1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Mauaji dhidi ya wanawake yaongezeka

Veronica Natalis
27 Oktoba 2023

Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu nchini Tanzania, LHRC, inayoonesha idadi ya wanawake wanaouwawa kila mwezi imeongezeka na kufikia 53 kutoka 43 kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

https://p.dw.com/p/4Y66d
Wanawake wakiwa katika kazi za mikono
Wanawake wakiwa katika kazi za mikonoPicha: Paul Lorgerie/DW

Ripoti hiyo iliyozinduliwa mjini Arusha kaskazini mwa Tanzania pia imeonesha kuwa  mauaji mengi ya wanawake hao yanafanywa na ndugu wa karibu, kwa imani za kishirikina na wivu wa kimapenzi. 

Utafiti wa ripoti hiyo uliofanyika katika mikoa ya Geita, Shinyanga, Mwanza, Dar es Salaam na Kilimanjaro, pamoja na mambo mengine ulikuwa na lengo la kutathimini kwa ujumla hali ya mauaji ya wanawakekatika mikoa iliyochaguliwa.

kadhalika ililenga kutathimini sera na mifumo ya kisheria ya sasa inayohusika kuwalinda wanawake pamoja na kutoa mapendekezo kwa serikali ya Tanzania juu ya kulishughulikia suala hilo. 

Soma pia:Kampeni ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake yaanza

Getrude Abene ni afisa mwandamizi wa masuala ya jinsia, wanawake, watoto pamoja na watu wenye ulemavu kutoka kituo cha  LHRC, pamoja na kusisitiza kuwepo na sheria zinazowalinda wanawake ili kukomesha vitendo hivyo, lakini pia alitilia mkazo  uwepo wa ushirikiano kutoka kwa mashirika yote yanayotetea haki za wanawake.  

"kuunganisha nguvu za wadau kama mahakama, jeshi la polisi kuhakikisha kunapatikana taarifa hizi,"  alisema Abene.

Aliongeza kuwa kuna haja matukio haya kurekodiwa kama mauaji ya wenza na si kama mfumo wa sasa , ambo unarekodi kama mauaji mengine.

Ripoti: Wanawake 53 wanauwawa kila mwezi

Ripoti hiyo inaonesha kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2018 hadi Septemba mwaka 2022, wanawake 2,438 waliuwawa ikiwa ni sawa na wastani wa wanawake 492 wanaouwawa kila mwaka na wastani wa wanawake 53  wanaouwawa kila mwezi. 

LHRC inasema kuwa mauaji ya wanawake ni ukatili unaopaswa kukemewa na kipigwa vita kwa nguvu zote.

Ukatili wa kijinsia, tunapambana nao vipi?

Jumuiya mbali mbali za kimataifa zimepitisha sheria za kupinga vitendo hivyo, azimio la Vienna la kupinga mauaji ya wanawake na wasichana, pamoja na azimio la kimataifa la baraza la haki za binadamu linazitaka nchi wanachama Tanzania ikiwamo, kufanya juhudi za kutokomeza mauji ya wanawake.

Soma pia:Matukio ya ukatili wa kijinsia yaongezeka Tanzania

Judith Singibara mwanaharakai wa haki za wanawake kutoka mjini Arusha alisema katika kutokomeza mauaji dhidi ya wananwake kuna haja ya kuwashirikisha wanaume katika kampeni za kupinga ukatili wa kijinsia.

"Kuna haja ya kuwashirikisha wanaume na wavulana katika kampeni za kupinga ukatili." Aliiambia DW Singibara.

Mapambano dhidi ya kuwalinda wanawake na aina zote za unyanyasaji yamekuwa yakisikika kote dunianiani.

Hata hivyo juhudi hizo zinaonekana kuzaa matunda lakini wanaharakati wa haki za wanawake wanasema bado kuna maeneo mengi yanahitaji kurekebishwa ili kumlinda mwanamke.