Viongozi wa Ulaya hawana wasi wasi na kura ya Cyprus
20 Machi 2013Kundi la mataifa yanayotumia sarafu ya euro limeelezea kwa tahadhari matokeo ya kura bungeni nchini Cyprus. Wakati huo huo lakini viongozi wa juu wa umoja wa Ulaya wanazungumzia zaidi kuhusu yaliyotokea nchini Cyprus.
Mkutano wa dharura katika ikulu ya rais nchini Cyprus pia unahudhuriwa na gavana wa benki kuu Panicos Demetriades na wajumbe wa kundi la pande tatu la wafadhili , Umoja wa Ulaya , benki kuu ya Ulaya na shirika la fedha la kimataifa IMF.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameeleza nia yao ya kuendelea kuisaidia Cyprus licha ya bunge la nchi hiyo kukataa masharti ya umoja huo. Waziri wa fedha wa Uholanzi Jeroen Dijsselbloem amesema ameyakubali matokeo ya bunge la Cyprus.
"Ni kweli kwamba inakatisha tamaa. Nasikitika kuwa Cyprus imefikia uamuzi huu. Lakini mpira bado uko upande wao , pendekezo la mpango wa uokozi la mataifa ya euro linaendelea".
Waziri wa Ujerumani aonya
Waziri wa fedha wa Ujerumani lakini ameonya kuwa , Wacyprus wasitarajie kupata matumaini ambayo hayawezekani.
"Matumaini ya Wacyprus hayawezi kuendelea kama yalivyo na kujaribu kuvutia mitaji, ambayo haijawekezwa na inagharamiwa na watu wengine, kwa kuwa utaratibu huo hauwezi kufanyakazi, hii ni hali ya kufikirika tu. Na viongozi nchini Cyprus ni lazima wafafanue kwa watu wao".
Cyprus yatoza kodi fedha za wateja
Chini ya masharti ya kupatiwa mpango huo wa uokozi uliofikiwa mwishoni mwa juma, kundi la pande tatu lilitarajiwa kuipatia Cyprus kiasi cha euro bilioni 10 kwa masharti kuwa nchi hiyo itafute yenyewe kiasi cha euro bilioni 5.8.
Nchi hiyo iliweka kodi ya asilimia 9.9 kwa fedha za wateja zilizoko katika benki nchini humo, na hatua hiyo ilizusha hasira miongoni mwa watu walioweka fedha zao na kuleta hofu kuwa mataifa mengine ya umoja wa Ulaya yenye matatizo ya kifedha kama Italia, na Uhispania huenda yakafuata mkondo huo.
Serikali ya Cyprus ilibadilisha msimamo, na jana Jumanne iliachana na pendekezo la kutoza kodi hiyo kwa fedha chini ya euro 20,000 , wakati ikiendelea na mpango wake wa kutoza asilimia 6.75 kwa fedha zilizowekwa kuanzia euro 20,000 hadi 100,000 na asilimia 9.9 kwa fedha zinazovuka kiwango hicho.
Lakini hatua hiyo pia ililalamikiwa na spika wa bunge la nchi hiyo na kusema ni kama uporaji.
Mwandishi : Andreas Reuter / ZR / Kitojo Sekione
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman