Viongozi wa dunia kumaliza umasikini ndani ya miaka 15 | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa dunia kumaliza umasikini ndani ya miaka 15

Viongozi wa dunia Ijumaa (25.09.2015)wameahidi kumaliza umasikini mkubwa ndani ya miaka 15, wakiidhinisha malengo ya Umoja wa Mataifa yenye matumaini na kusaidiwa na dola trilioni kadhaa katika matumizi ya maendeleo.

UN Vollversammlung UN Hauptquartier New York

Baraza kuu la Umoja wa mataifa

Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis amekaribisha ajenda ya malengo hayo mapya akisema kuwa "ni ishara muhimu ya matumaini" katika hotuba yake katika hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa na amewataka viongozi kutimiza ahadi zao za kuibadilisha dunia ifikapo mwaka 2030.

Akitoa hotuba yake ya kwanza katika Umoja wa mataifa , kiongozi huyo wa kidini ametoa tahadhari, akisema ahadi hazina maana bila ya nia ya utekelezaji.

Papst Franziskus UN Vollversammlung in New York

Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis

"Ahadi tupu, hata hivyo, hazitoshi, hata kama ni hatua muhimu kuelekea katika suluhisho," Papa amesema wakati akiwataka viongozi kuchukua "hatua muhimu na hatua za haraka" kulinda mazingira na kufikisha mwisho hali ya kuwatenga wengine.

Maendeleo endelevu

Ukionekana kuwa ni mpango kamambe wa kupambana na umasikini kuwahi kutolewa, malengo 17 ya maendeleo endelevu (SDGs) na shabaha 169, yaliidhinishwa mwanzoni mwa mkutano wa kilele ambao umefikisha mwisho miaka mitatu ya majadiliano magumu.

Malengo hayo yatachukua nafasi ya malengo ya maendeleo ya milenia (MDGs)ambayo muda wake unamalizika mwaka huu na yatatumika kwa nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea.

Ajenda mpya ya Umoja wa Mataifa ina lenga kumaliza umasikini, kuhakikisha maisha ya afya, kuhimiza elimu na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, kwa gharama kati ya dola trilioni 3.5 na 5 kwa mwaka hadi ifikapo mwaka 2030.

UN Vollversammlung 24.09.2014 - Ban Ki-moon

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon ameueleza mpango huo kuwa ni "orodha ya vitendo kwa watu na sayari yetu" ambao unatoa mwelekeo wa ,"kilimwengu, wa ujumuisho na unaoweza kuleta mabadiliko kwa ajili ya maisha bora duniani."

"Mtihani muhimu kwa nia thabiti kwa ajili ya ajenda 2030 itakuwa ni utekelezaji," Ban amewaambia viongozi. "Tunahitaji utekelezaji kutoka kwa kila mtu, kila mahali."

Malala awalilia viongozi kuhimiza elimu

Mshindi wa nishani ya amani ya Nobel msichana Malala Yousafzai amewataka viongozi kuangalia zaidi uhamasishaji wa elimu, ambao ameueleza kuwa "uwekezaji wa kweli ambao dunia inauhitaji na viongozi wa dunia wanalazimika kufanya."

Malala Yousafzai

Mshindi wa nishani ya amani ya Nobel Malala Yousafzai

Akipumzisha kidogo matatizo ya mzozo wa wakimbizi barani Ulaya, kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameyasifu malengo hayo mapya lakini akasisitiza kwamba amani ni "mahitaji muhimu "ili yapatikane maendeleo.

Mamilioni ya wakimbizi na wahamiaji wanakimbia "ugaidi na ghasia", Merkel amesema, kabla ya kuongeza kwamba,"Tunapaswa kupambana na sababu za watu hawa kukimbia."

Mara baada ya mkutano wao wa kilele wa siku tatu, viongozi wa dunia wanaanza mjadala katika baraza kuu la Umoja wa mataifa siku ya Jumatatu, ambapo vita nchini Syria na mzozo wa wahamiaji barani Ulaya vinatarajiwa kuchukua nafasi ya juu.

Merkel vor der UN-Vollversammlung

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Mtazamo mkubwa umeelekezwa katika kumaliza umasikini uliokithiri unaowakabili watu wanaokadiriwa kufikia milioni 836 ambao bado wanahangaika kuweza kuishi, wengi wao wakiwa katika mataifa ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara na barani Asia.

Bilioni kadhaa za dola za misaada ya maendeleo zitaelekezwa kutimiza malengo hayo, lakini Umoja wa Mataifa pia unataka kutumia vyanzo vya fedha katika nchi hizo kupitia ukusanyaji mzuri wa mapato.

Buhari aahidi kupambana na ufisadi

Katika hotuba yake ya kwanza katika Umoja wa mataifa, rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ameahidi "kuziba mianya yote" inayoruhusu ufisadi wa kuhamisha fedha kwa wizi na "kuzuwia wizi wa mafuta" ambao unadhoofisha uchumi wa taifa hilo lenye uchumi mkubwa barani Afrika.

Malengo ya dunia yanatoa wito wa kuimarishwa uwazi katika nchi zinazotoa mafuta na kuzuwia rushwa na kuhakikisha kwamba fedha zinazotokana na maliasili zinatumika kufanya maisha kuwa bora kwa raia wa nchi hizo.

New York Rede Narendra Modi UN-Vollversammlung 27.09.2014

Waziri mkuu wa India Narendra Modi

Waziri mkuu wa India Narendra Modi , ambaye serikali yake bado haijatangaza mpango wake wa mabadiliko ya tabia nchi, ametangaza kwamba kuwasaidia watu masikini katika nchi yake kutakuwa na "matokeo makubwa kwa ajili ya maendeleo endelevu kwa sayari yetu nzuri."

Si rahisi hata hivyo kwamba nchi zote zitafanikisha malengo hayo, lakini makundi ya kutoa misaada yanasema mpango huo utatoa vipimo kwa serikali katika kila eneo la maendeleo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Amina Abubakar

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com