USA-AFRICA-BUSH | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.02.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

USA-AFRICA-BUSH

Rais George W. Bush wa Marekani kesho anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania ambako atatumia muda wake mwingi ikiwa ni katika ziara yake ya kuzitembelea nchi tano barani Afrika

Polisi wakisachi nyumba ya bwana Klaus Zumwinkel

Polisi wakisachi nyumba ya bwana Klaus Zumwinkel


Rais Bush anatarajiwa pia kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na maendeleo ya kampeni dhidi ya UKIMWI.


Mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani, Stephen Hadley amesema kwamba ziara ya Bush itakuwa ni nafasi nzuri kwa marekani kuelezea majukumu iliyonayo kwa nchi za Kiafrika na waafrika kwa ujumla.


Anasema kwamba hivi sasa bara la Afrika linaleta matumaini makubwa na hali hiyo inawafanya watu wa Marekani kujivunia kwamba kila mipango wanayoianzisha inaleta mabadiliko.


Hata hivyo katika ziara hiyo ambayo ililenga kuangalia masuala ya uwekezaji katika afya na mipango ya maendeleo, itagubikwa pia na masuala ya migogoro inayoendelea nchini Kenya na katika jimbo la Darfur nchini Sudan.


Rais Bush pia anatarajiwa kuzungumza na viongozi wa Afrika kuhusu hali ya Kenya, ambako mapigano yaliyosababishwa na uchaguzi wa hivi karibuni yamesababisha vifo vya watu elfu moja pamoja na suala la kuwepo haja ya kupelekwa kikosi cha wanajeshi zaidi wa umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa cha kuweka amani.


Marekani ilitoa wito kwa jumuiya ya Kimataifa kuweka kiasi cha wanajeshi wa kulinda amani ishirini na tano elfu katika mipaka ya Darfur na Bush amekuwa akilaumu kwamba juhudi hizo zinakwenda taratibu.


Masuala hayo pia yameelezewa na rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ambaye sasa ni mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika wakati nchi yake pia imeathirika na mapigano ya nchi jirani ya Kenya.


Akiwa nchini Tanzania Rais Bush anatarajiwa kuelezea mikakati yake ya kuboresha hali ya afya barani Afrika ikiwa ni sehemu ya mpango wa dharura wa rais wa kupunguza maambukizi ya Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa UKIMWI na juhudi za rais za kupambana na Malaria.


Mpango huo wa kupambana na UKIMWI, haujabadilishwa tangu mwaka 2003, rais Bush alipotangaza kutengwa kwa bilioni kumi na tano kwa ajili ya mpango wa miaka mitano wa kupambana na ugonjwa huo kwa kutengeneza dawa za kupunguza makali kwa waathirika na kuboresha huduma za afya kwa wagonjwa wa UKIMWI.


Ziara ya Bush Afrika, inayoanza leo tarehe kumi na tano na kumalizika tarehe ishirini na moja mwezi huu, ni ya pili kwa kiongozi huyo na ya tano kwa mke wake Laura.


Rais Bush na mke wake Laura, watapata nafasi ya kutembelea Hospitali, shule na kukagua biashara mbalimbali na pia itakuwa ni nafasi nzuri kueleza imani na huruma aliyonayo.


Ziara hiyo itamwondoa rais Bush katika masuala kama ya Vita vya Iraq na kuyumba kwa uchumi wa Marekani ambao unazinyemelea familia nyingi za wamarekani ambao wapo katika harakati za kuelekea katika uchaguzi mkuu.


Mbali na kuitembelea nchi ya Tanzania, Rais Bush pia atazitembelea nchi za Rwanda, Benin, Ghana na Liberia, ziara ambayo imepangwa na Serikali ya Marekani.


Hii ni mara ya kwanza kwa rais wa Marekani kukaa Tanzania kwa siku nne, kwani mara ya mwisho rais wa zamani wa nchi hiyo Bill Clinton alipoitembelea nchi hiyo mwaka 2003, alikaa kwa muda wa masaa matatu pekee.


 • Tarehe 14.02.2008
 • Mwandishi Mazula, Scholastika
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D7Xx
 • Tarehe 14.02.2008
 • Mwandishi Mazula, Scholastika
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D7Xx
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com