1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yazidi kutuma vifaru Syria

25 Agosti 2016

Vifaru vyengine kumi vya Uturuki Alhamisi (25.08.2016) vimevuka mpaka kuingia Syria siku moja baada ya wapiganaji wa upinzani wa Syria wanaoungwa mkono na Uturuki kuwatimuwa wanajihadi katika mji wa Jarabulus.

https://p.dw.com/p/1JpPn
Türkei Offensive gegen IS in Syrien
Picha: Getty Images/AFP/B. Kilic

Vifaru hivyo vinatarajiwa kuungana na vile ambavyo vilivuka mpaka hapo jana katika Operesheni Ngao ya Euphrates ambayo Uturuki inasema inakusudia kuwatokemeza wanamgambo wa itikadi kali wa kundi la Dola la Kiislam na wale wa Kikurdi.

Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema hapo jana kwamba mashambulio yao yamelitimuwa kundi la Dola la Kiislamu kutoka kwenye mji wa Jarabulus na waasi wanaoungwa mkono na serikali ya Uturuki wameripoti kwamba wapiganaji hao wa jihadi wamerudi nyuma kuelekea kusini mwa mji wa Al- Bab.

Mlolongo mpya wa vifaru ulikuwa ukirindima kwenye barabara chafu maghaibi mwa mji wa mpakani wa Uturuki wa Karkamis na kutimua vumbi hewani kabla ya kuvuka mpaka.Vifaru hivyo baadae vilifuatiwa na magari ya deraya.

Operesheni kubwa kabisa

Operesheni hiyo kubwa kabisa kuwahi kuanzishwa na Uturuki katika kipindi cha miaka mitano na nusu ya mzozo wa Syria imeviweka nchi kavu vikosi maalum vya Uturuki na ndege zake za kivita zikishambulia maeneo ya kundi la Dola la Kiislamu.

Mashambulizi ya Uturuki nchini Syria.
Mashambulizi ya Uturuki nchini Syria.Picha: Getty Images/AFP/B. Kilic

Ndege hizo zinasaidia mashambulizi ya ardhini yanayofanywa na mamia ya waasi wa Syria ambao hapo jana waliingia katika mji wa Jarabulus na vijiji vya jirani bila ya kukabiliwa na upinzani mkubwa.

Waziri Mkuu wa Uturuki Binali Yildrim amekiambia kituo cha televisheni cha Haberturk katika mahojiano kwamba wapiganaji wa upinzani wa Syria wamebakia katika mji wa Jarabulus na wameanza kudhibiti miji na vijiji.

Wakurdi wawe sehemu ya ufumbuzi

Hapo jana mwanasiasa mwandamizi wa Kikurdi nchini Iraq ambaye ni mjumbe wa baraza la uongozi Ali Hussein amesema vyama vya kisiasa nchini Syria havina budi kuchukuwa hatua ambazo hazitokuwa tishio kwa usalama wa kanda hiyo baada ya Uturuki kutuma vifaru vyake nchini humo.

Mpiganaji wa Kikurdi nchini Syria.
Mpiganaji wa Kikurdi nchini Syria.Picha: picture-alliance/dpa/S. Suna

Hussein amesema "Tumewashauri na kuwashajiisha Wakurdi walioko nchini Syria wasikubali kukiachilia hata chama kimoja au kundi moja kuhodhi na kutumia kwa hila mamlaka ya kujiamulia mambo yao. Wakurdi na Wasyria wengine wote wanaweza kushirikiana kwa faida yao ya pamoja.Inabidi wajaribu kufikia makubaliano ya kisiasa.Hawapaswi kuwa sehemu ya tatizo nchini Syria bali wawe sehemu ya ufumbuzi nchini humo."

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amemwambia waziri mwenzake wa Uturuki kwamba vikosi vya Kikurdi nchini Uturuki vimeanza kujiondowa mashariki mwa mto Euphrates ambalo ni dali kuu la serikali ya nchi hiyo baada ya kutuma vikosi vyake maalum na vifaru kuwasaidia waasi kuwatimuwa wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu.

Serikali ya Uturuki imesema hapo jana kwamba itaendeleza operesheni zake hadi hapo itakapokuwa imeamini kwamba vitisho dhidi ya usalama wake wa taifa vimedhibitiwa.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/AP

Mhariri : Abdu- Mtulya