1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vilabu Bundesliga vinajiandaa kuingia duru ya pili

Sekione Kitojo
6 Januari 2020

Vilabu  18 vya  kandanda  nchini  Ujerumani vya  Bundesliga  vimo katika  maandalizi makubwa  hivi  sasa , kujiandaa  kwa  ajili  ya duru  ya  pili  ya  ligi  hiyo inayoanza  tarehe 17 mwezi huu.

https://p.dw.com/p/3VmBS
Katar | Manuel Neuer im Trainingslager
Picha: Imago-Images/MIS/B. Feil

Timu mbali  mbali zimekwenda  katika  vituo  mbali  mbali  na  kuweka kambi, ambapo ndimu nyingi ziko nje  ya  nchi  hiyo. Na  timu  hizo zimepanga  kufanya michezo  mbali  mbali  ya  majaribio, ambapo kesho Jumanne Borussia  Dortmund  inapambana  na  Standard Lutich  ya  Ubelgiji , FC Schalke 04 itajipima  nguvu  na  St. Truiden na  Jumatatu jioni  Werder Bremen itajipima  nguvu  na Monza.

Wakati  huo  huo Bayern Munich  imechukua  hatua  ya  maandalizi ya  muda  mrefu  ujao baada  ya  kupata  saini  ya  mlinda  mlango wa  Schalke Alexander Nuebel, ambaye  atajiunga  na  mabingwa hao  watetezi majira  ya  joto  mwaka  huu kwa  mkataba  wa  miaka mitano, kocha  wa  muda  wa  Bayern Munich Hansi Flick amesema leo. Hii  ni  kuona  mbali  sana, Flick  amesema  katika  siku  ya kwanza  ya  maandalizi  ya  timu  yake mjini  Doha  Qatar.

Flick  ambaye  amechukua  nafasi  ya  Niko Kovac  mwanzoni mwa mwezi  Novemba  na  atakuwa  mwalimu  wa  kikosi  hicho hadi pengine mwishoni  mwa  msimu, ana  matumaini  kwamba  mabingwa hao  wa  Ujerumani watafikia  makubaliano  na  nahodha Manuel Neuer ya  kurefusha  mkataba  wake.

Hans Tilkowski , mlinda  mlango wa  timu  ya  taifa  ya  Ujerumani magharibi  wakati  huo  katika  fainali  ya  kombe  la  dunia  la mwaka  1966 dhidi ya  England na  kufanyika  nchini  England amefariki  dunia  akiwa  na  umri  wa  miaka  84. Tilkowski  alikuwa mchezaji  wa  Borussia  Dortmund.