1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wasema "Uchaguzi wa DRC hautafanyika"

23 Novemba 2018

Muungano wa wakongomani kwa ajili ya kipindi cha mpito bila ya Kabila madarakani CCT umesema uchaguzi wa Disemba 23 hautafanyika.

https://p.dw.com/p/38mcy
Demokratische Republik Kongo Wahlmaschine
Picha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Rais wa muungano huo Emerie Damien Kalwira ameiambia DW leo kuwa uchaguzi ujao ni njama ya rais Joseph Kabila kuendelea kubakia madarakani na kutoa wito kwa upande wa upinzani na jumuiya ya kimataifa kukataa ulaghai wa serikali ya mjini Kinshasa

Kalwira ameorodhesha sababu lukuki ambazo kwa maoni ya vuguvugu analoliongoza zitatatiza uwezekano wa DRC kufanya uchaguzi ikiwemo suala la ukubwa wa kieneo wa nchi hiyo kuwezesha kusambaza vifaa vya uchaguzi na kusimamia zoezi la upigaji kura ikilinganishwa na muda mchache uliosalia.

Taifa hilo linaloandamwa na mizozo lina ukubwa wa kilomita za mraba zaidi milioni 2.3  zinazoifanya kuwa nchi kubwa kuliko zote kusini mwa Jangwa la Sahara na karibu robo tatu ya ukubwa wa bara zima la Ulaya lakini ina kilometa 27,877 pekee ya barabara za lami.

Mwanasiasa huyo amesema kiwango cha vifaa kilichokabidhiwa kwa tume ya uchaguzi hakitoshi kutokana na ukubwa wa nchi hiyo ambayo vilevile haina miundombinu ya kutosha ya barabara kuwezesha usafirishaji wa vifaa vya kupigia kura.

Changamoto ni nyingi kufanikisha uchaguzi

USA New York Vereinte Nationen Joseph Kabila
Picha: picture-alliance/Xinhua/Q. Lang

Serikali ya Congo ambayo ina uhusiano mgumu na Umoja wa Mataifa, imekataa aina yoyote ya msaada wa kimataifa wakifedha au wa vifaa kwa ajili ya uchaguzi katika taifa hilo la pili kwa ukubwa barani Afrika.

Ujumbe wa kulinda amani wa MONUSCO umependekeza kutumia helikopta zake na ndege kusafirisha mashine za kupigia kura nchini kote. Lakini serikali mjini Kinshasa inataka ujumbe huo uondoke kufikia 2020.

Kadhalika Kalwira amezungumzia suala la ukosefu wa nishati ya umeme kwa ajili ya kuendesha mashine za elektroniki za kupigia kura ambazo upinzani umepinga matumizi yake kwa miezi kadhaa sasa.

Tume ya uchaguzi CENI inasimamia uamuzi wake wa kutumia mashine 106,000 za kielektoniki katika uchaguzi huo, zilizotolea na Korea Kusini, licha ya matakwa ya upinzani -- na hasa Fayulu-- ya kutumia karatasi.

Kalwira amemtuhumu rais kabila na mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi nchini DRC Corneille Nangaa kuwa wanalenga kuvuruga uchaguzi na kuzusha machafuko yatakayolazimisha mazungumzo na kumwezesha Kabila kubakia madarakani.

Pazia la kampeni lafunguliwa

DR Kongo Wahlkampf in Kinshasa
Picha: Getty Images/AFP/S. Tounsi

Hayo yanakuja wakati kampeni za uchaguzi zimefungua pazia hapo siku ya Alhamisi.

Wagombea 21 wameandikishwa kuwania nafasi ya kumrithi Kabila mwenye umri wa miaka 47, ambae ameitawala nchi hiyo tangu Januari 2001, baada ya kuuawa kwa baba yake Laurent-Desire Kabila.

Karibu nusu ya raia wa Congo milioni 80 wana haki ya kupiga kura.

Baada ya kukabiliwa na shinikizo kubwa la kimataifa dhidi ya kuwania muhula wa tatu, Kabila aliamua kumuunga mkono mteule wake Emmanuel Ramazani Shadary mwezi Agosti.

Shadary ni mmoja ya Wacongo 15 waliowekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya, wakituhumiwa kwa uvunjaji wa haki za binadamu wakati alipokuwa waziri wa mambo ya ndani kati ya Desemba 2016 na mwanazoni mwa 2018.

Mmoja ya wapinzani wakuu wa Shadary ni Martin Fayulu, mbunge asiejulikana ambaye mapema mwezi huu aliteuliwa kuwa mgombea wa pamoja wa vyama kadhaa vya upinzani -- lakini siyo vyote -- vinavyounda muungano bungeni.

Mwandishi: Rashid Chilumba

Mhariri:Yusuf Saumu