Upinzani DRC wakubali mashine za kupigia kura | Matukio ya Afrika | DW | 17.12.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

UCHAGUZI DRC

Upinzani DRC wakubali mashine za kupigia kura

Hatimaye vuguvugu kuu la upinzani linalomuunga mkono mgombea Martin Fayulu limekubali kutumia mfumo wa upigaji kura kwa kompyuta likisema ni juhudi ya kumzuia Rais Joseph Kabila kuendelea kubaki madarakani.

Kupitia meneja wake wa kampeni yake Pierre Lumbi, Fayulu - anayeungwa mkono na Moise Katumbi pamoja na Jean-Pierre Bemba - alisema Jumapili ya tarehe 23, wafuasi wao wajitokeze kwa wingi kupiga kura kuweko au kusiweko mfumo wa kura za kieletroniki.

"Vuguvugu la LAMUKA linawakikishia raia nia yake ya kushiriki kwenye uchaguzi, na halitarajii hata kidogo kususia uchaguzi huo na haliwezi kukubali hata kidgo kuahirishwa kwa uchaguzi huu kwa sababu zozote zile," alsiema Lumbi kwa niaba ya Fayulu.

Fayulu alikuwa mstari wa mbele kupinga matumizi ya kompyuta za kupigia kura, msimamo uliomtafautisha na wapinzani wengine, wakiwemo Felix Tshisekedi na Vital Kamerhe, na wengine kudai ndiyo sababu ya kuvunjika kwa mkataba wa kuweko na mgombea mmoja wa upinzani.

Wadadisi wa mambo wanasema msimamo huu mpya wa Fayulu na vuguvugu lake la LAMUKA unawakanganya wafuasi wake.

CENI yaagiza fomu za matokeo Afrika Kusini

Hayo yakiripotiwa na Tume Huru ya Uchaguzi ya Kongo (CENI) ikielezea kwamba uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa, mwenyekiti wa tume hiyo, Corneille Nangaa, anaripotiwa kuwapo mjini Johanesburg, Afrika ya Kusini, kuagiza fomu za kunakili matokeo ya uchaguzi. 

Demokratischen Republik Kongo | Wahlkommision | Corneille Nangaa (DW/F. Quenum)

Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya DRC, Corneille Nangaa.

Fomu hizo zinasubiriwa katika vituo vya kupigia kura 80,000 kote nchini Kongo na tayari hofu imezuka endapo kweli uchaguzi utafanyika ndani ya kipidi cha siku sita zilizosalia, hasa inapozingatiwa pia hali ya kiusalama kwenye maeneo kadhaa ya taifa hilo kubwa kabisa kwenye ukanda wa Maziwa Makuu.
 
Tukio karibuni kabisa ni la hapo Jumapili (Novemba 16) ambapo waasi walilivamia ghala linalotumiwa na CENI kwenye mji mkuu huo wa jimbo la Kivu Kaskazini, Beni, mashariki mwa Kongo. 

Hata hivyo, waasi hao walishindwa nguvu na polisi na uvamizi wao haukuwa na madhara, kwa mujibu wa Jean-Pierre Kalamba, msemaji wa CENI.

Wiki iliyopita, moja ya maghala yanayotumiwa na CENI kwenye mji mkuu Kinshasa liliunguwa moto na kuharibu mashine 8,000 za kupigia kura. Kundi la waasi wa ADF limekuwa likiendelea na mashambulizi mashariki mwa nchi hiyo, ambapo wiki iliyopita liliwauwa watu 10 na wengine wanane kabla ya hapo.

Hali ya usalama nchini Kongo kuelekea uchaguzi huu unaotazamiwa kuwa wa kwanza kuwezesha makabidhiano ya madaraka kwa amani, imekuwa ikitia mashaka kila uchao, sio tu kutokana na kitisho cha makundi ya waasi, bali pia kutoka kwa vyombo vya usalama vya serikali.

Ijumaa iliyopita, mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, alilaani vikali mashambulizi yanayofanwa na vyombo vya usalama dhidi ya wapinzani, akitoa wito kwa serikali mjini Kinshasa kuhakikisha uhuru wa watu kukutana na kujieleza unalindwa kikamilifu. 

Wiki ya mwisho ya kampeni

Kongo Emmanuel Ramazani Shadary (REUTERS)

Mgombea urais kupitia muungano wa vyama tawala, Emmanuel Ramazani Shadary.

Mgombea urais wa muungano wa vyama tawala anayeungwa mkono na Rais Joseph Kabila, Emmanuel Ramazani Shadary, aliwasili jana mjini Goma akilakiwa na mamia ya wafuasi wake, siku sita tu kabla ya kura kupigwa.

Katika hotuba yake mbele ya raia waliokusanyika kwenye uwanja wa michezo wa Les Volcans, Shadary aliwaahidi vijana kuwapa ajira na kupambana na ufisadi ikiwa atachaguliwa kuwa rais wa nchi hii ambayo kwa miaka kadhaa raia wake wanakabiliwa na changamoto za umasikini na ukosefu wa ajira, licha ya kuongoza kwa utajiri wa madini na rasilimali duniani.

Shadary anasindikizwa kwa ziara yake ya Goma na mke wa Rais Kabila, Olive Lembe, ambaye naye alielezea matumaini mapya kwenye Kongo chini ya mgombea huyo. 

Lakini wakati Shadary na Olive Lembe wakiwahutubia wafuasi wao, vijana kadhaa wanaomuunga mkono Fayulu walikuwa wakiandamana barabarani mjini Goma wakipinga hotuba ya Shadary wakisema anawadanganya Wakongomani. 

Waandishi: Saleh Mwanamilongo akiwa Kinshasa na Benjamin Kasembe akiwa Goma
Wahariri: Iddi Ssessanga/Mohammed Khelef