Vilabu vya Ulaya vyaimarisha usalama | Michezo | DW | 20.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Vilabu vya Ulaya vyaimarisha usalama

Hisia za kuchanganyikiwa na hofu, badala ya msisimko na furaha, huenda zikawakumba mashabiki wakati ligi kuu za kandanda Ulaya zitakaporejea tena wikendi hii baada ya kutokea mashambulizi ya kigaidi mjini Paris

Real Madrid dhidi ya Barcelona kawaida unatambulika kuwa mchuano wa kufurahisha zaidi ulimwengu kutokana na vipaji vya washambuliaji bora zaidi, wakati mjini Turin, Juventus na AC Milan huwa mpambano unaozungumziwa sana kati ya vilabu hivyo vya Italia vyenye historia kubwa.

Lakini badala yake, michuano hii itadhihirisha hofu inayoizunguka michuano ya wikendi hii, huku usalama katika viwanja ukiwa mkubwa kabisa katika mazingira ambayo kawaida huwa tulivu.

Maafisa nchini Uhispania wameutaja mchuano wa leo wa EClassico kati ya Real Madrid na Barcelona kuwa na kitisho cha kikubwa lakini usalama utaimarishwa uwanjani Santiago Bernabeu. Ngome hiyo huwakaribisha mashabiki 81,000.

Andres Iniesta, kiungo wa Barca anasema licha ya yote, watajitahidi kuufurahisha ulimwengu uwanjani "Nadhani hali hiyo inaharibu kabisa amani kote ulimwenguni, haiepukiki. Nadhani tunakubaliana kuhusu hilo na kila kitu ni wazi. Lakini ninachojua, na vikosi vya usalama vinatwambia kutakuwa na usalama mkubwa, kila hatua zimewekwa na kila mmoja anapaswa kuchangia hili. Lakini mchuano, kama unavyokuwa, ni kivutio, na kandanda, mchezo wenyewe, unaweza kuangaziwa katika siku nzuri kabisa ya ulimwengu wa kandanda".

Hapa Ujerumani, michuano ya Bundesliga inaendelea kama kawaida licha ya kitisho kilichokuwepo cha mashambulizi wakati wa mchuano wa kirafiki kati ya Ujerumani na Uholanzi mjini Hannover Jumanne usiku.

Msemaji wa Shirikisho la Kandanda la Ujerumani Hendrik Grosse alisema wamechukua tahadhari. "Tulishirikiana na vilabu na tumejenga viwanja vilivyo salama Ujerumani. Ina maana kuwa usalama wa ramani za viwanya hivyo na muundo vimeimarishwa vizuri kwa miaka mingi. Ni wazi kuwa chini ya mazingira haya lazima tuongeze nguvu katika kazi ya upelelezi ya vyombo vya usalama na hatua mwafaka lazima zitekelezwe. Hiyo huenda ikajumuisha ukaguzi zaidi katika milango ya viwanja na uwepo wa polisi wengi hadi kuufuta mchuano kama uamuzi wa mwisho ikiwa itahitajika".

Vilabu vya Bundesliga vimeimarisha hatua za usalama, kwa kufanya ukaguzi zaidi wa mashabiki wanaoingia viwanjani na pia kupiga marufuku fataki uwanjani.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP/AP/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com