1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Ghana waonya njama za kuvuruga matokeo ya uchaguzi

Sylvia Mwehozi
9 Desemba 2020

Kiongozi wa upinzani wa Ghana amemuonya Rais Nana Akufo-Addo dhidi ya njama zozote za kuiba kura katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatatu, huku pande zote mbili zikidai kushinda uchaguzi.

https://p.dw.com/p/3mUDO
Afrika Ghana Präsidentschaftswahlen  John Dramani Mahama
Picha: Nipah Dennis/AFP/Getty Images

Kauli hiyo nzito iliyotolewa na mgombea wa upinzani John Mahama imepandisha joto baada ya uchaguzi wa rais na bunge uliofanyika siku ya Jumatatu katika taifa hilo linalofahamika kwa utulivu katika kanda iliyokumbwa na ghasia.

"Baadhi ya mambo yanayotokea hayakubaliki na Nana Akufo-Addo anaendelea kuonyesha rekodi ambazo si za kidemokrasia” alisema Mahama wakati alipozungumza na waandishi wa Habari Jumanne jioni.

Mahama alidai pia kuwa jeshi lilitumiwa kujaribu kupindua baadhi ya matokeo katika majimbo ambayo ameyashinda, na kutishia kugomea alichokitaja kuwa ''jaribio lolote la kuingilia dhamira ya watu wa Ghana”.

Waziri wa habari Kojo Oppong Nkrumah amekanusha madai kwamba wanajeshi waliingilia katika uchaguzi huo akisema hayana ukweli. Tume ya uchaguzi bado haijatangaza matokeo rasmi ya mwisho lakini ushindani ulitarajiwa kuwa baina za wagombea wawili, John Mahama na Nana Akufo-Addo wa chama cha New Patriotic Party NPP, huku kura za maoni za hivi karibuni zikimuweka mbele kwa ushindi kidogo rais aliyeko madarakani.

Mchakato wa kuhakikisha kura waendelea

Tume ya uchaguzi imewataka wananchi kusubiri, ikisema kwamba inafanya kazi kuhakikisha matokeo yanayotolewa ni sahihi na yanayoakisi matakwa ya wananchi”.

Timu ya rais ilitoa matokeo yasiyo rasmi siku ya Jumanne ikidai kuwa asilimia 91 ya matokeo kutoka vituo vya kupigia kura yanaonyesha kuwa rais Akufo-Addo anaongoza kwa asilimia 52.25 na Mahama ana asilimia 46.44. Mahama kiongozi wa chama cha National Democratic Congress NDC, wakati huo amedai kushinda viti vingi bungeni 140 kati ya 275.

Hata hivyo madai hayo ya upinzani ya ushindi bungeni yanapingwa vikali na serikali inayosema tangazo kama hilo "litahatarisha amani ya nchi”

Ghana | Präsidentschaftswahlen
Raia wa Ghana wakisherehekea ushindiPicha: Pius Utomi Ekpei/AFP/Getty Images

Jumla ya waangalizi 12,000 walisambazwa siku ya kupiga kura kote nchini Ghana. Muungano unaowakilisha asasi za uangalizi wa CODEO umesema waangalizi wake 4,000 wameripoti matukio 254 wakati wa zoezi la kupiga kura. "Wakati kulikuwa na baadhi ya changamoto, lakini changamoto hizo hazikuahiri uhalali wa mchakato mzima”, ulisema muungano huo.

Hakujawahi kuwepo na raundi ya pili katika chaguzi za Ghana na vyama viwili vikubwa vimekuwa vikikabidhi madaraka kwa amani kwa mara saba mfululizo tangu kurejea kwa demokrasia zaidi ya miaka 30 iliyopita.

Ili kuhakikisha utamaduni huo wa uchaguzi wa amani unaendelezwa, Akufo-Addo na Mahama walitia Saini mkataba wa ishara ya amani siku ya ijumaa. Utulivu katika taifa hilo unatofautiana na ule wa nchi za jirani katika ukanda huo ambazo hutawaliwa na ghasia ikiwemo Guinea na Ivory Coast.

Masuala muhimu yaliyotawala uchaguzi wa mwaka huu ni ukosefu wa ajira, miundombinu, elimu na afya. Nchi hiyo ambayo ni ya pili katika uzalishaji wa kakao duniani imepiga hatua katika kipindi cha miaka 20 iliyopita lakini watu wake wengi bado wanaishi katika umaskini uliokithiri n anchi ikikabiliwa na ongezeko la madeni.