusishwa na Corona nje ya China kiliripotiwa Ufilipino mnamo Februari 2. Mwanaume mwenye miaka 44 raia wa China alisafiri kutokea Wuhan hadi Manila kabla ya kuugua na kupelekwa hospitali, ambako alifariki baadae na nimonia.
Hospitali mpya ya Corona yajengwa ndani ya siku 10
Hospitali ya Huoshenshan mjini Wuhan iliyojengwa ndani ya wiki moja ilifunguliwa Februari 3. Hospitali hiyo ililenga kutumia mchanganyiko wa tiba za magharibi na tiba asili za China kuwatibu wale walioambukizwa virusi vya corona.