1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Virusi vya Corona yaziathiri timu za Bundesliga

Deo Kaji Makomba
27 Machi 2020

Vigogo vinne vya soka vinavyoshiriki ligi kuu ya kandanda ya Bundesliga vimeahidi kuzisaidia timu wapinzani wao katika ligi hiyo ambazo hivi sasa zinakabiliwa na tatizo la kiuchumi kufuatia mripuko wa virusi vya Corona.

https://p.dw.com/p/3a8eG
Fußball Champions League - RB Leipzig vs Tottenham Hotspur
Kikosi cha RB Leipzing, miongoni mwa timu nne za juu katika BundesligaPicha: Getty Images/AFP/J. Macdougall

Hatua hiyo imetangazwa Alhamis tarehe 26.03.2020 na kitengo cha bodi ya ligi ya Ujerumani, DFL.

Vilabu hivyo ni vile vilivyo katika nafasi nne za juu katika msimamo wa ligi kuu ya Bundesliga. Bayern Munich, Borussia Dortmund, Bayer Leverkusen na RB Leipzig ambavyo vyote vimefanikiwa kutinga katika msimu wa ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Kulingana na DFL, vilabu hivyo vilisema kuwa vitahakikisha fedha zinapatikana kwa ajili ya kuzisaidia timu hizo ambazo zinakabiliwa na tatizo la kiuchumi zilizoko ligi kuu ya Bundesliga na zile za daraja la pili ambazo zinaendeshwa na DFL.

"Uamuzi huu unasisitiza ukweli kwamba mshikamano sio maneno matupu katika Bundesliga," alisema Christian Seifert, rais wa DFL na kuongeza kuwa "DFL inawashukuru sana washiriki hao wanne wa ligi ya mabingwa barani Ulaya."

Vilabu hivyo vinne kutoa euro milioni 12.5

Vilabu hivyo vinne vitatoa euro milioni 12.5 kutoka katika sehemu za hisa zao za haki za mapato ya matangazo ya runinga na kuongeza kiasi kingine cha uero milioni 7.5 kutoka katika akiba zao.

DFL yenyewe itakuwa na jukumu la kuamua ni kwa namna gani fedha hizo zitagawanywa kwa vilabu hivyo vya ligi kuu na vile vya daraja la pili.

"Katika nyakati hizi ngumu, ni muhimu kwamba mabega yenye nguvu kuchangia kuyasaidia mabega dhaifu. Tunataka kuonyesha kwamba watu wa kandanda tunasimama pamoja," alisema mkurugenzi mtendaji wa klabu ya Bayern Karl-Heinz Rummenige katika taarifa yake.

"Siku zote tulisema kuwa tulitaka kuonyesha mshikamano wakati klabu zinapokuwa katika kipindi kigumu hasa kutokana na hali hii ya dharura na ambayo hawakuisababisha wao," alisema mwenzake wa klabu ya Dortmund, Hans Joachim Watzke.

Fußball Mitgliederversammlung von Borussia Dortmund
Hans Joachim Watzke mkurugenzi mtendaji wa Borussia Dortmund.Picha: picture-alliance/G. Kirchner

Awali mkurugenzi mtendaji wa klabu ya Dortmund alisababisha hasira aliposema kuwa vilabu ambavyo vilifanya makosa ya kifedha na michezo katika miaka ya hivi karibuni havipaswi kusaidiwa kifedha na wapinzani wao.

Katika nchi ambapo klabu chache zinadhaminiwa na wawekezaji mabilionea, timu nyingi za Bundesliga zina wasiwasi kuhusiana na hatma yao wakati wa kipindi cha shida.

Kwa upande wao wachezaji wa klabu ya Werder Bremen wamejitolea wasilipwe mishahara yao ili kuisaidia klabu hiyo ambayo iko katika hatari ya kushuka daraja huku pia ikikabiliwa tatizo la kiuchumi, wakati mkuu wa idara ya masoko wa klabu ya Schalke Alexander Jobs akisema kuwa klabu hiyo iko hatarini kutokana mtikisiko wa kiuchumi kufuatia mlipuko wa virusi hatari vya Corona.

Pamoja na mechi za ligi kuu ya Bundesliga kusimamishwa hadi angalau mwishoni mwa mwezi Aprili, klabu nyingi zinatumaini kuwa msimu wa ligi hiyo inaweza kuchezwa nje ya muda wakati wa kufungwa kwa dirisha katika kipindi cha majira ya joto kuzuia upotezaji mkubwa wa mapato ya televisheni.

Rais wa zamani wa klabu ya Bayern, Uli Hoeness Alhamis tarehe 26.03.2020, alionya kwamba kama hakuna mechi zitakazochezwa kabla ya mwisho wa mwaka, msingi mzima wa ligi hiyo utaathirika.

"Hivi sasa, mshikamano unahitajika kuwa hai, sio kuzungumziwa tu," Hoeness aliliambia jarida la habari za michezo la Kicker la hapa Ujerumani.