Vikosi zaidi vyahitajika Dafur | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 15.08.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

IDHAA YA KISWAHILI

Vikosi zaidi vyahitajika Dafur

Wito wa kuongeza wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa umekuwa ukiongezeka wakati makundi yanayopingana katika jimbo lenye vurugu la Dafur nchini Sudan yakiwa yamekwama kwenye mkondo wa umwagaji damu.

default

Muhanga alienusurika wa Dafur akishikilia mabufuru ya binaadamu.

Mzozo huo umepoteza maisha ya takriban watu nusu milioni katika kipindi cha miaka minne iliopita.

Generali Martin Luther Agwai ambaye anaongoza kikosi cha wanajeshi 9,000 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Dafur amewaambi waandishi wa habari kuwa wamepelekwa kwenye ulingo wa masumbwi huku mikono yao ikiwa imefungwa nyuma ya mgongo.Anasema wanahitaji helikikopta sita za mashambulizi lakini hakuna mtu aliekuwa tayari kutowa helikopta hizo na hafahamu kwa nini watu wanakataa kutowa helikopta hizo.

Agwai akiendelea kufafanuwa anasema wakati alipokubali kazi yake ya hivi sasa kama kamanda wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Matafa huko Dafur (UNAMID) zaidi kidogo ya mwaka mmoja uliopita alikuwa akitegemea kuongoza kikosi cha kimataifa chenye kujumuisha wanajeshi wasiopunguwa 26,000.

Generali huyo ameelezea matumani yake kwamba yumkini wakawa na asilimia 80 ya wanajeshi hao 26,000 waliopendekezwa mwishoni mwa mwaka huu.

Ifikapo mwakani takriban wanjeshi wengi wa zaidi wanatarajiwa kutoka katika mataifa kadhaa ya Afrika yakiwemo Burkina Faso,Gambia,Kenya, Malawi,Nigeria,Senegal na Afrika Kusini.

Shughuli hizo bado zinahitaji zaidi ya wanajeshi 17,000 lakini kumekuwepo na mapendekezo machache ya kutolewa kwa nguvu kazi na zana ukiachia mbali helikopta nne kutoka Ethiopia.Hivi karibuni Misri na Ethiopia zilichangia baadhi ya wanajeshi.

Serikali ya Sudan ambayo ina mashaka mazito juu ya dhamira za mataifa ya magharibi inasisitiza kuwepo kwa kikosi cha Kiafrika na tayari imekataa wanajeshi kutoka Norway na Sweden pamoja na kuelezea kusita kwake kukubali vikosi vya kijeshi kutoka Thailand na Nepal.

UNAMID kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Dafur kimekabidhiwa majukumu ya kuhakikisha kutekelezwa kwa Makubaliano ya Amani ya Dafur ya mwaka 2008 kati ya serikali na waasi wanaopambana kuwania udhibiti wa jimbo hilo.

Kikosi hicho cha kulinda amani chini ya uongozi wa Agwai kina mamlaka ya kuwalinda raia kutokana mashambulzi na kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa misaada pamoja na wafanyakazi wake yenyewe na vituo na vifaa.

Licha ya kuwapo kwa makubaliano hayo juu ya haja ya shughuli za amani jumuiya ya kimataifa inaendelea kugawika juu ya namna ya kukabiliana na serikali ya Sudan.Marekani na washirika wake bado ingali wanataka kuweka vikwazo dhidi ya Sudan lakini Urusi na China nchi zote mbili zinafikiri kwamba vikwazo havitokuwa na tija.

Kwa upande wake takriban mataifa yote ya Afrika sio tu yameleezea upinzani wao juu ya uwezekano wa kuweka vikwazo bali pia yameshutumu hatua ya kumshtaki Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan kama mhalifu wa kivita katika Mahkama ya Jinai ya Kimataifa huko The Hague nchini Uholanzi.

Kinyume chake katika mataifa ya magharibi makundi ya kutetea haki za binaadamu yamekaribisha ombi la hivi karibuni la mwendesha mashtaka wa mahkama hiyo la kumshatki Bashir kwa kuona kwamba hatua hiyo itaweka mfano kwa wakiukaji wa sheria za kimataifa za haki za binaadamu.Kuna ushahidi mkubwa kwamba serikali ya Sudan bado inaunga mkono mashambulizi ya wanamgambo wa Janjaweed huko Dafur.

Umoja wa Mataifa umedokeza kwamba zaidi ya watu milioni mbili wamepotezewa makaazi yao katika jimbo la Dafur tokea kuzuka kwa mzozo kati ya makundi ya waasi ya wananchi asilia na makundi ya wanamgambo ya Jananweed takriban miaka minne iliopita.

 • Tarehe 15.08.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Exda
 • Tarehe 15.08.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Exda
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com