1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uswisi yasonga 16 bora, Ujerumani yalizwa na Colombia

Lilian Mtono
30 Julai 2023

Uswisi na Norway zimefuzu kuingia kwenye hatua ya 16 bora kwenye michuano ya Kombe la Dunia la Wanawake huko nchini New Zealand na Australia

https://p.dw.com/p/4UYlh
Frauen Fußball WM 2023 | Philippinen v Schweiz
Picha: MOLLY DARLINGTON/REUTERS

Uswisi wamemaliza wakiwa wanaongoza kwenye kundi A, baada ya kutoka sare ya bila kufungana na New Zealand, wakati Norway ikiicharaza Ufilipino mabao 6-0, walipokutana huko Auckland na kuwapiku wenyeji hao wa michuano kwa tofauti ya mabao.

Colombia nayo imetoka kifua mbele baada ya kuwafunga Ujerumani kwa mabao 2-1 katika mechi ya makundi kwenye michuano ya Kombe la Dunia la wanawake.

Australien Sydney | Frauen Fußball WM | Kolumbien gewinnt gegen Deutschland
Timu ya soka ya wanawake ya nchini Colombia wakishangilia bao ya pili na kumaliza mchezo wao kwa mabao 2-1 dhidi ya UjerumaniPicha: Frank Fife/AFP/Getty Images

Ilikuwa dakika ya 97 ambapo Manuela Viegas alimalizia mpira wa kona, na kufunga bao la kichwa lililopeleka ushindi kwa kina dada hao walioonyesha soka safi kabisa dhidi ya Ujerumani na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya 16 bora.

Ujerumani ilijipatia bao lake kupitia mkwaju wa penati uliopigwa kwa ustadi na Alexandra Popp katika dakika ya 89. Bao la kwanza la Colombia lilifungwa na nyota wake Linda Caicedo. Ujerumani yenye pointi tatu, sasa itakwaana na Korea Kusini na Colombia itakutana na Morocco.