Viongozi wa dini Tanzania wawaonya wanasiasa | Tanzania Yaamua 2015 | DW | 10.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Tanzania Yaamua 2015

Viongozi wa dini Tanzania wawaonya wanasiasa

Ukiwa umebaki mwezi mmoja na kidogo kabla ya uchaguzi mkuu nchini Tanzania, viongozi wa dini wamekutana jijini Arusha kujadili namna ya kulinda umoja wa kitaifa wa taifa hilo la Afrika Mashariki.

Mmoja wa viongozi wa Shuraa ya Maimamu nchini Tanzania.

Mmoja wa viongozi wa Shuraa ya Maimamu nchini Tanzania.

Viongozi hao kwa pamoja wamesema ni wazi kuwa kuna viashiria vya wazi kutoka kwa wanasiasa ambavyo vina lengo la kuwagawa Watanzania kwa misingi ya kidini na kisiasa, jambo ambalo linapaswa kuachwa mara moja ili kuendelea kudumisha upendo, amani na udugu miongoni mwa raia.

Askofu Thomas, Mkurugenzi wa Kamati ya Mahusiano, Upendo na Amani miongoni mwa madhehebu ya dini mbalimbali nchini Tanzania, alisema kuwa Watanzania wamekuwa na umoja kwa miaka mingi kutokana na waasisi wa taifa hilo kuijenga nchi "kwa misingi isiyogemea dini wala imani yoyote na kupelekea kuonekana kimbilio kwa nchi jirani zinazokabiliwa na machafuko", akiongeza kuwa ni jambo linalopaswa kulindwa.

Kwa upande wake, Sheikh Shabani Juma Abdallah, ambaye ni Sheikh wa Mkoa wa Arusha, alisema ni vyema wanasiasa wakatafakari kwa kina kauli zao wanazotoa mbele ya umma ili kuepusha madhara yoyote yanayoweza kusababishwa na kauli hizo.

"Dini ya Kiislamu inahimiza upendo, amani na uvumilivu. Waislamu watekeleze maagizo haya ya Mwenyenzi Mungu na waepuke kutumiwa na watu wenye nia mbaya ya kuwagawa," aliongeza Sheikh Abdallah.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano, Amani na Upendo katika Mkoa wa Arusha, Mchungaji Andew Kajembe Hotai, aliwalaumu viongozi wa kisiasa kwa kauli zao ambazo ambazo alisema "zinakinzana na maadili na sheria za nchi na zinaweza kuleta jazba na hatimaye kuleta vurugu na kuliingiza taifa mgogoro usiokuwa na maslahi kwa Watanzania."

Mkutano pia ulihudhuriwa na wawakilishi wa vyama kisiasa, vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa dini za kijadi ambao kwa pamoja walizungumzia mustakabali wa Tanzania katika kipindi hiki cha uchaguzi na siku zijazo.

Mwandishi: Charles Ngereza/DW Arusha
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com